Imani ni hali ya kuamini kwamba kitu fulani ni kweli. Imani ni hisia au mawazo tuliyojengewa ndani yetu kutoka katika mazingira yaliyotuzunguka. Imani si kitu kinachoonekana. Mara nyingi imani huwa sehemu ya mambo unayoyaamini katika dini yako lakini muda mwingine inaweza kuwa hata masuala ya kisiasa. Naweza kusema imani ni hisia kali au nzito ndani ya mtu.
Na kwa sababu kila kitu kinaanzia ndani ya mtu, ni bayana imani inajenga mtizamo wa mtu katika masuala mbalimbali. Kupitia hisia au mitizamo hiyo unapata tabia ambayo unaiishi kila siku. Kadhalika imani ni hisia juu ya uwepo wa kitu fulani au mtu fulani. Imani hujengwa kwa kusoma, kusikia, kufundishwa au kuona.
Kwa asili ya binadamu wapo watu ambao wanaweza kujenga au kubomoa imani tuliyonayo. Hii linatokana na nafasi walizonazo katika maisha yetu. Wapo watu tunaowaheshimu na kuwaamini sana kiasi cha kwamba tumewaruhusu kupenyeza mawazo na mitizamo yao kutubadilisha na hatimaye na sisi kuamini kama wanavyoamini wao.
Imani yoyote uliyonayo ni kwa sababu uliruhusu siku moja kuwa nayo, namaanisha yaani bila ya wewe kuruhusu usingekuwa nayo. Hivyo kama ni wewe ndio chanzo kikuu cha ujenzi wa imani yako basi amini ni wewe unayeweza kuwa pia chanzo cha kubadili imani yako ya awali.
Nimekuletea somo hili ili kukusaidia kuondoa imani ambazo zimekuwa kikwazo cha mafanikio kwa wengi. Imani inaweza kuwa kikwazo kikubwa cha mafanikio yako. Unaweza kupambana kila kukicha kusaka mafanikio kumbe una mitizamo hasi katika mafanikio. Mafanikio ambayo leo nimeyalenga kuyangumzia hapa ni mafanikio ya kifedha, yaani utajiri.
Imani hizi ambazo ni kikwazo katika mafanikio yako mimi naziita ni imani potofu. Ukiwa na imani nzuri ukaiunganisha na matendo ni dhahiri utapata matokeo stahiki. Sasa zifuatazo ni imani potofu zinazokuzuia kusonga mbele:-
Imani ya Dini Kwamba ni Ngumu kwa Tajiri Kuingia Mbinguni. Hii ni imani iliyojengwa baadhi ya viongozi wa dini kwa watu. Na kwasababu viongozi wa dini ni watu tunaowaheshimu sana na kuaaminiwa na waumini tumewaruhusu kutupatia imani zao hata kama si sahihi kwa mujibu wa Biblia. Dhana hii imejengwa kutokana na mstari unaosema “Ni rahisi ngamia kupenya katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa MUNGU”Marko 10:25; mara nyingine hata si watumishi wa Mungu waliotupandikiza imani hii, bali ni sisi wenyewe kusoma maandiko kishabiki. Imani hii ikimea vilivyo kwako hutojishughulisha na kutafuta uhuru wa kifedha (utajiri) kabisa.
Awali ya yote tambua Mungu wetu ni tajiri sana, ndiye muumba wa vitu vyote. Hivyo haiwezekani akatukatalia kumiliki utajiri. Mungu anatuaambia atatufanikisha popote tuendako anasema “...........nawe utafanikiwa popote uendapo”, Yoshua: 1:7. Hivyo kufanikiwa ni mpango wa mungu kwa mwanadamu.
Hivyo imani ya kwamba tukiwa matajiri hatutaenda mbinguni ni imani potofu. Ukisoma vizuri habari ya tajiri, hiyo niliyoanza nayo hapo juu kutoka kwenye kitabu cha Marko, unapata jibu. Yesu katika habari hiyo anatupa ujumbe ya kwamba kama tutaweka utajiri mbele kuliko Mungu ni wazi mbinguni itakuwa ngumu kufika; anasema “Kwa binadamu haiwezekani, lakini kwa Mungu si hivyo, maana kwa Mungu mambo yote huwezekana.” Marko 10:27 . Badili hiyo Imani, weka juhudi, muamini Mungu lazima ufanikiwe.
Imani Kwamba ili Uwe Tajiri ni Lazima Ufanye Ushirikina. Imani hii inazidi kuwa kikwazo cha mafanikio kwa jamii zetu za kiafrika. Watu wanaamini ili uwe tajiri ni lazima uloge au uwe freemason nakadhalika. Wengi wanakimbilia kwa waganga na hatimaye hakuna wanachopata zaidi ya kuwanufaisha waganga tu. Kwanini hujiulizi iweje mganga atake mimi niwe tajiri wakati yeye anayesema anaweza kunitajirisha ana maisha magumu? Inuka tafadhali, acha kupoteza muda. Huwezi kuwa tajiri bila kujitoa kufanya kazi kwa bidii. Badili huo mtizamo na anza kubadilika kitabia na kimtizamo..
Imani Kwamba Utajiri ni Bahati. Hii ni hisia kali ambayo inapoteza wengi sana. Watu wanaimani ili uwe na utajiri ni mpaka upate bahati. Imani hii pia inachagizwa na wasanii wetu katika sanaa zao, nyimbo na filamu. Na jamii kwa sababu inatumia sana sanaa zao inakuwa rahisi kuamini hivyo kwa sababu sanaa inaweza kuishepu jamii itakavyo. Pia si ajabu ukakuta watu wengi wanacheza kamari na kubet kila kukicha kutokana na kusubiria bahati zao.
Kwanza ni vyema ukaelewa kwamba bahati ni pale fursa inapogongana na maandalizi. Unapaswa kuanza kufanya maandalizi ili siku fursa inapotokea uweze kuitumia ipasavyo. Hakuna bahati katika kufanikiwa chukua hatua ya kupanga na kutimiza ndoto zako. Imani unayopaswa kuisajili upya katika masijala ya akili yako ni kwamba “chochote ninachokita nawezakukipata”.
Imani Kwamba Kabila au Familia Yangu Imelaaniwa. Si kweli hata kidogo kwamba hufanikiwi kutokana na laana ya familia yako au kabila, au kwasababu familia yako hakuna aliyefanikiwa basi mmelaaniwa. Hawakuwa na mafanikio kwa sababu waliishi kama wewe unavyoishi sasa hivi. Huwezi kufanya matendo yale yale wanaofanya wasiofanikiwa alafu utegemee matokeo tofauti (mafanikio), huo unaitwa ni upumbavu. Mshukuru Mungu kwa uwepo wako hapa duniani, amekuumba ili ufanikiwe katika njia zako zote acha kuyaishi maisha ya wenzio kama walizembea ni wao si wewe. Tafadhali badili imani hiyo mara moja.
Habari njema ni kwamba matajiri wengi duniani wametoka katika familia na masikini kabisa lakini walichukua hatua dhidi ya maisha yao na leo ni matajiri wakubwa sana duniani.
Imani Kwamba Ili Uwe Tajiri ni Lazima Uwe Umesoma. Kuwa makini katika hoja hii. Niseme wazi elimu ni kitu kizuri sana katika maisha ya binadamu na hasa hasa katika karne hii. Bila elimu ni wazi zipo changamoto kadha. Uzuri hata kama hukuwa na elimu ya shule unaweza kutafuta elimu na maarifa ili ufanikiwe katika maisha yako kwa sababu kusudi mama la elimu ni kukuwezesha kuishi maisha bora. Kama hukufanikiwa kusoma sio sababu ya wewe kutofanikiwa au kuwa tajiri.
Wapo matajiri wengi mijini hata kusoma na kuandika kwao ni shida lakini wana utajiri mkubwa sana. Hivyo hata wewe kama hukusoma haimaanishi huwezi kufanikiwa kifedha, la hasha! Utajiri unaweza kutengenezwa na mtu yeyote anayejua siri kubwa ya kukuza mtaji wake au kubadilisha maisha ya wenzake. Muhimu hata kama hukusoma endelea kutafuta maarifa kwa kujisomea makala kama hizi zitakazo kusaidia kupata maarifa ya maisha.
Hizi ni baadhi ya imani ambazo zinawazuia wengi kupata utajiri. Ukiwa na imani na zikakujaa vyema ni wazi itakuwa ndoto kufanikiwa. Imani inapounganishwa na matendo ni wazi huleta matokeo chanya, badili imani yako potofu uliyonayo ongeza kutenda utafanikiwa tu. Asante kwakuwa na mimi katika makala yote hii, natumai umefurahia mafundisho yetu haya.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT