Ameagiza nguvu hizo wazitumie kwenye maeneo ambayo yanahatarisha usalama wa nchi na wananchi.
Aidha amewaambia wananchi wa Kata ya Bwawani Kitongoji cha Omapinu kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi atafika kijijini hapo wiki ijayo, kuzungumza nao namna ya kutatua mgogoro wa shamba la Tanzania Plantation na wananchi hao.
Waziri Mkuu Majaliwa aliyasema hayo baada ya kusimamishwa na wananchi wa kitongoji hicho, wakati alipokuwa akiendelea na ziara yake mkoani hapa jana.
“Kuanzia sasa ni marufuku kwa watu binafsi wenye uwezo wa fedha kutumia Jeshi la Polisi kuwapiga mabomu na kuwanyanyasa wananchi kwa kuwapiga mabomu wakati hawana silaha. “Polisi wanaruhusiwa kutumia nguvu hizo kwenye maeneo ambayo yanahatarisha usalama wa nchi na wananchi na si vinginevyo,” alisema Waziri Mkuu.
Kuhusu mgogoro wa shamba la Tanzania Plantation, Waziri Mkuu alihoji; “Ni kwanini polisi wawapige mabomu wananchi wanaozuiwa kulima au kuchota maji katika eneo hilo la shamba hadi kufikia hatua ya wanawake kuharibu mimba? “Nyie polisi kwanini mnawapiga mabomu hawa watu, nani anatoa amri ya kupigwa mabomu wananchi hawa. Nasema kuanzia leo msiwapige mabomu watu hawa na pia nawasihi nyie wananchi msifanye fujo, subirini Waziri Lukuvi anakuja wiki ijayo kwa ajili ya kutatua mgogoro huu wa shamba.”
Alisema polisi wanaruhusiwa kutumia nguvu, pale tu panapotokea jambo linaloweza kuhatarisha maisha au vurugu, ila si kuwanyanyasa wananchi wanaodai ardhi yao kwa kuwapiga mabomu.
Alisema Lukuvi atafika mkoani humo kwa ajili ya kushughulikia migogoro ya ardhi, ambayo ipo zaidi wilayani Arumeru, na atakaa muda mwingi kwa ajili ya kutatua kero za wananchi.
Alisema kuanzia sasa mwekezaji ambaye ana mashamba wilayani humo na hayaendelezi, mashamba hayo yatachukuliwa na serikali ili kugawanywa kwa wananchi.
Alisema Waziri Lukuvi akiwa wilayani humo pamoja na kushughulikia migogoro mingine, pia atatatua mgogoro huo baina ya shamba la Tanzania Plantation na wanachi hao.
Awali, Ofisa Ardhi Wilaya ya Arumeru, Rehema Jato alikiri kuwepo kwa mgogoro wa ardhi kati ya mwekezaji wa wa Shamba la Tanzana Plantation, Pradeep Lodhia na wananchi.
Alisema kuna kesi mahakamani na wanachosubiri sasa ni uamuzi wa Mahakama ndipo hatua zingine zichukuliwe. Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti alisema wilaya hiyo ni moja ya wilaya nchini zenye migogoro mingi ya ardhi na wakati mwingine watu wanauana.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT