Baba yake Ben Saanane aiangukia Serikali | Bepari Classic
Breaking News
Loading...

Jumapili, 18 Desemba 2016

Baba yake Ben Saanane aiangukia Serikali

Moshi. Focus Saanane, baba mzazi wa Ben Saanane ambaye ametoweka kwa mwezi mzima sasa, ameiangukia Serikali akiisihi imtafute na kumrejesha mwanae akiwa hai.

Ben (pichani) ambaye ni msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe inasadikiwa ametoweka tangu mwanzoni mwa Novemba.

Hiyo itakuwa mara ya pili kwa familia hiyo kuomba msaada huo. Wiki tatu baada ya Ben kutoonekana, mzazi huyo alitoa ombi hilo kwa niaba ya familia katika mitandao ya kijamii, akieleza kupotea kwa kijana wao na kuomba msaada kwa Mtanzania yeyote mwenye taarifa za mahali alipo.

Juzi, akizungumza na gazeti hili, mzazi huyo alisema familia haina chombo cha uchunguzi wala mamlaka ya kufanya uchunguzi, hivyo wajibu huo unapaswa kufanywa na Serikali kwa kutumia vyombo vyake kama Jeshi la Polisi.

“Hatuna la kufanya zaidi ya kumuomba Mungu,” alisema mzazi huyo.

Alisema mara ya mwisho kuzungumza na mwanaye ilikuwa mwanzoni mwa Novemba na walizungumza kwa simu masuala ya kifamilia na hakumwambia kama alikuwa akikabiliwa na jambo baya.

Tayari wanaharakati mbalimbali pamoja na Chadema ambako anafanyika kazi, wameshaitaka Serikali ieleze kama imemkamata Ben Saanane na kama haimshikilii, basi ichunguze mawasiliano yake ya simu.

Saanane anasemekana kutoweka katika mazingira ya kutatanisha tangu Novemba 18, na juhudi za kumtafuta katika vituo vya polisi, hospitalini na vyumba vya kuhifadhia maiti zimefanyika bila mafanikio.

Jumatano, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema chama hicho kama ilivyo familia ya Ben Saanane hawajui mahali alipo na wala hawajui kama yuko hai au amekufa.

“Katika mazingira haya, tunaiomba Serikali na vyombo vyake vya ulinzi, ituambie kama imemkamata na inamshikilia Ben Saanane tuanzie hapo. Lakini kama haijamkamata na haimshikilii, Serikali na vyombo vyake watueleze mawasiliano yake ya mwisho yalikuwa lini, na nani, wapi na yalihusu nini,” alisema.

Suala la kutoweka kwa Saanane limekuwa likijadiliwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii, na ndilo linafuatiliwa kwa wingi na watu.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT