Vijiji vyote nchini kuwaka umeme Aprili mwakani | Bepari Classic
Breaking News
Loading...

Jumamosi, 17 Desemba 2016

Vijiji vyote nchini kuwaka umeme Aprili mwakani

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali imesaini mkataba kwa ajili ya kukamilisha kuweka umeme katika vijiji 8,000 zilivyosalia katika awamu ya kwanza na ya pili ya Mradi wa Umeme Vijijini (REA).

Amesema wakandarasi hao walisaini mikataba hiyo jana na kwamba Aprili mwakani vijiji hivyo vitakuwa vimeshapata umeme na maeneo ambayo umeme huo hautafika wananchi watafungiwa nishati ya umeme wa jua kwa gharama ile ile ya Sh 27,000 ambayo ni sawa na gharama za umeme wa gridi ya taifa.

Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na watendaji mbalimbali wa idara za serikali wilayani Longido katika ziara yake ya kikazi mkoani Arusha ambapo alisema baada ya miradi hiyo kukamilika, vijiji vyote nchini vitakuwa na umeme.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, umeme huo utawezesha wananchi kujikwamua na hali ngumu ya maisha kwa kubuni miradi mbalimbali ya uzalishaji mali katika maeneo yao.

Aidha, alitumia kikao hicho kumwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Jumaa Mhina kuhakikisha halmashauri hiyo inakuwa na Hospitali ya Wilaya.

“Haiwezekani wilaya kubwa namna hii isiwe na hospitali ya wilaya. Nakuagiza kuanzia sasa kwa kuwa mna kiwanja, majengo ya hospitali yaanze kujengwa kwa kuanza na jengo la utawala, jengo la kupokea wagonjwa na chumba cha dirisha la dawa,” alisema.

Awali, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Sabore Moloimet alimweleza Waziri Mkuu kuwa wameshatenga eneo, lakini uwezo wa halmashauri wa kujenga hospitali ya wilaya ni mdogo kutokana na mapato yake kuwa kidogo.

Hata hivyo, alisema wanajitahidi kuhakikisha watapata fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo ikiwemo kuwashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo kwa pamoja waweze kujenga hospitali hiyo ya wilaya.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT