Habari rafiki yangu, natumai u mzima katika safari ya mafanikio. Leo nakuleta mbele yako somo muhimu sana katika safari ya mafanikio. Somo litakalokuongoza katika kusaka mafanikio yako. Nitakueleza juu ya tabia muhimu sana ambayo hunabudi kuwa nayo ili uweze kufikia mafanikio makubwa ya ndoto yako.
Ni tabia inayopaswa kujengwa na kila mtu mwenye kiu kubwa ya kufika mbali. Nina uhakika bila kuwa na tabia hii, mafanikio yako siku moja yatakuwa na ukomo. Bila kuwa na atabia hii uwe na hakika utabaki ulivyo au spidi yako ya kufanikiwa itakuwa ndogo sana. Kibaya zaidi kama hutoijenga tabia hii utaendelea kuona wengine wakifanikiwa wewe ukiwa pale pale.
Tabia hii si nyingine, ni tabia ya kupenda kujifunza. Tabia hii ni tabia mama ya waliofanikiwa wote duniani. Watu wenye mafanikio makubwa sana duniani hujifunza kila siku na kila muda wanaopata kufanya hivyo. Tabia itakusaidia kubadilika kimtizamo, kitabia na pia utaanza kuona tumaini mbele yako. Usipokuwa na tabia hii sikudanganyi mafanikio yako ni rahisi kupimwa yatapoishia.
Kujifunza nikuzungumziako mimi si kwa kipindi fulani tu kati hapana. Namaanisha kujifunza kwa maisha yako yote. Jenga mazoea ya kujifunza kila siku, na kila muda unapopatikana. Tabia ya kujifunza ni tabia inayopaswa kuwa kila siku katika maisha yako yote.
Kujifunza ni chakula cha ubongo wako. Ubongo/akili yako inapaswa kulishwa kila siku katika maisha yako. Ni kama mwili ulivyo kila siku unalishwa ili uwe na afya bora. Sasa usipokula kuna uwezekano mkubwa wakuwa na afya dhaifu. Kadhalika na ubongo wako usipolishwa kila siku uwe na hakika utakuwa shida tu.
Swali, nini nijifunze?
Hili ni swali muhimu sana la kujiuliza. Awali ya yote tuone maana halisi ya kujifunza. Kujifunza ni kupata maarifa au/na ujuzi kupitia kusoma, uzoefu au kufundishwa nakadhalika. Kwa maana hiyo kujifunza hapa ni zaidi ya kuwa shuleni, kwa sababu elimu pia ni sehemu ya kujifunza. Kujifunza ni zana pana zaidi.
Na watu wanapotosha hii zana ya kujifunza sana, ndio maana wasomi wengi wakishamaliza shule au vyuo hawasomi au kujighulisha tena juu ya kupata maarifa au ujuzi zaidi. Karne hii ya ishirini na moja mabadiliko yanatokea kwa fujo kubwa, kama husoma ni wazi utaachwa nyuma automatic. Wanaofurahia na kufaidi karne hii wote wanaojifunza kila kukicha.
Hii ni karne ya mapinduzi ya taarifa. Kila siku ni zaidi ya mamilioni ya machapisho na habari mbalimbali zinawekwa kwenye mitandao. Kipindi cha karne ya ishirini na kurudi nyuma watu walijima mafanikio yao kwa mali walizomiliki lakini si sasa tena. Leo katika karne hii, karne ya ishirini na moja mafanikio ni ya wote wanaomiliki maarifa na mawazo bora.
Na mawazo hayo hawayapati kwa bahati mbaya. Wanasoma vitabu sana. Kupitia vitabu unapata maarifa, ujuzi na uzoefu. Sasa wewe kama husomi ni wazi utaendelea kuwa na mawazo yale yale ya kipindi kile, na utashangaa unavyoachwa kwa kasi.
Soma vitabu vinavyokufanya kuwa bora katika eneo au fani yako. Usisome kila kitabu au machapisho, la hasha! Ongeza maarifa na ujuzi kwa kusoma vitabu vya fani yako. Kama weweni mwanamuziki soma vitabu hivyo, kama wewe ni mhasibu jikite kwenye vitabu vya mambo ya biashara na usimamizi wa fedha, kama wewe ni mtaalamu wa kilimo jikite katika vitabu vya kilimo ili uweze kuisaidia jamii katika changamoto za kilimo zinazoikabili.
Kupitia vitabu na machapicho hayo utajua namna ya kuwa ubora katika fani yako na hakuna anayefanya mambo yake kwa ubora asifanikiwe. Kwanza utafanya kila mwenye shida katika fani yako akutafute maana unafahamu mambo mengi kuihusu. Utajua ni kwa namna gani waliofanikiwa katika fani yako walifanya mpaka wakafika walipo. Na faida nyingine nyingi sana.
Kama kweli umejitoa kusaka ndoto yako, basi, anza tabia ya kujisomea kila siku. Anza kwa kutenga walau dakika ishirini tu kulisha ubongo wako kila siku. Utaanza kwa shida lakini taratibu utajikuta unasoma zaidi na zaidi. Nakuhakikishia hutopoteza, utanufaika zaidi. Kama unaona huna muda, sikia punguza dakika ishirini katika muda wako wa kuangalia tv, au wa kuwa kwenye mitandao ya kijamii.
Pia unaweza kujifunza kwa kuhudhuria kwenye semina na mafunzo mbalimbali yanayohusu fani yako. Haya yako mengi sana. Rafiki semina na mafunzo popote yanakotangazwa usiache hiyo fursa ikupite. Kimbilia kwa sababu utaongeza thamani yako kila unapopata maarifa na ujuzi mpya.
Leo waajiri mbalimbali, hawaangalii tena kiwango cha elimu ulichonacho bali wanataka kujua una mawazo na maarifa kiasi gani kusaidia taasisi zao kutimiza malengo. Kama unaendelea kuzunguka na vyeti vyako ukiwa na maarifa yale yale ya chuoni au shuleni nakuambia utasaga soli sana. Anza kujiimarisha kwa kusoma na kushiriki semina na mafunzo kuhusu fani yako.
Faida utakazozipata katika kujisomea vitabu:-
i. Kunaongeza kiwango cha kujiamini mbele ya jamii. Kwa sababu utafahamu mambo mengi.
ii. Kuna kusababisha kupata kazi unayoitaka. Kujisomea kunatoa hakikisho la kujua mambo mengi na hivyo kujiamini, mambo ambayo ni muhimu sana kwa anayetaka kuajiriwa
iii. Kujisomea kunahamasisha kufikia malengo yako.
iv. Kujisomea kunaongeza ujuzi na maarifa katika maisha.
v. Kujisomea vitabu kunakusaidia kufanya mabadiliko makubwa ya tabia, matendo na kuleta mtizamo chanya.
vi. Kujisomea ni njia nzuri yakujitambua na kuweza kuamsha uwezo wako wa ndani uliojificha. vii. Kujisomea kutakusaidia kutumia muda vizuri.
viii. Kujisomea kunaleta mawazo mbadala katika maisha.
Hizo ni baadhi ya faida unazoweza kuzipata kwa kuwa na tabia ya kupenda kujisomea vitabu. Zipo zaidi ya hizo lakini mimi nimechagua hizo kwa leo. Tafadhali usibaki kama ulivyokuwa baada ya kusoma makala hii. Chukua hatua na anza kujiakondisheni kusoma vitabu, kila siku ya Mungu. Asante kwa kuwa nami.
Naomba tuishie hapo mpaka siku nyingine katika makala nyingine. Zipo njia nyingi sana za kujifunza lakini mimi nimekuletea hizi mbili za kusoma vitabu na kuhudhuria mafunzo mbalimbali kwa sababu zina nguvu kubwa ya kukufikisha utakapo. Endelea kusoma makala zetu na usisahau kuzishare kwa wengine. Kushare bonyeza vitufe vya mitandao ya kijamii hapo chini.
Ni mimi mwalimu wako,
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT