Karibu tena mpenzi msomaji wetu wa blogu hii ya BEPARI CLASSIC katika makala nyingine ndani ya mfululizo wetu wa kila siku katika kuhakikisha unapiga hatua kuelekea mafanikio. Leo nitazungumzia suala muhimu sana, suala la kumiliki biashara yako. Ni dhahiri wengi wana kiu kubwa ya kumiliki biashara zao, suala hili kwao limekuwa ni ndoto ya muda mrefu sana.
Suala la kuanzisha biashara limekuwa ndoto kwa sababu changamoto kubwa kwa wengi ni namna gani wanapata mtaji ili watimize haja hiyo ya muda mrefu. Naamini somo hili ni muhimu sana kwako kwa sababu kwa namna moja au nyingine na wewe ulishawahi kuwa na mipango ya kumiliki biashara yako lakini kitendawili kimekuwa wapi utapata mtaji.
Bila shaka usiwe na wasiwasi kwa sababu nitakueleza hatua kwa hatua na hatimaye utaona namna utakavyotimiza ndoto hiyo. Watu wengi wenye mafanikio makubwa ni wale wanaofanya biashara zao. Hawa ni watu wanaotengeneza faida kubwa kuliko ya walioajiriwa. Si kwamba kuajiriwa ni kubaya, la hasha!
Zipo namna nyingi za kupata mtaji wa biashara na ukatimiza ndoto yako nitaelezea moja baada ya nyingine, utachagua njia moja ambayo ni bora kwako. Tuendelee kuwa pamoja.
Moja, unaweza kupata mtaji kwa kukopa. kukopa ni njia moja wapo ya kujipatia mtaji. Unaweza kukopa kutoka kwa mtu unayefaamiana nae au anayetoza riba na ukapata mkopo wa kuanzisha biashara. Changamoto kubwa ya kukopa kwa mtu mara nyingi huwezi kukopa kiasi kikubwa sana. Au unaweza kukopa kutoka kwenye taasisi za kifedha kama benki, katika taasisi za kifedha unaweza kupata kiasi chochote lakini ni lazima uwe na dhamana inayoendana na kiasi unachotaka kukopa.
Lakini kama una dhamana au mtu anayekuamini unaweza kukopa na ukaanza biashara yako.
Mbili, unaweza kuchanga mitaji.Hii pia ni mbinu nzuri ya kupata mtaji wa biashara. Hapa mnaungana wawili au zaidi na mnachanga kiasi kidogo kidogo hadi mnapata kiasi kinachoweza kuwafanya muanze biashara yenu mliyokusudia. Hii ni mbinu mnayoweza kuifanya lakini ni lazima mkubaliane juu ya mambo kadhaa katika hatua za awali. Lazima mkubaliane namna ya kugawana faida, namna ya kuiendesha na kuisimamia biashara. Zaidi ni lazima muwe ni watu wenye lengo linalofanana na makubaliano yote hayo ni lazima muyaweke katika maandishi na kuyasaini pamoja. Mkitumia njia hii ni wazi mnaweza kuanza biashara kubwa kwa kuunganisha nguvu zenu.
Tatu, kuuza mali unazomiliki. Hii pia ni njia ya kupata mtaji wa biashara. Ikiwa una mali yoyote iwe ya kuhamishika au kutokuhamishika unaweza kuiuza na ukatumia fedha hiyo uliyoipata kuanzisha biashara. Mfano unaweza kuuza smartphone ya laki nane au milioni moja, na ukatumia fedha utakayoipata kuanzishia biashara kama biashara hiyo inahitaji mtaji wa laki nane au milioni.
Nne, akiba uliyojiwekea. Unaweza kujiwekea akiba katika kila kipato unachokipata kwa muda fulani na hatimaye ukapata mtaji mkubwa tu wa kuanzisha biashara. Njia hii inahitaji nidhamu kubwa sana ya matumizi yako ya kifedha. Na zaidi ni njia bora lakini inahitaji uvumilivu sana.
Hizo ni njia nne ambazo zinapatikana katika mazingira yetu ya kawaida. Unaweza kutumia moja kati ya hizo na ukatimiza ndoto zako. Biashara si jambo la kusema tu, ni lazima uamue kuchukua hatua. Ukichukua hatua moja hatua nyingine zisikutishe kwa sababu hatua kubwa ni wewe kudhubutu na kuanza.
Asante kwa kuwa na mimi katika makala hii. Ubarikiwe sana. Usisahau kushare makala hii kwa wengine ili wapate maarifa haya. Kushare bofya vitufe vya mitandao ya kijamii chini ya makala hii.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT