Wanafunzi sekondari Kilimanjaro waongoza kwa mimba | Bepari Classic
Breaking News
Loading...

Alhamisi, 17 Novemba 2016

Wanafunzi sekondari Kilimanjaro waongoza kwa mimba

WANAFUNZI wa shule za sekondari mkoani Kilimanjaro wanaongoza kukatishwa masomo kwa kupata ujauzito, baada ya takwimu kuonesha kuwa kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka huu, jumla ya wanafunzi 216 wamepewa ujauzito.

Wakati hiyo ikitishia mustakabali wa maisha yao ya baadaye, kwa wenzao wa shule za msingi ni tisa tu waliopewa ujauzito katika kipindi hicho kufanya jumla iwe 225.

Mkuu wa mkoa huo, Saidi Mecky Sadiki alisema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao cha Kamati ya Ushauri cha Mkoa (RCC) ambacho kimelenga kujadili masuala ya maendeleo ya mkoa katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, miundombinu, uchumi na kilimo.

“Nimelileta kwenu hili suala la ubakaji na ulawiti hususani kwa wanafunzi wetu wanaopewa mimba za utotoni ili tujadiliane na tuweke azimio madhubuti...hali ni mbaya na tukikaa kimya tutasababisha balaa kubwa na kuathiri hali ya taaluma,” alisema mkuu wa mkoa.

Pamoja na tatizo la mimba, lakini pia mkoa una upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa 1,875 ambavyo kwa shule za msingi ni vyumba 1,531 na vyumba 344 kwa sekondari.

Mkuu wa Mkoa alisema takwimu zinaonesha kuwa Wilaya ya Hai inaongoza kwa upungufu wa vyumba 493, ikifuatiwa na Same vyumba 378, Mwanga vyumba 337, Moshi vyumba 275, Siha 216, Manispaa 119 na Rombo ni vyumba 57.

Kuhusu tatizo la uharibifu wa mazingira, Sadiki alisema mwezi uliopita kumekuwepo na tatizo la wananchi kuwasha moto katika misitu ambapo jumla ya hekta 3,500 ziliungua katika Msitu wa Hifadhi ya mlima Kilimanjaro eneo la Shira, Msitu wa Chome/Shengena na Msitu wa Kindoroko.

Akizungumzia mpango wa matumizi bora ya ardhi, mkuu wa mkoa alitaka halmashauri zote kupunguza migogoro isiyo ya lazima baina ya wafugaji na wakulima huku akitaka watendaji kutoegemea upande mmoja. Alisema baadhi ya migogoro inachochewa na tabia ya watendaji kuegemea upande mmoja na hivyo kuchochea migogoro.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT