Mwonekano wa ukumbi wa mikutano wa kituo hicho.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, ameiagiza Bodi ya Taifa ya Wahasibu na
Wakaguzi wa Hesabu nchini (NBAA) kuwachukulia hatua wale wote wanaoitia
doa taaluma hiyo kwa kufanya ubadhilifu wa fedha za umma.
Maagizo hayo yametolewa kwa niaba yake na Waziri wa Fedha na Mipango,
Dkt. Mpango, wakati wa Uzinduzi wa Kituo cha Taaluma ya Uhasibu (APC)
uliokwenda sambamba na ufunguzi wa Mkutano wa mwaka wa wahasibu
unaojumuisha wadau kutoka nchi za Afrika Mashariki, katika eneo la
Bunju, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Amesema kuwa Idadi ya Wahasibu wenye sifa inazidi kuongezeka na hivyo
kuisaidia Serikali, japo kuwa Serikali hairidhiki kuona wanataaluma wa
Uhasibu na Ukaguzi wa hesabu (CPA) wanaongezeka huku vitendo vya
ubadhilifu wa fedha za Umma na ufisadi vikiendelea kuripotiwa.
“Wapo hata wahasibu wanaotumia taaluma yao vibaya, wanaowawezesha
wafanyabiashara kukwepa kodi, wanachakachua vitabu vya taarifa za fedha
na kufanya ufisadi kwa njia ya kalamu na kompyuta jambo ambalo
halikubaliki hata kidogo” Aliongeza Dkt. Mpango
Amesema kuwa machozi ya masikini wa Tanzania yatawafuata mafisadi hadi
kaburini lakini serikali ya Awamu ya Tano haitasubiri hao mafisadi wafe,
itawatumbua na wala hakuna mzaha na kwamba tayari mahakama ya mafisadi
imeanza kazi na itawashughulikia.
Aidha, Waziri huyo wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amewaasa
wanataaluma wa uhasibu na ukaguzi wa hesabu kuitumia taaluma yao
kuisaidia Serikali katika hatua yake ya kuelekea katika uchumi wa kati
unaotegemea viwanda kwa kuwa taaluma hiyo ina umuhimu mkubwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na
Wakaguzi wa Hesabu, Bw. Pius Maneno amesema kuwa, Kituo hicho
kilichozinduliwa cha APC hadi kumalizika, kitagharimu Sh. Bilioni 35
ambapo mpaka sasa fedha zilizotumika ni takribani Sh. Bilioni 33
“Gharama halisi za ujenzi wa kituo hicho zilikuwa Bilioni 14 lakini
kutokana na mzabuni wa ujenzi kuchelewesha ujenzi ndio maana kumekuwa na
Ongezeko la kiasi hicho cha fedha” aliongeza Bw. Maneno.
Ujenzi wa kituo hicho ambao uko katika eneo lenye ukubwa wa takribani
ekari 14 umehusisha ujenzi wa Kumbi za mikutano zinazochukua zaidi ya
watu 1600, viwanja vya michezo na vyumba vya kisasa 108 vya kulala
wageni.
Bw. Maneno amesema kuwa kujengwa kwa kituo hicho kutaifanya Bodi hiyo
kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kilichokuwa kikitumika kukodi kumbi za
kufanyia na kusahisha mitihani ya Bodi (NBAA).
Amezitaja faida zingine kuwa ni kuboreshwa kwa mazingira ya kitaaluma na
wanataaluma wa uhasibu pamoja na kuimarika kwa utawala bora na kuwa
chachu ya uchumi wa viwanda, kwa kuwa Kituo hicho, kinatoa elimu bora
itakayowawezesha wahitimu kuingia kwenye ushindani ndani ya nchi za
Afrika Mashariki na Duniani kwa ujumla.
Ujenzi wa Kituo hicho umedhaminiwa na serikali kupitia mkopo kutoka
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii-NSSF, Bodi ya Uhasibu-NBAA na Mbia mwenza wa
kituo hicho, Mfuko wa Pensheni ya Watumishi wa Serikali-GEPF.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT