MWENYEKITI WA BODI HIYO, DK. HAROUN KONDO.
SHIRIKA la Posta limepoteza Sh. bilioni tatu kutokana na matumizi
ya mafuta hewa ambayo yalitolewa kwa magari mabovu ya shirika hilo, na
sasa Bodi ya Wakurugenzi imeagiza watendaji waliohusika na ubadhirifu
huo kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua za kisheria mara moja, ikiwamo
kuachishwa kazi.
“Shilingi bilioni tatu zimepotea baada ya kulipwa malipo hewa ya (mafuta) ya magari mabovu ya shirika hili,"alisema Dk. Kondo.
"Watendaji waliohusika lazima wachunguzwe, wakibainika wachukuliwe hatua za kisheria ikiwamo kufukuzwa kazi.
“Hakuna sababu ya kukaa na mtu mwizi kwa sababu akiwa mmoja anaambukiza wengine.
"Hii ni awamu ya tano lazima twende sawa na kasi ya serikali hakuna kufanyakazi kwa mazoea na hakuna kuoneana.”
Bodi ya Wakurugenzi mpya ya Shirika la Posta ilizinduliwa Oktoba 26 na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa.
Katika uzinduzi huo, Waziri Mbarawa aliitaka bodi hiyo kuisimamia vizuri menejimenti ya Shirika la Posta ili ifanye kazi kwa ufanisi mkubwa.
Aidha, alimuagiza mwenyekiti kuwekeana mkakati wa mikataba ya kazi na malengo ili kupata matokeo mazuri na kusimamia huduma mpya ya Posta mlangoni.
Akizungumza jijini jana, Dk. Kondo alisema bodi yake itasaini mkataba na mtendaji mkuu wa makubaliano na utekelezaji wa kuboresha shirika hilo ili liweze kuwa la kibiashara.
Aidha, alisema umefika wakati shirika kufikisha huduma majumbani kwa wateja wao badala ya mfumo wa sasa wa Sanduku la Barua uliopitwa na wakati.
Kabla ya kutangaza ufisadi huo wa Sh. bilioni tatu za mafuta, mapema mwezi huu Bodi hiyo ilielezea waandishi wa habari kubaini matatizo lukuki, ikiwamo mikataba mibovu, idadi kubwa ya wafanyakazi wenye elimu ya chini, rushwa na kuajiri kwa upendeleo.
Kutokana na kugundulika kwa madudu hayo, bodi iliipa miezi sita menejimenti ya kurekebisha kasoro hizo na kinyume na hapo, hatua kali za kisheria zingechukuliwa.
Naye Kaimu Posta Masta Mkuu, Fortunatus Kapinga, alisema jana kuwa shirika lake linaidai serikali pamoja na taasisi mbalimbali zaidi ya Sh. bilioni 9.2 zilizotokana na kutoa huduma mbalimbali pamoja na kodi za majengo.
“Madeni hayo yote yametokana na huduma zinazotolewa na serikali kwa wananchi kupitia shirika letu pamoja na taasisi mbalimbali,” alisema Kapinga.
Imeandikwa na Chauya Adamu na Hellen Mwango
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT