Mwingine aikimbia ACT-Wazalendo | Bepari Classic
Breaking News
Loading...

Jumapili, 11 Desemba 2016

Mwingine aikimbia ACT-Wazalendo

Dar es Salaam. Aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo Kibaha Mjini kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Habib Mchange amekuwa mwanachama wa pili maarufu kujiondoa katika chama hicho kichanga baada ya Moses Machali.

Hatua ya Mchange imekuja ikiwa ni siku 20, baada ya Machali ambaye alikuwa Mbunge wa Kasulu Mjini (2010-2015) kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi aliyehamia ACT-Wazalendo katika uchaguzi wa mwaka jana kujiunga na CCM akidai kuridhishwa na utendaji kazi wa Rais John Magufuli.

Makada hao wanafanya idadi ya viongozi wa chama hicho waliojiondoa kufikia watatu baada ya Aprili 26, kumteua Juma Saanani kuwa Kaimu Katibu Mkuu baada ya aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo, Samson Mwigamba kunga’tuka na kwenda masomoni katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Lakini hali imekuwa tofauti kwa Mchange ambaye alisema jana kuwa amejivua uanachama ili apate muda kufanya na kusimamia shughuli zake za ujasiriamali zinazomhitaji.

“Sasa hivi nita enjoy (furahia). Kwa sababu nipo huru, nitaviangalia vyama vyote vya siasa kuanzia kati, mbele na nyuma,” alieleza Mchange kwa simu.

Awali, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mchange alisema, “Naomba uamuzi wangu huu uheshimiwe.Kamwe nisihusishwe na aina yoyote ya siasa, bali Utanzania wangu. Ningeweza kufanya uamuzi huu kimyakimya, lakini kwa hatua niliyoifikia na ili kuweka kumbukumbu sawa, nimeutoa kwa umma,” alisema.

Mchange amekuwa akijihusisha na harakati za kisiasa na awali alikuwa mwanachama wa Chadema na baadaye ACT-Wazalendo ambako akiwa katika chama hicho kipya alipata kuwa Katibu wa Mipango na Mikakati.

“Natawakia kila la heri waliokuwa wanachama wenzangu wa ACT- Wazalendo katika kuyafikia malengo ya msingi ya uanzishwaji wa chama hiki,” alisema.

Alikitaka chama hicho, kutoingia katika malumbano, kutovunjika moyo, kupendana, kuheshimiana na kuongeza mshikamano ili kufikia malengo.

Ofisa Habari wa chama hicho, Abdallah Khamis alisema wanaheshimu uamuzi wa Mchange kwa sababu ni haki ya kila mtu kujiunga au kujiondoa katika chama chochote cha siasa.

“ACT-Wazalendo inathamini na itaendelea kuthamini mchango wa Mchange kipindi alichokuwapo katika chama hiki. Hatukuwa na ugomvi na punde nimetoka kuongea naye kabla ya kuongea na wewe (mwandishi),” alisema.

Alisema kuondoka kwake hakutakiyumbisha chama hicho kutokana misingi iliyojijengea.

Share this

Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT