Hata hivyo, baadhi ya maegesho mengine ya jiji hilo malipo hayo yamebaki yakitozwa kwa gharama ya Sh 300, huku viwango vipya vikipokewa kwa malalamiko na watu ambao hutumia maegesho hayo, wakidai kupanda ghafla kwa viwango hivyo bila kutolewa taarifa za kutosha kwa umma.
Akizungumza na gazeti hili jana, Msemaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Gaston Makwembe alisema viwango hivyo vipya vilipitishwa na Baraza la Madiwani tangu mwaka 2014, hata hivyo havikuanza kutumika kwa sababu mbalimbali.
“Viwango hivi sio vipya kabisa, Baraza la Madiwani lilipitisha toka mwaka 2014, lakini sasa ndio tumeamua kuanza kuvitumia, kwanza tulikuwa tunaainisha maegesho yetu, tumeangalia pia uwezo wa wananchi kumudu viwango hivyo,” alieleza Makwembe.
Alisema kampuni ambayo inakusanya tozo ya maegesho ni Kenya Airport Parking System (KAPS) ambayo ilishinda zabuni hiyo na imepewa mkataba wa mwaka mmoja.
Aidha, alisema Kariakoo awali ilikuwa makazi ya watu hivyo walikuwa wakilipa Sh 100, lakini kwa sasa limekuwa ni eneo la kibiashara ndiyo maana imepandishwa na kuwa Sh 500 pamoja na eneo la katikati ya jiji.
“Lengo letu pia ni kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji, magari mengine yanapaki pembezoni tu mwa barabara na kwenye maegesho ya daladala,” alifafanua Makwembe na kuongeza kuwa taratibu zote za kupata kampuni hiyo zilifanyika kwa zabuni kutangazwa, kushindanisha wazabuni mpaka kupatikana kampuni hiyo ambayo ilianza kazi jana.
Aidha, Makwembe alisema; “kuanzia leo wananchi wafahamu tuna wakala mpya wa kukusanya mapato na kwa katikati ya jiji, viwango ndiyo hivyo vilivyoamuliwa watu wanatakiwa kutoa ushirikiano tu.” Alisema wamefuatilia kwa siku ya jana ambapo wameona pamoja na malalamiko ya kiwango hicho cha malipo, lakini hakuna aliyegoma kulipa.
“Awali ilikuwa shilingi mia tatu ambayo ilipitishwa na Baraza la Madiwani mwaka 1998, lakini mwaka 2014 baraza lilipitisha mabadiliko hayo ya kiwango cha tozo la maegesho kwa katikati ya Jiji na Kariakoo. “Suala la kampuni hiyo ni ya kutoka nje, taratibu zote zilifuatwa na akapatikana kampuni ya KAPS tuangalie huduma zake tu, kama hazitaridhisha, zina mapungufu turekebishe na sisi tunaendelea kutoa elimu kwa umma,” alieleza Makwembe.
Alisema kabla ya kuanza kutozwa viwango hivyo vipya, matangazo mbalimbali yalitolewa kupitia vyombo vya habari na pia magari ya vipaza sauti yaliyopita mitaani. Alisema hata hivyo, mbali na katikati ya jiji ambayo ni pamoja na Kariakoo itabaki kuwa Sh 300.
Alisema mpaka sasa Jiji la Dar es Salaam lina maegesho 28,000 na kwamba wanaendelea kuainisha maegesho mengine.
Mwandishi wa habari hizi jana alipita katika baadhi ya maeneo ya katikati ya jiji ambayo ni pamoja na Mtaa wa Samora, fukwe ya mwambao wa bahari ya Hindi katika barabara ya Barack Obama na mitaa mingine na kukuta wafanyakazi wa kampuni hiyo mpya wakitoza Sh 500.
Baadhi ya madereva walilalamikia kiwango hicho, wakidai kuwa imekuwa ghafla kwao kwani hazikutolewa taarifa za kutosha.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT