Chadema yapongeza upinzani kushinda uchaguzi Ghana | Bepari Classic
Breaking News
Loading...

Jumapili, 11 Desemba 2016

Chadema yapongeza upinzani kushinda uchaguzi Ghana

Dar es Salaam. Siku moja baada ya chama cha upinzani cha Ghana, NPP, kushinda uchaguzi mkuu nchini humo, Chadema kimeibuka na kuwapongeza wananchi wa Ghana kwa uamuzi wao wa kuchagua upinzani.

Katika uchaguzi huo uliofanyika Desemba 9, kiongozi wa NPP, Nana Akufo- Addo aliibuka mshindi na kumbwaga, Rais John Mahama wa chama cha NDC.

“Tunampongeza pia aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Mahama na chama chake cha NDC kwa kukubali matokeo yanayotokana na uamuzi wa Waghana kupitia haki yao ya kikatiba, badala ya kutumia mabavu ya vyombo vya dola na kuminya uhuru wa tume ya uchaguzi, kulazimisha ushindi,” alisema Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene jana.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Ghana, Addo alipata asilimia 53.8 ya kura zote akimshinda Mahama aliyepata asilimia 44.4.

Makene alisema ushindi wa Addo na NPP kwa ujumla ni ushindi wa wananchi wa Ghana uliopatikana kutokana na uchaguzi huru na haki, chini ya mfumo imara.

Alisema Chadema inawapongeza wananchi wa Ghana kwa kuonyesha ukomavu wa kidemokrasia na utawala bora.

Alisema Chadema na NPP vimekuwa vyama rafiki kwa muda mrefu na kuwa ushirikiano wao umeimarika tangu vilipounganishwa kupitia Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Duniani (Idu) na ule wa Afrika (Dua).

“Chadema kama ambavyo imekuwa siku zote tangu kuanza kwa uhusiano kati ya vyama hivi, inakihakikishia chama cha NPP na Rais mteule Addo, ushirikiano wa dhati unaojengwa katika misingi ya urafiki wa imani thabiti katika demokrasia na maendeleo, wakati wote tutakapohitajika kufanya hivyo.” Alisema Makene.

Akizungumzia ushindi huo, aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa alisema moja ya mambo yanayochangia upinzani kushindwa kufanya vizuri katika uchaguzi ni migogoro baina ya ndani ya vyama vyao na chama kimoja dhidi ya kingine.

“Tatizo la upinzani hapa kwetu ni migogoro baina ya kiongozi mmoja na mwingine au kati ya chama na chama hiyo inawafanya wasiwe na ‘political management’ (uongozi wa siasa) nzuri itakayowafanya waweze kushinda, wajenge sera zitakazokubalika na wananchi,” alisema.

Tendwa ambaye ni msuluhishi wa migogoro katika nchi za Umoja wa Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) na Umoja wa Afrika (AU) na mtaalamu wa masuala ya demokrasia na utawala bora, alitolea mfano wa chama cha CUF na kusema mgogoro uliopo unaleta athari kubwa kwa upinzani na kusababisha imani ya wananchi kwa kambi ya upinzani kutoweka.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT