Changamoto
kubwa ambayo kila mfanyabiashara anaizungumzia ni kupata wafanyakazi
bora kwenye biashara zao. Kupata wafanyakazi bora wa kuweza kufanya kazi
na kukuza biashara imekuwa changamoto kubwa. Hii ni kwa sababu watu
wengi siyo waaminifu na pia hawapo tayari kujifuma ili kuweza kutoa
mchango kwenye biashara husika.
Watu
wengi wanaoajiriwa wamekuwa wakiangalia namna ya kufanya kazi ndogo
iwezekanavyo na wakati huo huo walipwe kiasi kikubwa iwezekanavyo. Watu
wameajiri watu ili wawasaidie kukuza biashara zao, kinachotokea wanaziua
kabisa. Wengine wameona labda tatizo ni watu wasiowajua, hivyo
wakaajiri ndugu na watu wa karibu, bado nao wakaharibu biashara zao.
Hivyo
pamoja na changamoto ya wafanyakazi, bado sisi wafanyabiashara pia tuna
changamoto katika kuajiri. Tumekuwa tunaangalia vigezo vichache katika
kuajiri na kuacha vigezo vingi hivyo kujikuta tunapata wafanyakazi ambao
siyo bora.
Wafanyabiashara
wengi wanapoajiri wamekuwa wanaangalia vigezo vikuu viwili, uwezo wa
mtu kufanya kazi na utayari wa mtu kupokea kipato kidogo. Hivi vigezo
vimekuwa vinatumika na wengi na vinawapatia wafanyakazi wenye sifa hizo,
ila pia wanakuja na sifa nyingine ambazo wafanyabiashara wanaowaajiri
wanakuwa hawajazijua. Sifa hizo ndiyo zinazopelekea biashara nyingi
kufa.
Leo
tunakwenda kujifunza vigezo vingine muhimu vya kuzingatia pale
unapoajiri wafanyakazi kwenye biashara yako. Kigezo cha utayari wa
kufanya kazi na kuwa tayari kulipwa mshahara kidogo hatutavijadili kwa
sababu wengi tayari wamekuwa wanatumia vigezo hivyo kuajiri.
UAMINIFU ni
kigezo muhimu ambacho kila mara unapoajiri lazima ukiangalie. Hata kama
mtu anajituma kiasi gani, hata kama yupo tayari kufanya kazi bure, kama
hana uaminifu ni mzigo kwenye biashara yako, na ataiua biashara yako.
Kuwa na mfanyakazi ambaye siyo mwaminifu ni mzigo mzito kwenye biashara
yako, kwa sababu vitendo vyake ambavyo siyo vya uaminifu vitaigharimu
biashara. Anaweza kufuja fedha za biashara na hivyo kuleta hasara kwenye
biashara. Na hatoishia hapo pekee, anaweza kuwadhulumu wateja wa
biashara yako, hivyo kuleta hasara na pia kufukuza wateja wa biashara
yako.
Unajuaje
uaminifu wa mtu pale unapomwajiri? Kwa kufanya uchunguzi wa kina kabla
hujamwajiri mtu. Na pia kuendelea na uchunguzi wako hata baada ya
kumwajiri, kwa kuangalia mienendo yake na kauli na matendo yake kama
inaendana.
UWEZO WA KUFANYA MAAMUZI ni
kigezo kingine muhimu cha kuangalia wakati unaajiri wafanyakazi kwenye
biashara yako. Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanawaajiri watu ambao
watawasimamia kwa kila kitu, sasa inapotokea wao hawapo kwenye biashara,
wafanyakazi wale wanashindwa kufanya maamuzi sahihi. Ajiri watu ambao
wana uwezo wa kufanya maamuzi sahihi katika mazingira mbalimbali ya
biashara yako. Unapokuwa na watu hawa, unakuwa huna wasiwasi hata pale
unapokuwa haupo kwenye biashara yako.
Unawezaje
kupima uwezo wa mtu wa kufanya maamuzi? Kwa kufanya usahili mzuri
wakati unaajiri, tengeneza maswali na mifano ambayo itakuwezesha kupima
uwezo wa mtu wa kufikiri sawasawa na kufanya maamuzi bora. Pia endelea
kuwajengea wafanyakazi wako uwezo wa kufanya maamuzi kadiri
mnavyokwenda.
MAONO MAKUBWA ni
kigezo kingine cha kutumia wakati wa kuajiri. Kama mfanyakazi
unayemwajiri hana maono makubwa na maisha yako, ni kwamba hana kitu
kinachomsukuma kila siku. Hivyo atakuwa anafanya kazi zake kwa ukawaida,
atakuwa hasukumwi kwenda hatua ya ziada. Kwa kifupi atakuwa mzigo
kwenye biashara yako.
Unaweza
kujua kama mtu ana maono makubwa na maisha yake kwa kumwuliza kuhusu
malengo yake ya muda mfupi na ya muda mrefu. Kumuuliza anajiona wapi
miaka mitano, 10 na hata 20 ijayo.
Zoezi
la kuajiri ni zoezi ambali ni nyeti na muhimu sana kwenye biashara
yako. Lipe uzito wa kutosha na lifanye kwa umakini. Kupata wafanyakazi
bora wa biashara yako ni zoezi ambalo litakuchukua muda, usikate tamaa,
endelea kutafuta na utapata wafanyakazi wazuri.
Ukijenga utamaduni wa kutembelea mtandao huu kila siku muda si mrefu unakuwa tajiri wa mali, maarifa na afya. Kazi kwako! Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT