Kitu
kimoja ambacho kila mfanyabiashara anakutana nacho kwenye maisha yake
ya kibiashara ni kukataliwa. Utakataliwa mara nyingi na kwa mambo mengi
kwenye biashara.
Kukataliwa
kunaweza kuanza mwanzo kabisa wa biashara yako, pale unapokuja na wazo
lako la biashara, watu wakakuambia haiwezekani, au huwezi au utashindwa.
Watakupa na mifano kwa nini utashindwa. Kama hujajiandaa na kujipanga
vizuri, hutaweza kuvuka hatua hii ya kwanza kabisa, hasa kama wazo lako
la biashara ni geni kwa wanaokuzunguka.
Kukataliwa
pia kunaendelea wakati unafanya biashara, unaweza kuwa na mipango yako
mizuri ya kukuza zaidi biashara ambayo unaifanya, na hivyo ukahitaji
msaada na ushirikiano wa wengine. Labda unahitaji kuongeza mtaji wa
biashara yako hivyo kuomba mkopo au mchango wa wengine ili kupata mkopo.
Hapa pia unaweza kukataliwa na watu au taasisi za kifedha unazohitaji
kupata mkopo. Wengine watakupa sababu kwa nini wanakataa, wengine
hawatakupa hata sababu.
Kukataliwa
pia kunafanywa na wateja wa biashara yako, unaweza kuwa na bidhaa au
huduma ambayo unajua kabisa kwamba mtu anaihitaji, unamweleza kuhusu
bidhaa hiyo lakini anakataa kununua. Kuna wateja ambao watakupa sababu
kwa nini wanakataa, wengine hawatakupa sababu kabisa. Na wale wanaokupa
sababu wanaweza kukupa sababu za kweli au za uongo.
Kwa
kifupi unapoamua kuingia kwenye biashara, maana yake umeingia kwenye
mchezo wa kukataliwa na watu wengi sana. Swali ni je unawezaje kuendesha
biashara yako na kufanikiwa katika mazingira haya ya kukataliwa? Hayo
ndiyo tunakwenda kujifunza leo kupitia makala haya.
Njia za kukata kukataliwa kwenye biashara.
Unapokataliwa
kwenye biashara, usikubali kirahisi, badala yake na wewe kataa. Ni
muhimu ukatae ili uweze kupata kile unachotaka kupitia biashara
unayofanya. Zifuatazo ni njia tano za kukataa kukataliwa kwenye
biashara.
- Waoneshe kwamba wamekosea au hawajui.
Pale
unapoamua kuanza biashara na watu wakakuambia kwamba haiwezekani au
utashindwa, badala ya kukubaliana nao na kuacha biashara hiyo, jipe
dhamira ya kuwaonesha kwamba wamekosea au hawajui kile wanachokisema.
Jitoe kwa hali na mali kuweka juhudi kubwa ili uweze kufanikiwa
kulingana na mipango yako. Pia angalia ni changamoto zipi ambazo watu
wanahofia zitakukwamisha, na zitatue mapema ili zisije kuwa kikwazo
kwako kufanikiwa kwenye biashara yako.
Biashara
zote kubwa tunazoziona leo, kuna watu waliwahi kusema zisingewezekana,
lakini waliozianzisha hawakukata tamaa na sasa zimewezekana.
- Jua kwa nini umekataliwa.
Kukataa
kukataliwa siyo tu unafanya kwa ubishi, badala yake unaangalia kipi
kimefanya ukataliwe na kisha kukirekebisha. Kwa mfano kama umeomba mkopo
na ukakataliwa, usikubali tu kwamba huwezi kupewa mkopo huo, badala
yake jua kwa nini wamekataa kukupa mkopo. Jua ni mambo gani unayohitaji
ili kuweza kupata mkopo huo unaohitaji.
Pia
pale mteja anapokukatalia unapomshawishi anunue kwako, jua kwa nini
amekataa, labda kuna kitu hajakijua kuhusu bidhaa au huduma yako. Au
kuna sehemu nyingine ambapo anapata kilicho bora zaidi ya unachotaka
kumuuzia wewe. Ni vyema kujua sababu ili uweze kuifanyia kazi.
- Kuwa king’ang’anizi.
Wakati
mwingine watu wanakukataa bila hata kujua vizuri ni kipi hasa unahitaji
au unataka kuwapa. Wanakuwa hawajajua kile hasa ulichonacho na kwa kuwa
hawana muda wa kuchunguza kwa undani, wanaamua kukukataa mara moja.
Hapa unahitaji kuwa king’ang’anizi, kuendelea kufanya hata kama
umekataliwa. Endelea kuomba hata kama maombi yako yamekataliwa.
Kama
ni kuhusu wateja, basi endelea kuwashawishi kununua kwako hata kama
wamekataa. Mara nyingi wateja wanahitaji kusikia mara nyingi kutoka
kwako ndiyo wafanye maamuzi ya kununua.
- Endelea mbele.
Wakati
unaendelea kung’ang’ana pale ambapo umekataliwa, pia angalia mbele na
fursa unazoweza kupata maeneo mengine. Kama umenyimwa mkopo kwenye
taasisi moja, angalia taasisi nyingine ambazo unaweza kuzishawishi na
ukapata mkopo. Kama mteja mmoja amekataa, angalia wateja wengine
unaoweza kuongea nao kuhusu biashara yako.
- Kamwe usikate tamaa.
Hakuna
sumu kubwa ya mafanikio kama kukata tamaa. Pale unapoona haiwezekani
tena, ndipo unapoagana na mafanikio yako. Usikubali kufikia hatua hii
kwenye biashara yako, hata kama mambo yamekuwa magumu kiasi gani.
Endelea kuwa na matumaini kwamba mambo yatakuwa vizuri na endelea kuweka
juhudi. Hakuna juhudi yoyote unayoweka kwenye biashara yako ambayo
inapotea.
Kukubali
kukataliwa kwenye biashara ni kuamua kujiondoa kwenye biashara wewe
mwenyewe. Kwa vyovyote vile, pambana, hakuna mtu aliyeweza kufanikiwa
kwenye biashara kwa urahisi, juhudi ni muhimu.
Ukijenga utamaduni wa kutembelea mtandao huu kila siku muda si mrefu unakuwa tajiri wa mali, maarifa na afya. Kazi kwako! Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT