Pombe, shisha saa za kazi, marufuku | Bepari Classic
Breaking News
Loading...

Jumanne, 6 Desemba 2016

Pombe, shisha saa za kazi, marufuku

MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Ayoub Mohamed, amepiga marufuku uuzaji pombe na uvutaji shisha saa za kazi kuanzia Desemba 4.
Akizungumza na waandishi wa habari, alisema serikali ya mkoa imechukua hatua hiyo katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji, uhalifu na kulinda maadili ya vijana visiwani hapo.

Alisema kuanzia sasa, baa zote marufuku kuuza pombe kuanzia asubuhi mpaka saa 9:30 alasiri na yeyote atakayekwenda kinyume, atachukuliwa hatua za kisheria akiwamo muuzaji na mtumiaji.

“Nimepiga marufuku matumizi ya pombe, wakati wa mchana mpaka saa 9:30 alasiri, ndiyo wamiliki wa baa wanaruhusiwa kutoa huduma ya pombe, lakini chakula wanaruhusiwa pamoja na vinywaji vya kawaida,” alisema.

Aidha, alisema ameamua kupiga marufuku matumizi ya shisha katika mkoa wake baada ya kubaini baadhi ya matajiri wakiwachanganya na dawa za kulevya na kusababisha idadi ya watumia dawa za kulevya kuongezeka visiwani humo.

Alisema serikali imeamua kupambana na vitendo vya udhalilishaji wanawake na watoto na kupiga vita biashara ya dawa za kulevya na kuwataka wananchi kushirikiana na serikali kuwafichua watu watakaokwenda kinyume na amri yake ikiwemo ya kupiga marufuku matumizi ya shisha kwa usalama wa afya.

Alisema serikali ya mkoa pia imepiga marufuku upigaji wa muziki katika kumbi za starehe bila ya kufuata sheria na badala yake muziki utapigwa kuanzia saa 2:30 usiku mpaka saa 6 usiku, baada ya waumini wa madhehebu yote kumaliza shughuli za ibada.

Katika hatua nyingine alisema uendeshaji wa pikipiki bila ya kuzingatia sheria maarufu ‘T One’.

“Takwimu zinaonyesha kila wiki kifo kimoja kinatokea kwa waendesha pikipiki wa T One tena vijana wakati ndiyo nguvu kazi ya taifa, lazima Sheria za Usalama Barabarani ziheshimiwe,”alionya.

Aidha, alisema serikali ya mkoa imeamua kupambana na biashara ya ukahaba na madangulo katika kulinda mila na utamaduni wa Zanzibar na vyombo vya ulinzi likiwamo Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa (Masheha) na wilaya watafanya ukaguzi kuhakikisha amri yake inatekelezwa.

Alisema ameamua kuchukua hatua hiyo kwa kutumia sheria namba 8 ya Usalama wa Taifa akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Sheria ya Mwaka 2014 ya Serikali za Mitaa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT