Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (BLM), Issa Haji Gavu, alipokua akijibu swali la Mwakilishi wa Mfenesini, Machano Othman Said, katika kikao cha Baraza la Wawakilishi jana.
Alisema sheria namba 2 ya 2012 imeanzishwa kwa madhumuni ya kuwaenzi na kuwatunza viongozi wastaafu Zanzibar kwa kutambua mchango wao katika kulitumikia taifa na wananchi wake.
“Sheria hii haikuzungumzia suala la kuwakataza viongozi hao kutogombea nafasi nyengine za uongozi katika serikali kupitia vyama vyao baada ya kustaafu.”
"Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi lazima mfahamu suala la kuchagua na kuchaguliwa ni haki ya kikatiba kwa kila mwananchi aliyefikia vigezo vilivyowekwa kwa mujibu wa kifungu cha 26 (a) (d) cha Katiba ya Zanzibar ya 1984.
Wakati huu serikali haioni busara ya kuwabana kisheria viongozi wa kisiasa wastaafu wasitumie fursa yao ya kikatiba kugombea uongozi pale wanapoona inafaa,” alisema Gavu.
Aidha, waziri huyo alisema haki ya kuwalipa viongozi wa kisiasa wastaafu ni jambo la kisheria na halitokani na utashi, hivyo serikali itaendelea kuwalipa na kuwapa haki zao nyengine viongozi hao kama sheria ilivyosema.
Pia alisema serikali haina wazo la kuwa na baraza la ushauri la viongozi wastaafu kwani Rais hakwaziki kutaka ushauri kwa mtu yoyote na wala halazimiki kufuata ushauri wa mtu yoyote katika utekelezaji wa majukumu yake.
Viongozi ambao wamestaafu nyadhifa za juu serikalini visiwani hapa na wamekua wakiwania nafasi ya urais wa ni Maalim Seif (CUF) na aliyekuwa Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha (CCM).
Awali katika swali lake, Machano alihoji kwa kuwa viongozi wastaafu wanalindwa na sheria na kunufaika na mafao, serikali haioni muda umefika kwa viongozi hao kubanwa kisheria wasigombee nafasi za uongozi ikiwamo urais.
“Kama serikali haina mpango huo, haioni kwamba kuendelea kuwapa stahiki zote wakati wanaendelea kufanya siasa na kugombea nafasi za juu za uongozi wa nchi ni kutumia ovyo haki ya wananchi?” alihoji.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT