Wajumbe hao ambao majina yao yalitangazwa jana wanaamini kuwa iwapo watafanikiwa kuwashawishi wenzao wengine 37 kutoka Chama cha Republican basi watakuwa wamefanikiwa kumzuia bilionea huyo kuingia ikulu.
Desemba 19 wajumbe 538 kutoka majimboni watakutana kupiga kura ya kisheria kumthibitisha Rais mteule anayetarajiwa kuapishwa Januari 20. Kura hizo zitahesabiwa mbele ya Bunge la Congress Januari 6.
Hatua ya wajumbe hao wa Democratic kuanzisha kampeni hiyo imekuja siku chache baada ya makundi ya kiharakati kuanza kukusanya saini nchi nzima ili kuwashinikiza wajumbe hao kutompitisha rais huyo ambaye tayari ameanza kutangaza vipaumbe vyake.
Mmoja wa wajumbe hao aliyetambulika kwa jina la Michael Baca anayewakilisha Colorado amekuwa akizunguka huku na kule kuwashawishi wajumbe wenzake kuepuka kumuunga mkono Trump wakati wa upigaji wa kura.
Mjumbe mwingine ambaye hakupenda jina lake kutajwa alisema kutokana na mvutano unaoendelea kujitokeza sasa kunaweza kuzusha hoja zitakazolazimisha kuangaliwa upya kwa mfumo unaotumika sasa kupitia kura za majimbo kumchagua rais.
Ingawa bado haijajulikana ni wajumbe wangapi wanaendelea kuwa waaminifu kwa kambi ya Trump lakini mchambuzi wa masuala ya siasa, Profesa George Edwards III amesema kama kutatokea wajumbe nane au 10 wakaamua kutomuunga mkono rais huyo mtarajiwa basi kunaweza kubadilisha ndoto za kiongozi huyo kuingia ikulu Januari 20 mwakani.
Tayari wafuasi hao wameitisha kampeni ya kuomba Wamarekani kuwaunga mkono mtandaoni kupitia tovuti ya www.change.org wa kuwashawishi wachaguaji hao kumchagua Clinton badala ya kumthibitisha Trump kwa kuwa hafai kuwa rais wa taifa hilo.
Ujumbe huo unaeleza kuwa iwapo watachagua kama ambavyo majimbo yamepiga kura katika uchaguzi huu, Trump atashinda.
“Hata hivyo, wanaweza kumpigia Hillary Clinton wakiamua,” inasomeka sehemu ya kampeni hiyo yenye kichwa cha habari; “Kura ya uamuzi: Mfanye Hillary Clinton kuwa rais Desemba 19”.
“Hata katika majimbo ambayo wajumbe hawatakiwi kufanya hivyo, wakiamua kura zao zitahesabika, wanaweza wakafanya uamuzi kidogo ambao tutaamini wafuasi wa Clinton watavutiwa nao.”
Mtandao huo unaeleza kuwa Clinton alishinda kura ya wengi hivyo anafaa kuwa rais kwa kuwa Trump alishinda majimbo yenye kura nyingi za majimbo basi mwenendo ukaonyesha bayana kuwa atashinda kura za uamuzi.
Katika uchaguzi uliofanyika Novemba 8 mwaka huu, Wamarekani waliwachagua wagombea wa urais kwa kura ya wengi na kuchagua wapigakura watakaomchagua rais mteule mwezi mmoja ujao.
Clinton aliongoza kura za wengi kwa zaidi ya kura 200,000 lakini Trump aliibuka mshindi kutokana na kushinda majimbo yenye kura nyingi za majimbo.
Ili Rais ashinde kinyang’anyiro hicho, anatakiwa kushinda kura 270 kati ya kura 538 zilizopo kutoka majimboni.
Kwa kutumia mfumo wa mshindi wa jimbo anashinda pia kura za uamuzi. Hadi sasa Trump ana kura 306 wakati mpinzani wake, Clinton akiondoka na kura 232. Ni mara chache kwa Marekani mshindi wa urais kuzidiwa katika kura za wengi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Fordham, Christina Greer alisema kati ya wajumbe 538 watakaopiga kura mwaka huu, 100 ni maseneta ambao ni wawili kila jimbo, wajumbe watatu kutoka makao makuu ya nchi, Washington D.C, na wabunge 435.
“Majimbo yote kasoro mawili ya Maine na Nebraska mgombea mwenye kura nyingi kwenye jimbo basi ndiye mshindi pia wa kura za wajumbe.
“Hii ina maana matokeo yakitoka tu mwenye kura nyingi huwa ni mshindi licha ya kura kusubiri kura za uamuzi Desemba 19,” Dk Dreer.
Hata hivyo, matumaini ya wafuasi hao wa Clinton huenda yasizae matunda kwa kuwa sheria za majimbo mengi likiwamo la Minnesota Marekani zinakataza uwepo wa “wajumbe wasiowaaminifu” na baadhi yanatoza faini kati ya Dola 500 (Sh1 milioni) za Marekani hadi 1,000 (zaidi ya Sh2 milioni).
Faini hiyo ni matokeo ya uamuzi wa Mahakama juu ya nchi hiyo iliamua mwaka 1952 wapigakura hao wawe wanakula viapo mapema wakati wa mkutano mkuu wa chama juu ya nani watamchagua, mtandao wa Factcheck.org unaochapisha habari za siasa, umeeleza.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT