Habari za wewe mpenzi msomaji wa makala zetu. Natumai u-mzima wa afya. Karibu tena katika siku nyingine ya kujifunza maarifa mbalimbali katika safari ya mafanikio. Karibuni tuwe wote.
“Fursa za kutajirika zimejificha. Zinapojitokeza huchukuliwa kwanza na watu wenye tabia ya kuweka akiba. Hivyo kuna kila sababu ya kuweka akiba”
Wanaochangamkia fursa na kustawisha maisha yao ni wale wote wenye tabia hii muhimu ya kuweka akiba. Zifuatazo ni mbinu zitakazokusaidia kuanza tabia ya kuweka akiba:-
Moja, tenga asilimia 10 ya kila kipato unachopata kama akiba.Hakikisha kila fedha unayoipata kama kipato kwako unatenga fungu la kumi kama akiba. Tenga fungu la kumi kama akiba kwa kila kiasi unachokipata hata kama ni kidogo kiasi gani. Kama ni mshahara, kila mwenzi weka asilimia kumi pembeni kama akiba. Ukifanya hivi utajikuta taratibu unajenga tabia ya kuweka akiba. Kuna wakati utafika utaweka akiba zaidi ya asilimia 10 kutokana na tabia ya kuweka akiba kujengeka ndani yako. Lakini wewe anza sasa hivi na kiasi hicho kama akiba.
Pili, epukana na matumizi yasio na ulazima. Epuka kabisa kufanya matumizi yasio na ulazima, alafu kama ndiyo unaanza kujenga tabia ya kuweka akiba basi anza kuweka akiba fedha iliyokuwa itumike kwenye matumizi yasio na umuhimu wowote. Kuepuka matumizi yasio na umuhimu kwako jifunze kuchelewesha kufanya matumizi. Kabla ya kufanya matumizi yoyote jiulize kwanza maswalia haya; kwa nini nifanye matumizi haya; nini faida ninayopata kwa matumizi haya, na je hii pesa ya haya matumizi haiwezi kutumika kwenye mambo mengine ya muhimu zaidi? Tabia hiyo ya kujiuliza maswali kabla ya kufanya matumizi yoyote itakusaidia kutadhimini na kujua nini cha muhimu na nini si cha muhimu.
Tatu, anza kuweka akiba kiasi kidogo. Kwa sababu watu wengi hawaweki akiba kwa kisingizio cha kwamba kipato ni kidogo, basi anza kuweka akiba na kiasi kidogo kulingana na kipato unachokipata. Kadri utakavyoweka akiba kwa kiasi kidogo ndivyo utapata nguvu ya kuweka akiba kiasi kikubwa zaidi na zaidi siku zinavyokwenda. Usitake kuweka akiba kiasi kikubwa kama unaanza kwa sababu utashindwa mapema. Usikatishe matumizi yako ya zamani uliyokuwa umeyazoea ghafla. Kukata ghafla ni kuilazimisha akili ikukubalie kuanza tabia mpya bila ya kuizoesha tabia mpya, kufanya hivyo ni hatari. Usifanye hivyo wewe nenda mdogo mdogo. Utapata nguvu zaidi ya kuweka akiba kadri siku zinavyosoge, na itakuja kuwa ni utamaduni wako wa kawaida.
“aliyemwaminifu kwa kidogo ataongezewa bali yeye azuiaye (asiyewekeza) hata kidogo alichonacho(anachosema hakitoshi kuweka akiba wala kuweka akiba) atanyanga’anywa”
Nne, tengeneza mpango wa matumizi. Ili uweke akiba jambo la muhimu sana kwako ni kutengeneza mpango wa matumizi kabla ya kufanya matumizi yoyote ya fedha . Hapa namaanisha lazima ukae chini uchukue kalamu na karatasi. Andika kiasi ulichonacho au unachotegemea kukipata baada ya hapo anza kuorodhesha matumizi muhimu utakayo yafanya na achana kabisa na matumizi yasiyo na umuhimu. Ukishafanya hivyo tenga fedha ya kuweka akiba na kwa ushauri wangu anza na asilimia kumi ya pato lako. Kumbuka nidhamu kwenye hili ni suala la muhimu sana, hakikisha hufanyi matumizi yoyote nje ya mipango uliyojiwekea.
Tano, jenga mtizamo wa kuweka akiba kwenye kila fedha unayoipata. Hapa namaanisha kwamba kila kitu kinaanzia ndani mwetu. Huwezi kuanza kuweka akiba kama huna mtizamo huo. Anza kusema na akili yako na kujiambia ni lazima niweke akiba, fanya hili zoezi mara kwa mara pia anza kusoma vitabu na makala zinazohusu masuala ya fedha. Utaanza kuona mabadiliko katika mtizamo wako. Usikubali taarifa za watu kuwa kipato kidogo hakiwezi weka akiba, puuza na waone kama watu wasiojali hatma zao.
Sita, badili mazingira. Kwa asilimia kubwa mazingira yanachangia kutengeneza tabia na mtizamo ulionao. Hapa nazungumzia marafiki na watu wanaokuzunguka. Watu wanaokuzunguka wana athari kubwa sana katika tabia zako. Ukitaka kuamini hili angalia marafiki zako wote unaoshinda nao kama utaona mwenye ya sana na wewe, angalia kama kuna mwenye tabia ya kuweka akiba, mara zote utakuta wana hali kama wewe au hali mbaya zaidi. Kama ulikuwa unapenda kampani za kula bata acha na anza kutumia huo muda wakula bata kufanya mambo mengine chanya. Ni muhimu sana kubadili mazingira, kwa sababu ugumu wa maisha yako unaujua vizuri wewe mwenyewe, wakati unaangaika unapokosa akiba utakuwepo mwenyewe.
Saba, jiwekee malengo. Wakati mwingine huweki akiba kwa sababu huna malengo au ndoto. Weka malengo ya maisha yako na tengeneza mpango wa kuyafikia. Katika mpango utakaouweka ainisha kiasi cha fedha kitakachohitajika na weka mikakati ya kukipata. Katika hiyo mikakati weka kiasi cha akiba kutoka katika kila kipato unachopata. Usikubali kuishi bila mipango kwa sababu hutajua wapi unataka kufika.
Niishie hapo katika makala hii, kesho nitaendelea na mfululizo wa makala hizi juu ya uwekaji akiba na uwekezaji. Endelea kuwa nasi. Usisahau kushare makala hizi kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza vitufe vya mitandao husika kama vinavyoonekana hapo chini.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT