NAIBU KATIBU MKUU WA CHAMA HICHO, MAGDALENA SAKAYA.
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimekaribisha taasisi au watu wenye nia
ya kushauri kutatua mvutano wa viongozi wakuu unaoendelea ndani ya
chama hicho kwa kuwashirikisha viongozi wakuu wa pande mbili wanaovutana
badala ya kuegemea kwa kiongozi mmoja.
Sakaya alikuwa akitolea ufafanuzi juu ya masuala mbalimbali yanayoendelea ndani ya chama hicho.
Aidha, alitoa onyo kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa alivyodai wamekuwa wakiingilia mgogoro huo.
Kauli hiyo ya Sakaya ameitoa ikiwa bado kuna mvutano ndani ya chama hicho unaendelea hususan baina ya Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad na Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba.
Maalim Self pamoja na kundi lake, wanadai kutomtambua Prof. Lipumba kuwa Mwenyekiti wa chama hicho, wakati yeye anajinadi kuwa ni Mwenyekiti halali.
Sakaya alisema mvutano na migogoro iliyopo ndani ya chama hicho, itamalizwa na wanachama wenyewe na si mtu mwingine.
Hata hivyo, alisema kama kuna watu wanaona wana uwezo wa kutatua mgogoro ndani ya chama hicho, wanapaswa kuwaita viongozi hao wote wanaovutana na kuwakalisha pamoja badala ya kuegemea upande mmoja huku upande mwingine ukiendelea kuukandamiza na kuuona haustahili.
“Hivi karibuni baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wamenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari wakisema kuwa watatumia uwezo walionao kuinusuru CUF. Tunapenda kuwaeleza kuwa hawana ubavu wa kufanya hivyo, si wao wala wafadhili wao pamoja na kwamba wanatumika kuchochea mvutano huu,” alisema na kuongeza:
“CUF ni taasisi na siyo chama cha mtu au kikundi cha watu fulani, kwa hiyo tunawasihi viongozi hao na wale wengine wote wanaoingilia na kujifanya wanaweza kutatua mgogoro ndani ya chama chetu kwamba hawana uwezo huo na kama wana nia nzuri wanapaswa kukutanisha pande zote mbili na siyo kuegemea upande mmoja," alisisitiza.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT