Katika
makala yetu ya biashara leo, tunakwenda kuangalia changamoto moja
ambayo imekuwa inawasumbua wengi. Changamoto hii, siyo changamoto kweli,
bali watu wamechagua iwe changamoto na kuitumia kama sababu ya
kutokuingia kwenye biashara au kushindwa kukuza biashara zao.
Mara
nyingi watu wanapoomba ushauri, kitu cha kwanza wanachotaja ni mtaji.
Ninawezaje kuingia kwenye biashara ili hali sina mtaji. Au nitapata wapi
mtaji wa kuanza biashara? Maswali na changamoto nyingi zimekuwa
zinaanzia kwenye mtaji.
Leo
tunakwenda kulijadili hili kwa kina na kuona namna wewe unavyoweza
kuanzisha au kukuza biashara yako bila ya kisingizio cha mtaji.
Kabla hatujaangalia namna unavyoweza kuanza biashara hata kama huna mtaji, kwanza tuangalie mtaji ni nini.
Mtaji
ni rasilimali ambayo unawekeza kwenye biashara ili iweze kuzalisha
faida. Kwa maana hii rahisi ya mtaji, ina maana kwamba mtaji siyo lazima
uwe fedha. Kuna vitu vingine vingi ambavyo unaweza kuweka kwenye
biashara yako kama mtaji, hata kama kwa sasa huna fedha.
Kwenye
makala ya leo tutaziangalia hizi rasilimali ambazo tayari unazo na
unaweza kuzitumia kuanzisha biashara yako, hata kama mtaji wa kifedha
huna.
Rasilimali ya kwanza ni uaminifu wako.
Hakuna
mtaji mkubwa kwenye biashara kama uaminifu. Unapokuwa mwaminifu watu
wanakuamini na hivyo kuweza kushirikiana na wewe kwenye jambo lolote
unalofanya. Kwa kuwa mwaminifu unatengeneza daraja la kukufikisha mbali
zaidi kupitia watu wengine.
Je unawezaje kutumia uaminifu kama mtaji wa kuanza biashara?
- Unaweza kuongea na watu wanaokuamini, wakakupa mchango wa fedha ambao utautumia kuanzisha biashara yako. Kwa kuwa tayari wanakuamini, hawatakuwa na wasiwasi juu ya usalama wa fedha zao.
- Unaweza kutumia uaminifu wako kupata malighafi au bidhaa za kuwauzia wateja wako hata kama huna fedha. Kwa kuaminika na watu, unaweza kupewa bidhaa ukauze halafu ndipo ulete fedha. Hii yote inaletwa na uaminifu.
- Unaweza kutumia fedha za wateja wako kwenda kununua bidhaa au malighafi unazohitaji. Hapa wateja wanakupa fedha kabla hata hujawapa kile wanachotaka. Hii pia inatokana na imani waliyonayo kwako.
Hivyo
popote ulipo, jijengee uaminifu, jenga mazingira ya kuaminika na
wengine. Uaminifu ni mtaji ambao utakunufaisha sana baadaye.
Rasilimali ya pili; muda.
Muda
ni rasilimali kubwa sana unayoweza kuitumia kama mtaji wa kuanzisha
biashara. Kama wewe una muda wa kutosha, kwa maana kwamba huna kitu cha
kufanya, unaweza kutumia muda huo kuanza biashara yako, au kushirikiana
na mtu mwingine ambaye hana muda ila ana fedha.
Unaweza
kutumia muda wako vizuri na kuanza biashara ambayo haihitaji mtaji wa
kuanzia. Pia unaweza kutumia muda huo kufanya kazi kwa muda kwenye
biashara nyingine au maeneo mengine ili kupata mtaji kidogo wa kuanzia.
Kwa kuwa na muda una mtaji mkubwa sana, unaweza hata kuanza biashara
ambayo ni tofauti na iliyopo kwenye ndoto yako, lengo ni baadaye uweze
kuingia kwenye biashara ya ndoto yako.
Rasilimali ya tatu; ujuzi au uzoefu ulionao.
Ujuzi
au uzoefu ambao umeupata mkapa sasa, ni mtaji tosha kwako kuanza
biashara yako. Ujuzi na uzoefu wako ni mtaji unaoweza kuutumia kutoa
huduma au msaada kwa wengine na wao wakakulipa. Kwa kufanya hivi kwa
watu wengi unaweza kukusanya mtaji utakaokutosha kuanzisha ile biashara
unayotaka kufanya.
Kama
ukiweza kuchanganya rasilimali hizi tatu pamoja, yaani ukawa mwaminifu,
ukawa na muda halafu ukawa na uzoefu au ujuzi fulani, unaweza kuvitumia
kuanzisha biashara kubwa, ambayo haihitaji hata shilingi moja kuanzia.
Angalia hapo ulipo una nini tayari, kisha tumia kuanzisha biashara yako.
Ukijenga utamaduni wa kutembelea mtandao huu kila siku muda si mrefu unakuwa tajiri wa mali, maarifa na afya. Kazi kwako! Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT