Mambo Matano Yanayokupotezea Muda Kwenye Biashara Yako. | Bepari Classic
Breaking News
Loading...

Jumanne, 13 Desemba 2016

Mambo Matano Yanayokupotezea Muda Kwenye Biashara Yako.

Image result for mafanikio katika biashara
Moja ya rasilimali muhimu unayohitaji ili kukuza biashara yako ni muda. Na kama tunavyojua, hakuna anayeweza kununua muda wa ziada, tuna haya masaa 24 pekee kwa siku. Pamoja na ukomo huu wa muda tulionao, bado wafanyabiashara wengi wamekuwa wanafanya mambo ambayo yanawapotezea muda, kitu ambacho kinazuia biashara zao kukua.
Leo tutaangalia mambo matano unayopenda kufanya na yanakupotezea muda ambao ungeweza kuutumia kukuza biashara yako.
  1. Mikutano isiyo ya lazima.
Kitu kimoja kinachotafuna muda wa biashara ni mikutano isiyo ya lazima wala umuhimu. Kama mfanyabiashara, kuna mikutano mingi utahitaji kufanya na wasaidizi wako na pia kufanya na wafanyabiashara wenzako. Lakini kama utakazana kuhakikisha kila mkutano unashiriki utapoteza muda mwingi. Hii ni kwa sababu mikutano huwa inachukua muda mwingi kuliko inavyotarajiwa, na pia huwa na mambo mengi ambayo siyo muhimu kwako.
Hatua z akuchukua ni punguza mikutano kwenye eneo lako la biashara, hakikisha mnakuwa na mikutano mifupi na yenye tija. Pia punguza idadi ya mikutano ya nje ya biashara ambayo unahudhuria. Haijalishi ni namna gani unataka kuwepo kwenye mikutano ya kibiashara, wewe siyo mfanyabiashara kama huna biashara, hivyo kuza biashara yako.
  1. Mawasiliano yasiyo ya muhimu.
Mara nyingi wafanyabiashara wamekuwa wanajikuta kwenye mawasiliano ambayo siyo muhimu. Wamejikuta wanapokea kila simu ambayo wanapigiwa, kujibu kila ujumbe ambao wanatumiwa, bila kujali wanafanya nini kwa wakati huo. Kama unafanya jukumu muhimu la biashara yako, kuliacha ili kupokea simu ya mtu anayetaka tu kukusalimia ni matumizi mabaya ya muda wako. Mtu kama huyu unaweza kumpigia baadaye kwa ajili ya salamu, ila wakati wa kazi unahitaji kuweka akili na nguvu zako kukuza biashara yako.
Kosa jingine kubwa ni pale mfanyabiashara anapoacha kumhudumia mteja na kuongea na simu, mambo ambayo hayana uhusiano wowote na biashara yake wala kwa wateja wake.
  1. Mitandao ya kijamii.
Hili hatuhitaji kujadili sana, liko wazi ni namna gani matumizi ya mitandao ya kijamii yamekuwa kama ulevi kwa watu wengi. Mitandao ya kijamii imekuwa mingi na usumbufu nao umezidi mara dufu. Wafanyabiashara wengine wamekuwa wanasema wanatumia mitandao hiyo kutangaza biashara zao, lakini ukipima muda wanaotangaza na muda wanazurura kwenye mitandao hiyo, unakuta wanapoteza muda zaidi.
Hatua ya kuchukua ni kupunguza muda unaotumia kwenye mitandao ya kijamii, kuhakikisha unatumia zaidi mitandao hii kukuza biashara yako na siyo kufuatilia maisha ya wengine pekee. Kuwa na kurasa zinazohusu biashara yako kwenye mitandao hii na wape watu maelezo pamoja na kutatua changamoto zao kupitia mitandao hii.
  1. Kulalamika na kulaumu.
Biashara ngumu sana sasa hivi.... ni moja ya kauli ambazo wafanyabiashara wengi wamekuwa wanazitumia. Kadiri wanavyozidi kutumia kauli kama hizi ndivyo wanavyozipokea na kuziamini. Kama biashara ni ngumu unapolalamika unasaidia nini? Hakuna, ni kupoteza tu muda wako.
Usipoteze muda wako kulalamikia ugumu wa biashara yako. Badala yake peleka akili na mawazo yako kwenye hatua unazoweza kuchukua ili kukuza biashara yako katika mazingira magumu unayopitia.
  1. Kutafuta njia za mkato.
Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanadanganyika kwamba ipo njia ya mkato ya kuwawezesha kufanikiwa kwenye biashara, ukweli ni kwamba njia hiyo haipo, na kama ipo huwa haidumu kwa muda mrefu. Watu wamepoteza muda mwingi na fedha nyingi kutafuta njia hii ya mkato kwenye biashara na mwisho kujikuta wakipata hasara.
Acha kabisa kutafuta njia ya mkato kwenye biashara, weka juhudi kwenye biashara uliyochagua kufanya na utapata matunda mazuri.
 Ukijenga utamaduni wa kutembelea mtandao huu kila siku muda si mrefu unakuwa tajiri wa mali, maarifa na afya. Kazi kwako!

Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT