
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vicent
Mashinji, amesema uchaguzi ujao wanawake watapewa nafasi kubwa ya
kuwakilisha majimboni kutokana na ushindi waliouonyesha Uchaguzi Mkuu
uliopita.
Hayo aliyasema jana Dar es Salaam alipokuwa akifungua mkutano wa Kamati ya Utendaji ya Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha).
Alisema katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2015, wanawake waliopewa
nafasi majimboni kuwania ubunge na uwakilishi walikuwa tisa ambao
walionyesha uwezo mkubwa na kufanikiwa kushinda viti sita.
“Hiyo ni dalili tosha kuwa wanawake ni jeshi kubwa na hata kama
wangepewa wengi nchi nzima, walikuwa na uwezo wa kufanya vizuri zaidi,”
alisema Dk. Mashinji.
Alisema taswira ya chama hicho mitaani ni kwamba kinaongozwa na nguvu
kubwa na hivyo kuwekwa katika nafasi ya kuonekana ni cha wanaume pekee
jambo ambalo si kweli, hivyo ni vyema kuongeza idadi ya wanawake katika
uwakilishi majimboni.
Dk. Mashinji alisema anaamini wanawake watakaopewa nafasi za kuwakilisha
majimbo, watafanya vizuri kwani sio wa kuingia kwa ajili ya kuuza sura
bali ni jeshi la ushindi.
Akizungumzia hali ya kisiasa nchini, Dk. Mashinji alisema Serikali ya
CCM ina lengo la kuzorotesha wapinzani, lakini pamoja na hali hiyo
watakwenda nao sambamba huku wakitumia mbinu ili kuweza kushinda zaidi.
“Pamoja na jitihada za kuizorotesha Chadema na upinzani kwa ujumla kama
wanavyofanya wateule wa rais, wakiwamo wakuu wa mikoa na wilaya kwa
kuwakamata watendaji wa ngazi za chini, kutangaza kuwanyang’anya mihuri
ya kazi, lakini bado kuna nguvu ya kuendelea kuimarisha chama.
“Viongozi wa chini wananyanyaswa, wanapigwa na viongozi wateule wa rais
pasipo sababu na mfano mzuri Iringa, na hata ‘muvi’ ya mihuri
ilitengenezwa ili kuwakomoa Ukawa,’’ alisema Dk. Mashinji.
Alizungumzia pia Ukawa inavyopambana katika chaguzi ndogo kutokana na
CCM kuelezwa kutumia nguvu kubwa ya vyombo vya dola ya kuwakandamiza
wapinzani, huku akitolea mfano uchaguzi mdogo wa ubunge Dimani na
Igunga.
Dk. Mashinji alisema matatizo hayo yatakwisha endapo kutakuwa na Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee, alisema wanawake wa
Chadema walikuwa na nguvu katika uchaguzi uliopita kutokana na matokeo
yake.
Alisema katika ubunge licha ya kupewa nafasi chache za kuwakilisha
majimbo, lakini walifanya vizuri huku akiyaelezea majimbo mawili
yaliyokuwa na mfumo dume lakini wamefanikiwa.
Alisema ishindi wa Esther Bulaya Bunda Mjini na Esther Matiko Tarime
Mjini ni ishara tosha kwamba wanawake ni jeshi kubwa na linaweza
kuongoza na kusimama jimboni na kushinda.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT