Wahenga
wanasema kila zama na kitabu chake, na hapa Tanzania tumekuwa tunapita
kwenye zama mbalimbali, hasa pale tunapobadili viongozi wakubwa wa nchi
yetu, nikiwa nina maana ya rais wa nchi.
Tangu
tumepata kiongozi mpya wa nchi yetu, kumekuwa na mabadiliko makubwa
yanayoendelea kutokea hapa nchini. Mambo mengi yamebadilika tofauti na
tulivyozoea. Na moja ya maeneo ambayo yamebadilika sana ni swala la
ajira.
Tumesikia
na kuona watu wengi ambao wameachishwa kazi (kutumbuliwa), na wengine
ambao wameamua kuacha kazi wenyewe kutokana na mabadiliko haya. Sasa
swali linakuja, nini kinafuata baada ya kuachishwa au kutumbuliwa kwenye
kazi? Je ndiyo maisha yamefika ukomo?
Kwa
watu ambao wamekuwa kwenye ajira kwa muda mrefu, ile taarifa tu ya
kwamba kazi huna tena, inaleta mshtuko mkubwa. Ni hali ya kusikitisha
kwa sababu kitu ambacho mtu alikizoea kinaondoka mara moja.
Lakini
haijalishi umeachishwa au kulazimika kuacha kazi, maisha lazima
yaendelee. Ni lazima uweze kutengeneza kipato cha kufanya maisha yako
yaende vizuri.
Na
hapa ndipo unakuja umuhimu wa kuanza biashara. Kama umeachishwa au
kuacha kazi mwenyewe, njia mpya bora kwako kutengeneza kipato ni
kuanzisha biashara, au kuendeleza kama tayari ulishaanzisha ukiwa bado
umeajiriwa.
Lakini
kama ambavyo wengi tunajua, biashara zina changamoto zake. Hata kama
una mtaji mkubwa kiasi gani, hutaweza tu kuingia kwenye biashara kama
utakavyo wewe na ukafanikiwa. Kuna mambo muhimu ya kuzingatia ili uweze
kuanzisha na kukuza biashara yenye mafanikio.
Kwa leo tujifunze haya muhimu kwako kuzingatia;
- Fanya biashara inayoendana na kazi uliyokuwa unafanya.
Kazi
ambayo ulikuwa unafanya, kuna mambo mengi ambayo unayajua kwa undani.
Kuna vingi unavyovijua ambavyo vitakupunguzia wewe muda wa kujifunza
kama utaanza biashara ya kitu kipya kabisa.
Fanya
biashara inayoendana na uzoefu ulioupata kwenye kazi ambayo ulikuwa
unafanya. Hapa fikiria bidhaa au huduma ambayo unaweza kuitoa kutokana
na uzoefu ambao umeupata kwenye kazi uliyokuwa unafanya.
Tumia kila ambacho umejifunza kwenye kazi yako ya zamani, kuweza kuongeza thamani kwa wengine na wao waweze kukulipa wewe.
- Tumia mtandao uliotengeneza kwenye ajira yako.
Ulipokuwa
kwenye ajira, kuna watu ambao ulijuana nao. Watu hao wanaweza kuwa
muhimu sana kwenye biashara yako mpya uliyoanzisha. Fikiria kila mtu
ambaye umewahi kushirikiana naye wakati umeajiriwa, na ona ni namna gani
anaweza kukusaidia au wewe kumsaidia kupitia biashara mpya
uliyoanzisha.
Kwa
kuweza kutumia mtandao ambao tayari ulikuwa nao, inakupunguzia wewe
ugumu wa kuanza na kuendeleza bishara yako. Kila mtu ambaye
ulishashirikiana naye kwenye kazi kuna namna unaweza kushirikiana naye
kwenye biashara yako. Ni wewe kujua njia hiyo na kuweza kuitumia.
- Kuwa na matumizi mazuri ya fedha zako.
Kwanza
kama una kiasi kikubwa cha fedha ambacho unaanza nacho, unahitaji kuwa
makini sana kwenye matumizi ya fedha hizo. Wengi wamekuwa wakitumia
fedha nyingi kwa mara moja na kujikuta wakiishiwa fedha huku biashara
bado haijasimama. Jua kabisa biashara itahitaji muda kukua na kuweza
kujiendesha yenyewe, hivyo kuwa na matumizi mazuri ya fedha zako.
Pili
kumbuka sasa haupo tena kwenye ajira, ulipokuwa kwenye ajira, kila
mwisho wa mwezi ulikuwa na uhakika wa kupokea mshahara, sasa hivi upo
kwenye biashara, hakuna uhakika wowote hasa kwenye swala la fedha.
Unaweza kutegemea utauza sana lakini usiuze kwa kiwango hicho. Ili
kuepuka hali hii kuathiri maisha yako, hakikisha umetenga fedha kwa
ajili ya kuendesha maisha yako ya kawaida.
Kuachishwa
au kuacha kazi siyo mwisho wa dunia, bali ni fursa nzuri kwako kuweza
kuanzisha biashara ambayo itakuletea uhuru wa kipato baadaye. Yafanyie
kazi mambo haya matatu kwenye biashara unayopanga kuanzisha ili uweze
kuwa na biashara bora na yenye mafanikio.
Ukijenga utamaduni wa kutembelea mtandao huu kila siku muda si mrefu unakuwa tajiri wa mali, maarifa na afya. Kazi kwako! Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT