Bepari Classic: Biashara
Breaking News
Loading...
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo Biashara. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo Biashara. Onyesha machapisho yote

Jumapili, 21 Mei 2017

Jinsi ya Kuanzisha Salon Yenye Faida

Utunzaji wa nywele ni kitu cha kila siku kwenye maisha yetu.Kwenye jamii yetu kila mtu anajali anavyoonekana.Nywele zinaongezea muonekano wa kuvutia.Kuanzia mtoto mpaka mtu mzima wanataka huduma ya kutunza nywele.

Kama unaweza kuhesabu gharama ulizotumia kwa mwaka mzima kutunza nywele utashangaa kwa kiwango kikubwa.Biashara ya salon zipo kila mahali lakini leo tutajifunza jinsi gani unaweza kukabiliana na ushindani huo na kumiliki idadi kubwa ya wateja.

Kabla ya yote kwanini nakushawishi uanzishe biashara ya saloni.
Biashara ya salon unaweza kutenga muda wakufanya huku ukiwa na shughuli nyingine labda jioni tu na weekend(part time job).
Biashara hii unaweza kuiendesha ukiwa nyumbani.
Biashara unaweza kuifanya na biashara nyingine kama kuuza bidhaa za nywele, mafuta ya nywele n.k.
Hauhitaji kubuni bidhaa yako binafsi.

Jinsi ya kufanikiwa katika biashara ya salon.

Unatakiwa uwe na ujuzi mzuri wa salon.Kama wewe ni kinyozi ama msusi utakiwa uwe na utaalamu wa nywele hivyo utakiwa uwaone watu wenye uzoefu katika maswala haya.
Uwe na ukarimu kwa wateja.
Siku macho yako yawaangalie washindani wako.Unatakiwa kuwatawala washindani wako.Unatakiwa ujue mapungufu ya saloni zao na pia nini kinawaimarisha katika saloni zao na ndio utafaidika zaidi.
Huduma nzuri kwa wateja.
Chagua sehemu sahihi.Watu wenye hukosea kuchagua sehemu sahihi, Sehemu sahihi si sehemu isiyo na saloni tu bali sehemu yenye watu wengi na inafikika kwa urahisi.Sehemu yenye wapitaji wengi inayoonekana kwa urahisi.Kuanzisha biashara mpya sehemu isiyo na biashara kama yako ninaweza kuwa hatari ama faida.


Mahitaji.
Kabla ya kuanzisha biashara hii hakikisha una vitu vya msingi kama,


    Curlers
    Hair Brush
    Chana
    Hair Dryer
    Hair Rollers
    Hair Wand
    Hair Waver
    Mkasi
    Straighteners
    Vibanio
     Kioo
     Kiti
    TV kuburudisha  wateja
    Barber Chairs

Kumbuka vifaa vya biashara ya salon inategemea salon ni mahususa kwa jinsia gani.

Biashara nyingine unazoweza kuzifanya pamoja na hii ni:-

Kupaka nywele rangi.(Hair Colouring)
Shampooing.
Kuuza mafuta ya nywele.

Njia nyingine kuvutia wateja ni.

Ukarimu kwa wateja.
Usafi na huduma nzuri.
Punguzo la bei kwa mwezi wa mwanzo.

Jumamosi, 17 Desemba 2016

Mambo Matatu Muhimu Ya Kuzingatia Unapoajiri Wafanyakazi Kwenye Biashara Yako.

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgCJiUlrwQZOTYNomL-twT-pPaDX0MCBHOaYoQCiT9N6UOM7q0vSWy4MDnonkP-OoNUqzQT6b1Qer8I__i2sbN-D95Vaszod5pccTWj9waDgNsMBuaWIVvdm2k5fA3nOrSisgtdRSo_Kw1w/s1600/J.jpg 
Changamoto kubwa ambayo kila mfanyabiashara anaizungumzia ni kupata wafanyakazi bora kwenye biashara zao. Kupata wafanyakazi bora wa kuweza kufanya kazi na kukuza biashara imekuwa changamoto kubwa. Hii ni kwa sababu watu wengi siyo waaminifu na pia hawapo tayari kujifuma ili kuweza kutoa mchango kwenye biashara husika.
Watu wengi wanaoajiriwa wamekuwa wakiangalia namna ya kufanya kazi ndogo iwezekanavyo na wakati huo huo walipwe kiasi kikubwa iwezekanavyo. Watu wameajiri watu ili wawasaidie kukuza biashara zao, kinachotokea wanaziua kabisa. Wengine wameona labda tatizo ni watu wasiowajua, hivyo wakaajiri ndugu na watu wa karibu, bado nao wakaharibu biashara zao.
Hivyo pamoja na changamoto ya wafanyakazi, bado sisi wafanyabiashara pia tuna changamoto katika kuajiri. Tumekuwa tunaangalia vigezo vichache katika kuajiri na kuacha vigezo vingi hivyo kujikuta tunapata wafanyakazi ambao siyo bora.
Wafanyabiashara wengi wanapoajiri wamekuwa wanaangalia vigezo vikuu viwili, uwezo wa mtu kufanya kazi na utayari wa mtu kupokea kipato kidogo. Hivi vigezo vimekuwa vinatumika na wengi na vinawapatia wafanyakazi wenye sifa hizo, ila pia wanakuja na sifa nyingine ambazo wafanyabiashara wanaowaajiri wanakuwa hawajazijua. Sifa hizo ndiyo zinazopelekea biashara nyingi kufa.
Leo tunakwenda kujifunza vigezo vingine muhimu vya kuzingatia pale unapoajiri wafanyakazi kwenye biashara yako. Kigezo cha utayari wa kufanya kazi na kuwa tayari kulipwa mshahara kidogo hatutavijadili kwa sababu wengi tayari wamekuwa wanatumia vigezo hivyo kuajiri.
UAMINIFU ni kigezo muhimu ambacho kila mara unapoajiri lazima ukiangalie. Hata kama mtu anajituma kiasi gani, hata kama yupo tayari kufanya kazi bure, kama hana uaminifu ni mzigo kwenye biashara yako, na ataiua biashara yako. Kuwa na mfanyakazi ambaye siyo mwaminifu ni mzigo mzito kwenye biashara yako, kwa sababu vitendo vyake ambavyo siyo vya uaminifu vitaigharimu biashara. Anaweza kufuja fedha za biashara na hivyo kuleta hasara kwenye biashara. Na hatoishia hapo pekee, anaweza kuwadhulumu wateja wa biashara yako, hivyo kuleta hasara na pia kufukuza wateja wa biashara yako.
Unajuaje uaminifu wa mtu pale unapomwajiri? Kwa kufanya uchunguzi wa kina kabla hujamwajiri mtu. Na pia kuendelea na uchunguzi wako hata baada ya kumwajiri, kwa kuangalia mienendo yake na kauli na matendo yake kama inaendana.
UWEZO WA KUFANYA MAAMUZI ni kigezo kingine muhimu cha kuangalia wakati unaajiri wafanyakazi kwenye biashara yako. Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanawaajiri watu ambao watawasimamia kwa kila kitu, sasa inapotokea wao hawapo kwenye biashara, wafanyakazi wale wanashindwa kufanya maamuzi sahihi. Ajiri watu ambao wana uwezo wa kufanya maamuzi sahihi katika mazingira mbalimbali ya biashara yako. Unapokuwa na watu hawa, unakuwa huna wasiwasi hata pale unapokuwa haupo kwenye biashara yako.
Unawezaje kupima uwezo wa mtu wa kufanya maamuzi? Kwa kufanya usahili mzuri wakati unaajiri, tengeneza maswali na mifano ambayo itakuwezesha kupima uwezo wa mtu wa kufikiri sawasawa na kufanya maamuzi bora. Pia endelea kuwajengea wafanyakazi wako uwezo wa kufanya maamuzi kadiri mnavyokwenda.
MAONO MAKUBWA ni kigezo kingine cha kutumia wakati wa kuajiri. Kama mfanyakazi unayemwajiri hana maono makubwa na maisha yako, ni kwamba hana kitu kinachomsukuma kila siku. Hivyo atakuwa anafanya kazi zake kwa ukawaida, atakuwa hasukumwi kwenda hatua ya ziada. Kwa kifupi atakuwa mzigo kwenye biashara yako.
Unaweza kujua kama mtu ana maono makubwa na maisha yake kwa kumwuliza kuhusu malengo yake ya muda mfupi na ya muda mrefu. Kumuuliza anajiona wapi miaka mitano, 10 na hata 20 ijayo.
Zoezi la kuajiri ni zoezi ambali ni nyeti na muhimu sana kwenye biashara yako. Lipe uzito wa kutosha na lifanye kwa umakini. Kupata wafanyakazi bora wa biashara yako ni zoezi ambalo litakuchukua muda, usikate tamaa, endelea kutafuta na utapata wafanyakazi wazuri.
 Ukijenga utamaduni wa kutembelea mtandao huu kila siku muda si mrefu unakuwa tajiri wa mali, maarifa na afya. Kazi kwako!
 

Jumanne, 13 Desemba 2016

Mambo Matano Yanayokupotezea Muda Kwenye Biashara Yako.

Image result for mafanikio katika biashara
Moja ya rasilimali muhimu unayohitaji ili kukuza biashara yako ni muda. Na kama tunavyojua, hakuna anayeweza kununua muda wa ziada, tuna haya masaa 24 pekee kwa siku. Pamoja na ukomo huu wa muda tulionao, bado wafanyabiashara wengi wamekuwa wanafanya mambo ambayo yanawapotezea muda, kitu ambacho kinazuia biashara zao kukua.
Leo tutaangalia mambo matano unayopenda kufanya na yanakupotezea muda ambao ungeweza kuutumia kukuza biashara yako.
  1. Mikutano isiyo ya lazima.
Kitu kimoja kinachotafuna muda wa biashara ni mikutano isiyo ya lazima wala umuhimu. Kama mfanyabiashara, kuna mikutano mingi utahitaji kufanya na wasaidizi wako na pia kufanya na wafanyabiashara wenzako. Lakini kama utakazana kuhakikisha kila mkutano unashiriki utapoteza muda mwingi. Hii ni kwa sababu mikutano huwa inachukua muda mwingi kuliko inavyotarajiwa, na pia huwa na mambo mengi ambayo siyo muhimu kwako.
Hatua z akuchukua ni punguza mikutano kwenye eneo lako la biashara, hakikisha mnakuwa na mikutano mifupi na yenye tija. Pia punguza idadi ya mikutano ya nje ya biashara ambayo unahudhuria. Haijalishi ni namna gani unataka kuwepo kwenye mikutano ya kibiashara, wewe siyo mfanyabiashara kama huna biashara, hivyo kuza biashara yako.
  1. Mawasiliano yasiyo ya muhimu.
Mara nyingi wafanyabiashara wamekuwa wanajikuta kwenye mawasiliano ambayo siyo muhimu. Wamejikuta wanapokea kila simu ambayo wanapigiwa, kujibu kila ujumbe ambao wanatumiwa, bila kujali wanafanya nini kwa wakati huo. Kama unafanya jukumu muhimu la biashara yako, kuliacha ili kupokea simu ya mtu anayetaka tu kukusalimia ni matumizi mabaya ya muda wako. Mtu kama huyu unaweza kumpigia baadaye kwa ajili ya salamu, ila wakati wa kazi unahitaji kuweka akili na nguvu zako kukuza biashara yako.
Kosa jingine kubwa ni pale mfanyabiashara anapoacha kumhudumia mteja na kuongea na simu, mambo ambayo hayana uhusiano wowote na biashara yake wala kwa wateja wake.
  1. Mitandao ya kijamii.
Hili hatuhitaji kujadili sana, liko wazi ni namna gani matumizi ya mitandao ya kijamii yamekuwa kama ulevi kwa watu wengi. Mitandao ya kijamii imekuwa mingi na usumbufu nao umezidi mara dufu. Wafanyabiashara wengine wamekuwa wanasema wanatumia mitandao hiyo kutangaza biashara zao, lakini ukipima muda wanaotangaza na muda wanazurura kwenye mitandao hiyo, unakuta wanapoteza muda zaidi.
Hatua ya kuchukua ni kupunguza muda unaotumia kwenye mitandao ya kijamii, kuhakikisha unatumia zaidi mitandao hii kukuza biashara yako na siyo kufuatilia maisha ya wengine pekee. Kuwa na kurasa zinazohusu biashara yako kwenye mitandao hii na wape watu maelezo pamoja na kutatua changamoto zao kupitia mitandao hii.
  1. Kulalamika na kulaumu.
Biashara ngumu sana sasa hivi.... ni moja ya kauli ambazo wafanyabiashara wengi wamekuwa wanazitumia. Kadiri wanavyozidi kutumia kauli kama hizi ndivyo wanavyozipokea na kuziamini. Kama biashara ni ngumu unapolalamika unasaidia nini? Hakuna, ni kupoteza tu muda wako.
Usipoteze muda wako kulalamikia ugumu wa biashara yako. Badala yake peleka akili na mawazo yako kwenye hatua unazoweza kuchukua ili kukuza biashara yako katika mazingira magumu unayopitia.
  1. Kutafuta njia za mkato.
Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanadanganyika kwamba ipo njia ya mkato ya kuwawezesha kufanikiwa kwenye biashara, ukweli ni kwamba njia hiyo haipo, na kama ipo huwa haidumu kwa muda mrefu. Watu wamepoteza muda mwingi na fedha nyingi kutafuta njia hii ya mkato kwenye biashara na mwisho kujikuta wakipata hasara.
Acha kabisa kutafuta njia ya mkato kwenye biashara, weka juhudi kwenye biashara uliyochagua kufanya na utapata matunda mazuri.
 Ukijenga utamaduni wa kutembelea mtandao huu kila siku muda si mrefu unakuwa tajiri wa mali, maarifa na afya. Kazi kwako!

Ijumaa, 9 Desemba 2016

Siri Kubwa Ya Mafanikio Kwenye Biashara, Kataa Kukataliwa.

Kitu kimoja ambacho kila mfanyabiashara anakutana nacho kwenye maisha yake ya kibiashara ni kukataliwa. Utakataliwa mara nyingi na kwa mambo mengi kwenye biashara.
Kukataliwa kunaweza kuanza mwanzo kabisa wa biashara yako, pale unapokuja na wazo lako la biashara, watu wakakuambia haiwezekani, au huwezi au utashindwa. Watakupa na mifano kwa nini utashindwa. Kama hujajiandaa na kujipanga vizuri, hutaweza kuvuka hatua hii ya kwanza kabisa, hasa kama wazo lako la biashara ni geni kwa wanaokuzunguka.
Kukataliwa pia kunaendelea wakati unafanya biashara, unaweza kuwa na mipango yako mizuri ya kukuza zaidi biashara ambayo unaifanya, na hivyo ukahitaji msaada na ushirikiano wa wengine. Labda unahitaji kuongeza mtaji wa biashara yako hivyo kuomba mkopo au mchango wa wengine ili kupata mkopo. Hapa pia unaweza kukataliwa na watu au taasisi za kifedha unazohitaji kupata mkopo. Wengine watakupa sababu kwa nini wanakataa, wengine hawatakupa hata sababu.
Kukataliwa pia kunafanywa na wateja wa biashara yako, unaweza kuwa na bidhaa au huduma ambayo unajua kabisa kwamba mtu anaihitaji, unamweleza kuhusu bidhaa hiyo lakini anakataa kununua. Kuna wateja ambao watakupa sababu kwa nini wanakataa, wengine hawatakupa sababu kabisa. Na wale wanaokupa sababu wanaweza kukupa sababu za kweli au za uongo.
Kwa kifupi unapoamua kuingia kwenye biashara, maana yake umeingia kwenye mchezo wa kukataliwa na watu wengi sana. Swali ni je unawezaje kuendesha biashara yako na kufanikiwa katika mazingira haya ya kukataliwa? Hayo ndiyo tunakwenda kujifunza leo kupitia makala haya.
https://encrypted-tbn2.gstatic.com/images?q=tbn:ANd9GcTrhyacwGTfLbnlzymRdnsWJFfKKA3Qp9yPAiYvS_f8VkEDs2As
Njia za kukata kukataliwa kwenye biashara.
Unapokataliwa kwenye biashara, usikubali kirahisi, badala yake na wewe kataa. Ni muhimu ukatae ili uweze kupata kile unachotaka kupitia biashara unayofanya. Zifuatazo ni njia tano za kukataa kukataliwa kwenye biashara.
  1. Waoneshe kwamba wamekosea au hawajui.
Pale unapoamua kuanza biashara na watu wakakuambia kwamba haiwezekani au utashindwa, badala ya kukubaliana nao na kuacha biashara hiyo, jipe dhamira ya kuwaonesha kwamba wamekosea au hawajui kile wanachokisema. Jitoe kwa hali na mali kuweka juhudi kubwa ili uweze kufanikiwa kulingana na mipango yako. Pia angalia ni changamoto zipi ambazo watu wanahofia zitakukwamisha, na zitatue mapema ili zisije kuwa kikwazo kwako kufanikiwa kwenye biashara yako.
Biashara zote kubwa tunazoziona leo, kuna watu waliwahi kusema zisingewezekana, lakini waliozianzisha hawakukata tamaa na sasa zimewezekana.
  1. Jua kwa nini umekataliwa.
Kukataa kukataliwa siyo tu unafanya kwa ubishi, badala yake unaangalia kipi kimefanya ukataliwe na kisha kukirekebisha. Kwa mfano kama umeomba mkopo na ukakataliwa, usikubali tu kwamba huwezi kupewa mkopo huo, badala yake jua kwa nini wamekataa kukupa mkopo. Jua ni mambo gani unayohitaji ili kuweza kupata mkopo huo unaohitaji.
Pia pale mteja anapokukatalia unapomshawishi anunue kwako, jua kwa nini amekataa, labda kuna kitu hajakijua kuhusu bidhaa au huduma yako. Au kuna sehemu nyingine ambapo anapata kilicho bora zaidi ya unachotaka kumuuzia wewe. Ni vyema kujua sababu ili uweze kuifanyia kazi.
  1. Kuwa king’ang’anizi.
Wakati mwingine watu wanakukataa bila hata kujua vizuri ni kipi hasa unahitaji au unataka kuwapa. Wanakuwa hawajajua kile hasa ulichonacho na kwa kuwa hawana muda wa kuchunguza kwa undani, wanaamua kukukataa mara moja. Hapa unahitaji kuwa king’ang’anizi, kuendelea kufanya hata kama umekataliwa. Endelea kuomba hata kama maombi yako yamekataliwa.
Kama ni kuhusu wateja, basi endelea kuwashawishi kununua kwako hata kama wamekataa. Mara nyingi wateja wanahitaji kusikia mara nyingi kutoka kwako ndiyo wafanye maamuzi ya kununua.
  1. Endelea mbele.
Wakati unaendelea kung’ang’ana pale ambapo umekataliwa, pia angalia mbele na fursa unazoweza kupata maeneo mengine. Kama umenyimwa mkopo kwenye taasisi moja, angalia taasisi nyingine ambazo unaweza kuzishawishi na ukapata mkopo. Kama mteja mmoja amekataa, angalia wateja wengine unaoweza kuongea nao kuhusu biashara yako.
  1. Kamwe usikate tamaa.
Hakuna sumu kubwa ya mafanikio kama kukata tamaa. Pale unapoona haiwezekani tena, ndipo unapoagana na mafanikio yako. Usikubali kufikia hatua hii kwenye biashara yako, hata kama mambo yamekuwa magumu kiasi gani. Endelea kuwa na matumaini kwamba mambo yatakuwa vizuri na endelea kuweka juhudi. Hakuna juhudi yoyote unayoweka kwenye biashara yako ambayo inapotea.
Kukubali kukataliwa kwenye biashara ni kuamua kujiondoa kwenye biashara wewe mwenyewe. Kwa vyovyote vile, pambana, hakuna mtu aliyeweza kufanikiwa kwenye biashara kwa urahisi, juhudi ni muhimu.
 Ukijenga utamaduni wa kutembelea mtandao huu kila siku muda si mrefu unakuwa tajiri wa mali, maarifa na afya. Kazi kwako!
 

Jumatatu, 5 Desemba 2016

Aina Mbalimbali za Mitaji ya Kuanzisha Biashara.

Karibu tena mpenzi msomaji wetu wa blogu hii ya BEPARI CLASSIC katika makala nyingine ndani ya mfululizo wetu wa kila siku katika kuhakikisha unapiga hatua kuelekea mafanikio. Leo nitazungumzia suala muhimu sana, suala la kumiliki biashara yako. Ni dhahiri wengi wana kiu kubwa ya kumiliki biashara zao, suala hili kwao limekuwa ni ndoto ya muda mrefu sana.

Suala la kuanzisha biashara limekuwa ndoto kwa sababu changamoto kubwa kwa wengi ni namna gani wanapata mtaji ili watimize haja hiyo ya muda mrefu. Naamini somo hili ni muhimu sana kwako kwa sababu kwa namna moja au nyingine na wewe ulishawahi kuwa na mipango ya kumiliki biashara yako lakini kitendawili kimekuwa wapi utapata mtaji.
Bila shaka usiwe na wasiwasi kwa sababu nitakueleza hatua kwa hatua na hatimaye utaona namna utakavyotimiza ndoto hiyo. Watu wengi wenye mafanikio makubwa ni wale wanaofanya biashara zao. Hawa ni watu wanaotengeneza faida kubwa kuliko ya walioajiriwa. Si kwamba kuajiriwa ni kubaya, la hasha!
Zipo namna nyingi za kupata mtaji wa biashara na ukatimiza ndoto yako nitaelezea moja baada ya nyingine, utachagua njia moja ambayo ni bora kwako. Tuendelee kuwa pamoja.
http://bongoposts.com/wp-content/uploads/2014/09/mtaji-wa-biashara-5.jpg
Moja, unaweza kupata mtaji kwa kukopa. kukopa ni njia moja wapo ya kujipatia mtaji. Unaweza kukopa kutoka kwa mtu unayefaamiana nae au anayetoza riba na ukapata mkopo wa kuanzisha biashara. Changamoto kubwa ya kukopa kwa mtu mara nyingi huwezi kukopa kiasi kikubwa sana. Au unaweza kukopa kutoka kwenye taasisi za kifedha kama benki, katika taasisi za kifedha unaweza kupata kiasi chochote lakini ni lazima uwe na dhamana inayoendana na kiasi unachotaka kukopa.
Lakini kama una dhamana au mtu anayekuamini unaweza kukopa na ukaanza biashara yako.

Mbili, unaweza kuchanga mitaji.Hii pia ni mbinu nzuri ya kupata mtaji wa biashara. Hapa mnaungana wawili au zaidi na mnachanga kiasi kidogo kidogo hadi mnapata kiasi kinachoweza kuwafanya muanze biashara yenu mliyokusudia. Hii ni mbinu mnayoweza kuifanya lakini ni lazima mkubaliane juu ya mambo kadhaa katika hatua za awali. Lazima mkubaliane namna ya kugawana faida, namna ya kuiendesha na kuisimamia biashara. Zaidi ni lazima muwe ni watu wenye lengo linalofanana na makubaliano yote hayo ni lazima muyaweke katika maandishi na kuyasaini pamoja. Mkitumia njia hii ni wazi mnaweza kuanza biashara kubwa kwa kuunganisha nguvu zenu.

Tatu, kuuza mali unazomiliki. Hii pia ni njia ya kupata mtaji wa biashara. Ikiwa una mali yoyote iwe ya kuhamishika au kutokuhamishika unaweza kuiuza na ukatumia fedha hiyo uliyoipata kuanzisha biashara. Mfano unaweza kuuza smartphone ya laki nane au milioni moja, na ukatumia fedha utakayoipata kuanzishia biashara kama biashara hiyo inahitaji mtaji wa laki nane au milioni.
Nne, akiba uliyojiwekea. Unaweza kujiwekea akiba katika kila kipato unachokipata kwa muda fulani na hatimaye ukapata mtaji mkubwa tu wa kuanzisha biashara. Njia hii inahitaji nidhamu kubwa sana ya matumizi yako ya kifedha. Na zaidi ni njia bora lakini inahitaji uvumilivu sana. 

Hizo ni njia nne ambazo zinapatikana katika mazingira yetu ya kawaida. Unaweza kutumia moja kati ya hizo na ukatimiza ndoto zako. Biashara si jambo la kusema tu, ni lazima uamue kuchukua hatua. Ukichukua hatua moja hatua nyingine zisikutishe kwa sababu hatua kubwa ni wewe kudhubutu na kuanza.
Asante kwa kuwa na mimi katika makala hii. Ubarikiwe sana. Usisahau kushare makala hii kwa wengine ili wapate maarifa haya. Kushare bofya vitufe vya mitandao ya kijamii chini ya makala hii.


Ukijenga utamaduni wa kutembelea mtandao huu kila siku muda si mrefu unakuwa tajiri wa mali, maarifa na afya. Kazi kwako!

Jumamosi, 3 Desemba 2016

Hivi ndivyo unavyoweza kuanza biashara hata kama huna mtaji.

http://www.mwananchi.co.tz/image/view/-/3415446/highRes/1460225/-/maxw/600/-/2s24cmz/-/TAJIRI+PICHA.jpg 
Katika makala yetu ya biashara leo, tunakwenda kuangalia changamoto moja ambayo imekuwa inawasumbua wengi. Changamoto hii, siyo changamoto kweli, bali watu wamechagua iwe changamoto na kuitumia kama sababu ya kutokuingia kwenye biashara au kushindwa kukuza biashara zao.
Mara nyingi watu wanapoomba ushauri, kitu cha kwanza wanachotaja ni mtaji. Ninawezaje kuingia kwenye biashara ili hali sina mtaji. Au nitapata wapi mtaji wa kuanza biashara? Maswali na changamoto nyingi zimekuwa zinaanzia kwenye mtaji.
Leo tunakwenda kulijadili hili kwa kina na kuona namna wewe unavyoweza kuanzisha au kukuza biashara yako bila ya kisingizio cha mtaji.
Kabla hatujaangalia namna unavyoweza kuanza biashara hata kama huna mtaji, kwanza tuangalie mtaji ni nini.
Mtaji ni rasilimali ambayo unawekeza kwenye biashara ili iweze kuzalisha faida. Kwa maana hii rahisi ya mtaji, ina maana kwamba mtaji siyo lazima uwe fedha. Kuna vitu vingine vingi ambavyo unaweza kuweka kwenye biashara yako kama mtaji, hata kama kwa sasa huna fedha.
Kwenye makala ya leo tutaziangalia hizi rasilimali ambazo tayari unazo na unaweza kuzitumia kuanzisha biashara yako, hata kama mtaji wa kifedha huna.
Rasilimali ya kwanza ni uaminifu wako.
Hakuna mtaji mkubwa kwenye biashara kama uaminifu. Unapokuwa mwaminifu watu wanakuamini na hivyo kuweza kushirikiana na wewe kwenye jambo lolote unalofanya. Kwa kuwa mwaminifu unatengeneza daraja la kukufikisha mbali zaidi kupitia watu wengine.
Je unawezaje kutumia uaminifu kama mtaji wa kuanza biashara?
  1. Unaweza kuongea na watu wanaokuamini, wakakupa mchango wa fedha ambao utautumia kuanzisha biashara yako. Kwa kuwa tayari wanakuamini, hawatakuwa na wasiwasi juu ya usalama wa fedha zao.
  2. Unaweza kutumia uaminifu wako kupata malighafi au bidhaa za kuwauzia wateja wako hata kama huna fedha. Kwa kuaminika na watu, unaweza kupewa bidhaa ukauze halafu ndipo ulete fedha. Hii yote inaletwa na uaminifu.
  3. Unaweza kutumia fedha za wateja wako kwenda kununua bidhaa au malighafi unazohitaji. Hapa wateja wanakupa fedha kabla hata hujawapa kile wanachotaka. Hii pia inatokana na imani waliyonayo kwako.
Hivyo popote ulipo, jijengee uaminifu, jenga mazingira ya kuaminika na wengine. Uaminifu ni mtaji ambao utakunufaisha sana baadaye.
Rasilimali ya pili; muda.
Muda ni rasilimali kubwa sana unayoweza kuitumia kama mtaji wa kuanzisha biashara. Kama wewe una muda wa kutosha, kwa maana kwamba huna kitu cha kufanya, unaweza kutumia muda huo kuanza biashara yako, au kushirikiana na mtu mwingine ambaye hana muda ila ana fedha.
Unaweza kutumia muda wako vizuri na kuanza biashara ambayo haihitaji mtaji wa kuanzia. Pia unaweza kutumia muda huo kufanya kazi kwa muda kwenye biashara nyingine au maeneo mengine ili kupata mtaji kidogo wa kuanzia. Kwa kuwa na muda una mtaji mkubwa sana, unaweza hata kuanza biashara ambayo ni tofauti na iliyopo kwenye ndoto yako, lengo ni baadaye uweze kuingia kwenye biashara ya ndoto yako.
Rasilimali ya tatu; ujuzi au uzoefu ulionao.
Ujuzi au uzoefu ambao umeupata mkapa sasa, ni mtaji tosha kwako kuanza biashara yako. Ujuzi na uzoefu wako ni mtaji unaoweza kuutumia kutoa huduma au msaada kwa wengine na wao wakakulipa. Kwa kufanya hivi kwa watu wengi unaweza kukusanya mtaji utakaokutosha kuanzisha ile biashara unayotaka kufanya.
Kama ukiweza kuchanganya rasilimali hizi tatu pamoja, yaani ukawa mwaminifu, ukawa na muda halafu ukawa na uzoefu au ujuzi fulani, unaweza kuvitumia kuanzisha biashara kubwa, ambayo haihitaji hata shilingi moja kuanzia.
Angalia hapo ulipo una nini tayari, kisha tumia kuanzisha biashara yako.
 Ukijenga utamaduni wa kutembelea mtandao huu kila siku muda si mrefu unakuwa tajiri wa mali, maarifa na afya. Kazi kwako!