Rais John Magufuli amefichua sababu za kumuongezea siku nne zaidi
aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Davis
Mwamunyange, akisema kwa kuwa alikuwa nje ya nchi, hakuwa na mtu
anayemwamini kumwachia nafasi hiyo.
Mwamunyange alistaafu rasmi Januari 31, 2017 na alimtaarifu Rais
Magufuli wakati akijiandaa kusafiri kwenda Addis Ababa, Ethiopia
kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika (AU).
Akizungumza wakati wa hafla ya kumwapisha mkuu mpya wa majeshi, Jenerali
Venance Mabeyo iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana, Rais
Magufuli alisema alipata wakati mgumu kuteua mrithi wa Jenerali
Mwamunyange ndani ya siku nne ambazo alisafiri kwani alikuwa bado
hamjui.
“Nilipokuwa nikienda kwenye mkutano wa AU, Jenerali Mwamunyange
aliniambia ‘unajua siku zangu zinaisha tarehe 31 (Januari), sasa
ninafanyaje, naomba umteue anayekuja’. Nikasema ‘sasa nikiondoka leo
nikamteua (mkuu mpya) tarehe 24 (Januari) na wewe unaondoka tarehe 31
(Januari), si wataanza kusema nimekutumbua? Kwa sababu Watanzania
wanajua kubadilisha maneno kweli. Wataanza kusema fulani ametumbuliwa
kabla ya wakati wake na hiyo ndiyo itakuwa stori’,” alisema Rais.
“Lakini nikamwambia mimi nasafiri, ninayekujua ni wewe, ninayemteua
simjui. Sasa nikishamteua ambaye simjui, hizi siku nne ambazo nitakaa
nje itakuwaje?”
Alisema ilibidi amwombe Jenerali Mwamunyange aendelee na wadhifa huo hadi atakaporudi kutoka Ethiopia.
Rais Magufuli alisema akiwa Ethiopia, viongozi wa nchi nyingine walikuwa
wakiulizia nani anayerithi baada ya Mwamunyange kuondoka.
“Nikawa naulizwa nani atakuwa mkuu wa majeshi, naulizwa na watu wa nchi
nyingine, wala si Watanzania. Nikajua kumbe hii nafasi inaangaliwa na
watu wengi,” alisema Rais Magufuli.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT