Mshauri wa Donald Trump ajiuzulu | Bepari Classic
Breaking News
Loading...

Jumanne, 14 Februari 2017

Mshauri wa Donald Trump ajiuzulu

Image result for Michael FlynnMshauri mkuu wa ikulu ya White House kuhusu usalama wa taifa Michael Flynn amejiuzulu kuhusiana na uhusiano wake na maafisa wa Urusi, vyombo vya habari Marekani vinaripoti.
Bw Flynn anadaiwa kujadili vikwazo vya Marekani dhidi ya Urusi akiwa na balozi wa Urusi kabla ya Rais Donald Trump kuingia madarakani.
Anadaiwa kuwapotosha maafisa wa utawala huo mpya kuhusu mazungumzo yake na balozi huyo.
Awali, vyombo vya habari Marekani viliripoti kwamba Wizara ya Haki ilitahadharisha ikulu ya White House mapema kuhusu mawasiliano ya Flynn na maafisa wa Urusi mwishoni mwa mwezi uliopita.
Walisema Bw Flynn huenda akashurutishwa kuwa kibaraka wa urusi.
Maafisa wakuu wa chama cha Democratic walikuwa wametoa wito kwa Bw Flynn kuachishwa kazi.
Mashirika ya habari ya Associated Press na Washington Post yanasema wizara ya haki Marekani ilitahadharisha kuhusu kile ilichosema ni mambo aliyoyasema Bw Flynn kuhusu mazungumzo yake na balozi wa Urusi.
Ni kinyume cha sheria kwa raia wa kawaida kujihusisha na shughuli za kidiplomasia Marekani.
Mazungumzo kati ya Flynn na balozi wa Urusi yanadaiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka jana, kabla ya Bw Flynn kuteuliwa kuhudumu katika uatawala wa Bw Trump.
Bw Flynn, ni luteni jenerali mstaafu.
Awali alikana kuzungumza kuhusu vikwazo dhidi ya Urusi na balozi huyo, na Makamu wa Rais Mike Pence pia alijitokeza hadharani kumtetea.
Bw Flynn baadaye aliambia maafisa wa White House kwamba kuna uwezekano yeye na balozi huyo walizungumzia vikwazo hivyo.
Gazeti la Washington Post lilisema Kaimu Mwanasheria Mkuu Sally Yates aliambia White House kwamba mshauri wao mkuu wa usalama wa taifa "alijiweka katika hali ya hatari" kwa kuzungumza na Warusi kabla yake kuruhusiwa kisheria kufanya hivyo na kwamba Wizara ya Haki ilifahamu kwamba alimpotosha Bw Pence.
Mwezi uliopita, Bi Yates alifutwa kazi na Bw Trump kwa kukataa kutetea marufuku yake dhidi ya raia wa mataifa saba yenye Waislamu wengi kuruhusiwa kuingia Marekani.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT