Leo tunaangalia nguvu ya watu wanaokuzunguka katika
kukufanikisha kibiashara na katika maeneo mengine yote. Ninaposema watu
wanaokuzunguka ninamaanisha wale watu ambao una ukaribu nao,
unaoshirikiana nao katika kazi zako — marafiki, washauri wako, wapambe
na hata wale unaowashirikisha mambo yako — iwe ni mara kwa mara ama kila
siku.
Upo
msemo wa Waingereza usemao, nioneshe marafiki zako nami nitakueleza
wewe ni mtu wa aina gani. Pia msemo mwingine wa Kiswahili unasema ndege
wanaofanana huruka katika kundi moja. Vile vile mwandishi na mzungumzaji
wa kimataifa, Jim Rohn anasema, “Kila mtu ni wastani wa watu watano
ambao hutumia muda mwingi pamoja nao”.
Iko
hivi: tabia, mwenendo na hali ya mtu huakisiwa kupitia wale
anaoshirikiana nao. Machinga utaona marafiki zake wengi ni machinga
wenzie. Mfanyabiashara wa nyama naye atakuwa na marafiki na watu wake
wanaomfanikishia biashara yake.
Hapa
ngoja nikupe mfano wa Mwalimu Yesu Kristo anayefahamika kwa watu wengi.
Kwa mujibu wa maandiko matakatifu tunaona kuwa mwalimu huyu alikuwa na
watu wengi sana anaofahamiana nao katika miji na maeneo alikokuwa
akifanyia shughuli zake.
Alikuwa
na urafiki na viongozi wa kiserikali, alikuwa na urafiki na watu wa
mitaani lakini pia alikuwa akiambatana na watu wanaotambulishwa kama
wanafunzi lakini walikuwapo wafuasi yaani wale ambao walivutiwa na
mafundisho yake na kuamua kumfuata. Watu wake wengine wa karibu walikuwa
ni matajiri wa miji na wenye ushawishi mkubwa mmoja wapo akiwa Yusufu
wa Armataya.
Katika
wanafunzi wake huyu Yesu tunaambiwa alikuwa nao “wengine sabini” ambao
majina yao hayatajwi ijapokuwa tunaona kuwa nao walitumwa kazini. Nini
maana yake? Maana yake ni kwamba hawa sabini hawakuwa karibu sana na
mwalimu huyu kama walivyokuwa wale kumi na wawili ambao kimsingi majina
yao yanajulikana. Hata katika hawa kumi na mbili rekodi zinaonesha kuwa
mwalimu huyu alikuwa na ukaribu zaidi na wanafunzi watatu ambapo kati
yao yupo mmoja aitwaye Petro aliyemwachia uongozi alipoondoka.
Yapo
mambo nataka ujifunze kutokana na mfumo alioutumia mwalimu huyu kuhusu
watu wanaokuzunguka. Rekodi zinatuonesha kuwa alipohitaji msaada kutoka
serikali ya ‘Kirumi’ kuna watu walikuwapo kumsaidia. Alipohitaji fedha
tunaambiwa watu wake wa karibu walimtumikia kwa fedha na mali zao. Hata
alipofariki rafiki yake Yusufu wa Armataya, mtu tajiri na kiongozi
katika baraza la mji ndiye aliyegharimia mazishi yake.
Alipohitaji
kupeleka bidhaa zake (mafundisho) sehemu mbalimbali wakawapo na
“wengine sabini” kwa ajili ya kusaidia kutanua biashara (huduma).
Matajiri wa miji walimpenda kwa sababu mafundisho yake yanathibitisha
namna alivyowafundisha kwa umakini namna ya kuzalisha fedha na kukuza
mitaji yao kiufasaha.
Ninachokueleza
hapa ni kwamba hakikisha unakuwa na marafiki ama watu ambao watasaidia
kukamilisha malengo na mipango yako. Hakikisha unakuwa na mpango
madhubuti wa kutafuta, kujiunganisha na kubanana na marafiki na watu
wenye maana kwako. Lazima uhakikishe kwamba katika kila jambo
unalolihitaji kuwepo na mtu wa uhakika wa kukusaidia ufanikishe.
Huna
sababu ya kung’ang’ana kila siku na watu wanaokurudisha nyuma ama ambao
hawana thamani yoyote wanayoongezea kwako. Unakuwaje na marafiki ama
watu wanaokuzunguka ambao kwa asilimia 90 wanakunyonya? Huyu anakukopa
fedha hakulipi, mwingine hana wazo lolote jipya la kimaendeleo
analokushirikisha, yupo yupo tu!
Hawa
unadirikije kuwaita marafiki zako? Inabidi ulijue hili, ukiona mahali
kuna mtu mmoja anayejiweza katikati ya watu saba, basi uwe na uhakika
kuwa baada ya muda utakuja kukutana na watu saba wasiojiweza kabisa! Kwa
nini? Mtu mmoja anayewakilisha wengine sita watammalizia kila
anachozalisha.
Ndiyo
maana ninashauri mambo mawili. Kwa wale watu ambao ni wategemezi kwako
(ndugu, wazazi n.k) hutakiwi kuwasaidia bali unatakiwa ufanye bidii
kuwawezesha. Pili kwa wale watu ambao wanachagulika (mfano, marafiki),
chagua wale ambao mtakuwa mkiinuana na si wale ambao watakuwa wakikuona
wewe kama kituo cha kupatia misaada.
Usishirikiane
na watu ili kuwaridhisha na wala usiogope kuwatema marafiki na watu
wasiokufaa katika safari yako ya mafanikio. Maisha haya peke yake ni
mzigo mkubwa kuubeba, sembuse kubeba tena furushi na marafiki mizigo!
Kuna wakati inabidi hata uende mbele za Mungu umuombe akutenganishe na
marafiki wanaorudi nyuma na kisha akuunganishe na watu na marafiki
wanaoenda mbele!
Lakini kuna kitu nataka utambue kuhusu ‘levels’
za marafiki na watu wanaokuzunguka. Kuna watu wa karibu na kuna watu wa
ndani. Watu wa karibu wanaweza kuwa ‘wowote’ kutegemea na jambo
unalotaka wakufanikishie lakini watu wa ndani ni lazima (nasisitiza ni
lazima) wawe wale wenye mtazamo, moyo, ari na utayari wa kuhakikisha
mnainuana. Mwalimu Yesu Kristo alikuwa na ukaribu na wanafunzi wote
(wale 12 na wengine 70) lakini lilipokuja suala la kukabidhi uongozi wa
biashara yake alikuwa na “vichwa” vitatu tu, alivyoviamini zaidi.
Kufanikiwa
kibiashara na katika maeneo mbalimbali huhitaji kuwa na ukaribu wa
ndani na watu wengi. Unahitaji watu wachache tu na wakati mwingine hata
mtu mmoja tu ambaye ‘mmeshibana’ kweli kweli na mioyo yenu imeambatana
kwa dhati katika kusaidiana. Kuna mambo yako ambayo si wote wa karibu
yako wanapaswa kuyajua, isipokuwa wale wa ndani.
Jambo
kubwa linalomfanya mtu kuwa na ukaribu ama urafiki na watu wa aina
fulani ni mtazamo wake, ‘unaoendana’ na mtazamo wa watu wa aina hiyo.
Kitakachokuwezesha ukubaliwe katika kundi fulani la watu si ulichonacho
bali ni mtazamo unaokuwa nao. Kwa maana hii, unaweza kuwa na ukaribu ama
urafiki na mtu yeyote kuanzia Ikulu hadi mtaani ikiwa ‘uta-tune’ mtazamo wako kuendana na ule wa unaotaka kuambatana nao.
Mathalani,
kitakachokuunganisha na kundi la matajiri si kiasi cha mali
unachomiliki isipokuwa ni mtazamo unaokuwa nao kuhusu utajiri.
Kitakachokuwezesha kukaa kundi moja na wasomi si wewe kuwa na digrii
nyingi kichwani, isipokuwa ni ule moyo wa kujifunza unaowezesha wasomi
hao kukugawia maarifa.
Unawaza
nini kuhusu utajiri? Unazungumza nini kuhusu matajiri? Namna unavyowaza
kuhusu utajiri ndiko kunakoweza kuuvuta utajiri kukujia ama kuusukuma
utajiri mbali na wewe. Nimekuwa nikiwasikia baadhi ya watu wakisema
maneno haya, “Utajiri mkubwa ni mateso”, “Matajiri hawana amani” na
wengine husema, “Bora niwe na fedha kiasi, zisiwe nyingi wala zisiwe
chache, ziwe wastani”.
Huwezi
kuwaza kuwa utajiri ni mateso halafu utazamie kuwapata marafiki walio
matajiri. Huwezi kunena maneno hasi dhidi ya matajiri, halafu utazamie
kuwa na ukaribu na matajiri. Hapo juu nimekupa baadhi ya kauli ambazo
huwa nazisikia kutoka kwa watu mbalimbali kuhusiana na utajiri na
matajiri.
Uhalisia
ni kwamba ukichunguza maisha ya watu wenye imani kama hizi, utagundua
kuwa watu waliowazunguka nao wana imani kama hizi hizi. Na kwa kuwa
wanaamini kuwa fedha ya wastani ndiyo inayofaa, basi huendelea kufanya
mambo yao, ajira zao, biashara zao kwa vipimo vya wastani. Kufikia
viwango vya juu ni lazima ukutane na watu wanaofikiria viwango vya juu.
Kukutana na kuambatana na watu wanaofikiria viwango vya juu ni lazima
ubadilishe mtazamo wako, uachane na kufikiria ukawaida uanze kufikiria
“u-juu”.
Kagua
marafiki na watu wako wa karibu kisha hakikisha ‘una-pruni’ wasioenda
unakoenda. Mtu anaweza kuwa mwema na mzuri, lakini kama haendi unakoenda
jitenganishe naye kwa sababu ukikomaa kwenda naye, ujue yeye atafika
lakini wewe utakuwa umepotea!
Ukijenga utamaduni wa kutembelea mtandao huu kila siku muda si mrefu unakuwa tajiri wa mali, maarifa na afya. Kazi kwako! Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT