Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Flechesmi Mramba, mradi huo umeshaanza na tayari wameshakusanya takwimu kutoka kwa wateja wake wote wa Dar es Salaam na sasa wanaendelea na kazi ya kuhifadhi takwimu hizo katika mifumo ya kompyuta ya Tanesco.
Mramba amesema kuwa mradi huo ambao utatumia mfumo wa GPS, utaweza kutambua kila mteja mahali alipo na matumizi yake ya umeme, lakini pia utatambua kitu chochote kinachoweza kufanywa na mteja katika matumizi yake ya umeme na pia kama kuna mtu anafanya hila kinyume cha utaratibu.
“Huu ni mfumo ambao hata vishoka itakuwa ni rahisi kuwakamata. Ni mfumo ambao utaweza kutambua kila mteja wetu na mahali alipo, na hata kukitokea tatizo tunakwenda moja kwa moja tukitoka ofisini kwetu bila kuhitaji kuuliza alipo mteja,” alifafanua Mramba wakati wa ziara ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari katika miradi ya ukarabati wa miundombinu ya usambazaji umeme jijini Dar es Salaam juzi.
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Tanesco alisema mradi huo unatarajiwa kukamilika mwakani na ni moja ya sehemu ya kuboresha huduma kwa wateja wao, na kwamba tayari wateja walishachukuliwa takwimu zao zote muhimu.
Katika ziara hiyo, Mramba alieleza kuhusu uboreshaji wa vituo hivyo ya usambazaji umeme jijini Dar es Salaam ambavyo ni takriban 32, na tayari baadhi yake vimekamilika na vingine vitakamilika mwakani kwa ufadhili wa Serikali ya Tanzania na washirika wa maendeleo zikiwamo nchi za Finland na Japan.
Wahariri walipata fursa ya kutembelea vituo vya Muhimbili, kituo kipya cha City Centre, kituo cha Sokoine, kituo cha udhibiti wa mifumo yote ya usambazaji umeme cha Mikocheni na Kituo cha Ilala ambavyo vinafanyiwa ukarabati mkubwa na wa kisasa.
Akizungumzia kituo cha udhibiti wa mifumo yote ya usambazaji cha Mikocheni, Mramba alisema kituo hicho kitasaidia kuona matatizo katika vituo mbalimbali vya usambazaji umeme na wataalamu watagundua tatizo na kutoa ufumbuzi wake papo hapo bila kuhitaji kwenda kwa mafundi katika eneo la tukio kama ilivyo sasa.
Kwa kituo cha City Centre, alisema ni cha kisasa na kimejengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Tanzania na Serikali ya Finland kwa gharama ya Sh bilioni 77, na kina njia za kupokea na kusambaza umeme ambazo zinafanya wakati wote umeme upatikane kwani kunapokuwa na hitilafu katika njia mojawapo, inatumika nyingine.
Mtendaji huyo wa Tanesco alieleza kuwa katika kuendana na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwa na uchumi wa kati ambao unajengwa katika viwanda, alieleza kuwa Tanesco inatekeleza miradi mingi ya umeme yenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 5 ukiwamo mradi mkubwa maarufu kama ‘Backbone” wenye gharama ya Sh trilioni moja wa kilovolti 220 kutoka Iringa kwenda Singida hadi Shinyanga ambao pia utalisha mikoa ya Mara, Mwanza, Kilimanjaro, Arusha utakaokamilika mapema mwakani.
“Hii ni miradi mikubwa kufanywa tangu Uhuru. Nina matumaini makubwa na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, siyo matumaini ya kufikirika, kuna ushahidi wa wazi. Hasa katika miradi hii mikubwa ya umeme ambayo itaitanya Tanzania kuwa na nishati ya umeme ya kutosha kuhimili viwanda,” alieleza Mramba.
Kuthibitisha hilo, aliongeza kuwa tayari wameanzisha njia tatu za umeme kwa ajili ya kwenda Mkuranga mkoani Pwani zenye megawati 90 ambazo zitatumiwa na viwanda vilivyoanzishwa na vitakavyoanzishwa katika maeneo hayo kikiwamo cha mfanyabiashara maarufu nchini, Said Salim Bakhresa ambacho kimeshapatiwa umeme tangu Novemba 30, mwaka huu kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kukipatia umeme kiwanda hicho cha juisi za matunda.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT