
Sakata la vyeti fedha limemuondoa kazini mhudumu wa chumba cha
kuhifadhia maiti wa hospitali ya Mkoa wa Shinyanga baada ya kukutwa na
cheti cha kughushi.
Katibu tawala wa Shinyanga, Albert Msovela amemtaja mtumishi huyo kuwa
ni Christopher Lwambo na kusema kuwa ndiye pekee katika hospitali hiyo
aliyebainika kuwa na cheti feki.
Msovela amesema hakuna mtumishi mwingine wa umma katika taasisi hiyo
aliyenaswa na cheti bandia na kwamba, huduma zinaendelea vizuri.
Wakati mtumishi huyo akiondolewa, Mwenyekiti wa CCM wilayani Chamwino,
Charles Ulanga ambaye ni mratibu wa elimu wa Kata ya Buigiri ameandika
barua ya kukata rufaa lakini ametakiwa kuipeleka kwa mwajiri wake ambaye
ni mkurugenzi mtendaji wa halmashauri.
“Nilishaandika barua, lakini tulielekezwa kuzipeleka kwa waajiri wetu
ambao wao ndiyo watazifikisha kwa wahusika. Mimi nimeshafanya hivyo,”
amesema Ulanga.
Jina lake lilikuwa miongoni mwa majina yaliyojitokeza katika orodha ya watumishi wanaodaiwa kughushi vyeti.
Hata hivyo, alijitokeza hadharani na kupinga suala hilo akisema alisoma
elimu ya msingi na baadaye ualimu bila ya kupitia elimu ya sekondari na
kuwa ndivyo vyeti alivyowasilisha.
Wakati Ulanga akikata rufaa, Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa
(Talgwu) mkoani Morogoro kimepokea wafanyakazi zaidi ya kumi
wakilalamikia kutotendewa haki.
Katibu wa Talgwu mkoani humo, Lawrence Mdega amesema wafanyakazi hao
walifika ofisini kwake wakilalamika kuwa waliajiriwa kwa elimu ya darasa
la saba, lakini wanashangaa wameandikwa kuwa walimaliza kidato cha nne.
Mkuu wa kitengo cha utawala na fedha wa Chuo Kikuu cha Sokoine (Sua),
Yonica Ndaga amesema watumishi watatu wa chuo hicho wameonyesha nia ya
kukata rufaa wakidai kuonewa na uhakiki uliofanyika ambao haukuwatendea
haki.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT