Uhaba wa abiria Ubungo watishia ajira maelfu | Bepari Classic
Breaking News
Loading...

Ijumaa, 2 Desemba 2016

Uhaba wa abiria Ubungo watishia ajira maelfu


WAKATI sekta mbalimbali zikiwamo za benki, hoteli na shule zikilalamikia kukosa wateja, hali kama hiyo pia ipo kwenye sekta ya usafirishaji ambapo katika Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani cha Ubungo jijini Dar es Salaam

Inadaiwa basi la abiria 60, linaweza kuondoka likiwa na wasafiri 10.

Hali hiyo inatishia ajira za maelfu ya vijana wanaojiajiri kwenye sekta hiyo wakiwamo madereva, utingo na mawakala kutokana na baadhi ya wamiliki wa mabasi kuanza kuuza magari yao.

Licha ya kuwa siyo kawaida hata kwa miezi ya kawaida kupungua kwa abiria kwa kiasi kikubwa, kwenye kipindi hiki cha mwisho wa mwaka, hali imelezwa kuwa tete zaidi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Nipashe, mawakala wa mabasi mbalimbali kwenye kituo hicho, walisema hali ya kutokuwapo kwa abiria imejitokeza karibu kwenye njia zote za safari kasoro Dar-Morogoro.

Makamu Mwenyekiti wa chama cha mawakala wa mabasi, Hassan Msigiti, ambaye pia ni wakala wa kampuni ya Ratco Express, alisema hali iliyopo sasa ni tofauti kabisa na ilivyokuwa mwaka jana kipindi kama hiki.

“Mwaka uliopita, kuanzia Novemba mpaka Desemba magari yalikuwa yanajaa,” alisema.

Naye Meneja wa Kampuni ya Kisbo Express, inayofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na mikoa ya Kanda ya Ziwa, Said Shaban, alisema mwaka jana wakati kama huu walikuwa wanajaza gari siku moja kabla ya safari, jambo ambalo kwa sasa halipo.

Alisema kipindi hiki ndicho kilikuwa fursa kwa kampuni mbalimbali kulipa madeni waliyolimbikiza maeneo mbalimbali, ikiwamo kwenye vituo vya mafuta, jambo ambalo anadhani mwaka huu itakuwa ngumu kulifanya.

Wakati mawakala wa mabasi yanayofanya safari za kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya mbali 'wakilia njaa', Wakala wa Kampuni ya Mabasi ya Abood, Said Mbata, alisema kwa upande wao, safari za Morogoro hazijaathirika.

“Tunasafirisha kwa siku mabasi 10 hadi 15 na yote yanajaa, kwangu mimi nasafirisha abiria wa Morogoro na ni mkoa wa karibu," alisema Mbata.

"Wanaolalamika kuwa abiria wachache ni wale wa safari za mbali kama Mwanza au sehemu nyingine.
"Huko abiria ni wa kutafuta.”

Karani wa Kampuni ya Mabasi Hai Express, Raymond Lewis, alisema suala la abiria linategemea na kampuni yenyewe lakini akaeleza kuwa abiria wengi wanaofika ofisini kwake kipindi hiki wamekuwa wakiomba kupunguziwa nauli, wakilalamika kuwa hali ya maisha ni ngumu.

KILIO CHA MURO
Lewis aliongeza kuwa miaka miwili iliyopita walikuwa wanasafirisha magari yote ya kampuni yao kila siku lakini kwa sasa wanaweza kusafirisha mabasi mawiili hadi matatu na huku yakiwa na upungufu wa wastani wa abiria 10.

Hivi karibuni mmiliki wa kampuni ya Muro Investiment, Maggid Muro, alitangaza kuuza mabasi yake 18 kutokana na kile alichokiita uendeshaji wa biashara kuwa mgumu.

Muro alisema kutokana na hali hiyo, anatarajia kupunguza wafanyakazi 60 kati ya 110 wanaofanya kazi kwenye kampuni yake, inayomiliki pia vituo vya mafuta.

“Ni kweli tunauza, naondoa magari kama 18 hivi na vituo vya mafuta viwili au vitatu, inategemea na bei nitakayoipata, bei ikiwa nzuri nitauza vituo vitatu," alikaririwa akisema.

“Biashara hakuna, biashara imekuwa ngumu sana, yaani hakuna kinachowezekana, sasa unaumia kichwa, unahangaika na vitu vingi, pesa hakuna, sasa tunajaribu kupunguza baadhi ya wafanyakazi pamoja na biashara, napunguza wafanyakazi kama 60.”

Muro ambaye anamiliki mabasi zaidi ya 40, alisema kwa ujumla biashara zimekuwa mbaya na kwamba basi la abiria 60 wakati mwingine linasafiri na abiria 20.

“Na basi la kupeleka ruti tatu au nne kwa siku linaondoka halijai, nafikiri sasa hivi mtu akifiwa na mzazi ndiyo anasafiri, lakini sijui mama mdogo, wanaambiana nenda tu, wanachangiana,” alisema Muro.

Alisema katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka, ‘booking’ (kukata tiketi mapema) nyingi zilikuwa zikifanyika kwa ruti kama Bukoba, Musoma na Mwanza na zilikuwa zinajaa mapema hadi tarehe za mwanzoni mwa mwezi wa 12 kuelekea sikuku za Krismasi na Mwaka Mpya, lakini kwa sasa hakuna.

Aidha, katika mahojiano na gazeti hili hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), Mustafa Mwalongo, alisema wapo wanachama wake ambao hali zao zimeyumba, lakini bado chama hicho hakijakutana kujadili jinsi ya kuwasaidia.

“Suala hilo liko wazi, tunalijua. Tutakutana kujadili nini cha kufanya ili kuwanusuru wafanyabiashara wenzetu,” alisema.

Katika bajeti yake ya kwanza iliyojadiliwa kwenye Bunge la Bajeti lililoanza Aprili 19 hadi Juni 30, mwaka huu, serikali ya awamu ya tano imepanga kutumia Sh. trilioni 29.53 kwa mwaka 2016/17.

Kati ya fedha hizo, Sh. trilioni 17.72 zitakuwa za matumizi ya kawaida, wakati Sh. trilioni 11.82, sawa na asilimia 40 ya bajeti nzima, zitatumika kwa shughuli za maendeleo.

Uamuzi huo wa serikali umefyeka mabilioni ya shilingi yaliyokuwa yanatafunwa kupitia bajeti kubwa ya matumizi ya kawaida iliyokuwa inapangwa katika miaka iliyotangulia.

Katika bajeti ya mwaka jana (2015/16), kwa mfano, Bunge liliidhinisha Sh. trilioni 22.45. Kati yake, Sh. trilioni 16.7 zikiwa ni za matumizi ya kawaida ambayo ni sawa na asilimia 74.3 huku Sh. trilioni 5.76, sawa na asilimia 25.7 zikiwa za shughuli za maendeleo.

Imeandikwa na Mariam Hassan na Mary Mafuru (TSJ)
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT