
SIKU ya Mei 6 mwaka huu (2017) ni kati siku zitakazokumbukwa na wakazi Arusha na Tanzania kwa ujumla wake kwa muda mrefu.
Siku hii imeacha kumbukumbu mbaya kufuatia ajali mbaya ya gari
iliyopoteza uhai wa wanafunzi 33 wa shule ya mchepuo wa Kiingereza ya
Lucky Vicent iliyopo eneo la Kwa Mrombo katika Jiji la Arusha.
Pamoja na wanafunzi hao 33 ambao wote ni wa darasa la saba pia katika
ajali hiyo maisha ya walimu wawili wa shule hiyo, Innocent Pappian na
Julius Mollel na dereva Dismas Kessy, walipoteza maisha hivyo kufanya
idadi ya waliofariki katika ajali kufikia watu 36.
Walionusurika katika ajali hiyo ni wanafunzi wawili wa kike ambao hadi
usiku wa kuamkia leo (Mei 7, 2017) walikuwa wamelazwa katika Hospitali
ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru ambao hata hivyo majina yao hayakuweza
kupatikana mara moja.
Ajali hiyo mbaya ambayo itabaki katika kumbukumbu za ajali mbaya kuwahi
kutokea mkoani Arusha na nchini ilitokea saa 2.30 asubuhi (Mei 6) katika
kijiji cha Rhotia baada ya gari hilo kuacha barabara na kutumbukia
katika korongo la mto Marera, lenye urefu unaokadiriwa kuwa kati ya mita
20 hadi 25.
Wanafunzi hao waliokuwa wakitumia usafiri wa basi la shule aina ya
Toyota Coaster lenye namba za usajili T 872 BYS walikuwa safarini
kuelekea wilayani Karatu, kushiriki mitihani ya ujirani mwema na wenzao
wa shule ya Tumaini Academy iliyopo mjini Karatu.
Basi hilo lilikuwa kati ya mabasi matatu ya shule hiyo yaliyokuwa
yameongozana na taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa gari
iliyopata ajali ilikuwa katikati.
Taarifa kutoka eneo la tukio na chanzo cha ajali
Bado hakuna uhakika wa taarifa rasmi kuhusu chanzo cha ajali hiyo lakini
taarifa zilizopo zinadai kuwa ni kutokana na mfumo wa breki za gari
hilo kushindwa kufanya kazi na hivyo dereva kushindwa kumudu usukani na
gari kutumbukia korongoni.
Aidha taarifa nyingine zinadai kuwa dereva huyo alikuwa katika mwendo
kasi eneo hilo ambalo lina mteremko mkali na kona kali hivyo kushindwa
kuhimili mwendo kasi wa gari lake.
Lakini Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Charles Mkumbo aliwaambia
waandishi wa habari kwamba polisi bado wanachungunza chanzo cha ajali
hiyo na taarifa itatolewa kwa umma uchunguzi huo utakapokamilika.
Taarifa zilizopatika kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa wanafunzi 29
walifariki papo hapo pamoja na walimu wao wawili na dereva wa gari hilo
na kufanya idadi ya waliokufa wakati huo kuwa 32.
Majeruhi walikimbizwa katika hospitali teule ya Wilaya Karatu na kituo
cha afya cha Rhotia ambapo inaelezwa kuwa watatu walifariki dunia
wakati wakipatiwa matibabu katika hospitali teule na majeruhi watatu
walihamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Arusha ambapo mmoja alifariki dunia
saa 10 jioni hivyo kubakia wawili ambao wote ni wasichana.
Habari kutoka kwa mashuhuda wa ajali zinadai kuwa polisi wakishirikiana
na wananchi wa kijiji hicho pamoja na wapita njia walianza uokoaji mara
moja baada ya kutokea kwa ajali.
Kutokana na kuharibika vibaya kwa gari hilo wananchi hao walitumia
mashoka, mitarimbo, nyundo, majembe na vifaa vingine kutoa miili ya
marehemu na majeruhi.
“Hali ilikuwa ya kutisha na kuogofya katika eneo la ajali, miili mingi
iliyotolewa ilikuwa na majeraha makubwa ya kutisha na wengi walikuwa
wamevunjika viungo vyao,” alidai mmoja kati ya waokoaji ambaye hakutaka
kutajwa gazetini.
Majonzi, vilio, Mount Meru Hospitali
Hali ilikuwa ya kusikitisha katika Hospitali ya Mount Meru ambapo vilio,
majonzi, simanzi vilitanda kila kona na kila mmoja wakiwamo madaktari,
wauguzi, viongozi wa serikali na wa kisiasa walionekana kuguswa na
tukio hilo.
Umati mkubwa wa wakazi wa Arusha na vitongoji vyake ulianza kukusanyika
kuanzia saa 6 mchana baada ya taarifa kuzagaa kuwa majeruhi pamoja na
miili ya waliofariki ilikuwa njia kuletwa hospitalini hapo.
Hadi kufikia saa 9 alasiri eneo lote la hospitali lilikuwa limefurika
watu na barabara maarufu ya Afrika Mashariki nayo ilikuwa imefurika
kiasi kwamba magari yalilazimika kupita kwa taabu.
Aidha eneo la kuhifadhia chumba cha maiti nalo lilikuwa limefurika watu
ambao walikuwa wakisubiri kuona na kutambua miili ya wapendwa wao hali
iliyowalazimu polisi wa kikosi cha FFU waliokuwa na silaha nzito
kuimarisha ulinzi.
Ilipotimu saa 9.46 alasiri miili ya majeruhi watatu iliwasili kwa magari
ya kubeba wagonjwa (ambulance) na ndipo viliposikika vilio kutoka kila
kona ya viwanja vya hospitali hiyo.
Baadaye umati huo ulihamia katika eneo la chumba cha kuhifadhia maiti na
miili ilipowasili polisi walishindwa kuthibiti hali kutokana na wazazi
na ndugu wa marehemu kushinikiza kuwa wanataka kutambua miili ya watoto
wao.
Kutokana na hali hiyo, ilimlazimu Mkuu wa Wilaya Arusha, Gabriel
Dagharo, kuingilia kati na kuwataka wale tu waliofiwa waruhusiwe kuingia
ndani ya chumba cha maiti kutambua miili ya watoto wao.
Kauli za viongozi
Akizungumzia tukio hilo Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Dagharro,
alisema binafsi na serikali amesikitishwa na msiba huo na kuongeza kuwa,
serikali iko pamoja na wazazi walipoteza watoto wao.
“Msiba huu umetugusa wote, si msiba wa watu wa Arusha peke yao huu ni
msiba wa taifa na ndiyo maana Rais wetu ametuma salamu za rambirambi kwa
Mkuu wa Mkoa wa Arusha na watu wote wa Arusha,” alisema.
Alisema wakati viongozi wa serikali wakikutana kufanya taratibu za
mazishi kwa kusaidiana na familia ibada ya pamoja ya kuaga miili
itafanyika katika uwanja wa michezo wa Sheikh Amri Abeid siku ya
Jumatatu kuanzia saa 6 za mchana.
Kwa upande wake Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro, alisema anaungana
na wazazi na wanafamilia katika kipindi hiki kigumu cha kupotea kwa
maisha ya wanafunzi hao na walimu wao.
“Hakuna jambo limetuumiza watu wa Arusha kama ajali hii, natoa pole kwa
wazazi na wamiliki wa shule. Naomba tuungane sote bila kujali itikadi
zetu za kisiasa na imani zetu za dini huu msiba ni wetu sote watu wa
Arusha na Watanzania kwa ujumla,” alisema.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Longino Vicent Nkana, aliwaambia
waandishi wa habari kuwa wanafunzi hao waliondoka shuleni hapo saa 12.30
asubuhi kuelekea Karatu kwa ajili ya kushiriki mitihani hiyo ya
ujirani mwema.
Alieleza kuwa wamekuwa wakifanya mitihani hiyo ya ujirani mwema kwa
wanafunzi wa darasa la saba kwa zaidi ya miaka mitatu sasa na hakukuwahi
kutokea tatizo lolote.
“Magari yetu hufanyiwa matengenezo katika karakana zetu mbili kila wiki
na yako salama na hata wakati mwingine tunakodishwa kwa shughuli
nyingine za kijamii,” alifafanua.
Aliongeza kuwa shule hiyo ilianzishwa mwaka 2006 na imekuwa katika shule
bora kitaaluma mkoani Arusha ambapo mwaka 2016 ilishika nafasi ya pili
ngazi ya mkoa katika mitihani ya darasa la saba.
Majina ya waliofariki
Majina ya waliofariki yaliyopatikana ni pamoja na Mteage Amos, Justine
Alex, Irene Kishari, Gladness Goodluck, Praise Roland, Shadrack Biketh,
Junior Mwashuye, Aisha Said, Oumligh Herri Rashid, Gema Gerald, Rebecca
Daudi, Hagai Lucas, Said Ally na Ruth Ndemna.
Wengine ni Atusa Kassim, Neema Eliwashi, Neema Martine, Greyson Robson
Masana, Heavennight Enock, Ian Tarimo Anold Alex, Naomia Hosea, Rukia
Altam, Eliapendo Elihudi, Marion Mrema, Rehema Msuya, Sabrina Said na
Prisca Charles.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT