Muswada
wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali Namba 3 wa Mwaka 2016
unatarajiwa kuwasilishwa bungeni leo, ukigusa sheria tisa ikiwemo ya
Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu ambapo sasa mnufaika wa mkopo
aliyejiajiri atalipa kiasi kisichopungua Sh 120,000 au asilimia 15 ya
kipato chake, huku taasisi za umma, bodi, wakala na tume zimebanwa
zisirekebishe au kuwianisha mishahara, posho na marupurupu kwa
watumishi.
Kwa
mujibu wa muswada huo, kwenye Sheria ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu
ya Juu, waajiri wanaoshindwa kuwasilisha marejesho ya mwezi baada ya
makato wataadhibiwa, ambapo mwajiri atawajibika kuitaarifu Bodi ya
Mikopo kuhusu ajira ya mtu yeyote ambaye ana shahada au stashahada na
kukata makato ya mwezi kutoka kwenye mshahara wa mnufaika wa mkopo.
Kifungu
hicho kinapendekeza kufanya marejesho ya mkopo kuwa ya kisheria na
kupewa nafasi ya awali katika orodha ya makato na kinapendekeza
kupunguzwa idadi ya wajumbe wa Bodi ya Mikopo na kufikia saba kwa lengo
la kupunguza gharama za uendeshaji.
Kwenye
marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma, Kifungu cha 8 kinapendekeza
kufanyiwa marekebisho ili kumpa mamlaka Katibu Mkuu (Utumishi)
kurekebisha na kuwianisha mishahara, posho na marupurupu mengine kwa
watumishi wa umma.
Inapendekezwa
kumuondolea Katibu mamlaka ya kuteua watumishi wa umma wanaounda baraza
la majadiliano ya pamoja ya watumishi wa umma na sasa waziri atateua
katibu kutoka wizara yenye dhamana na kada husika ya watumishi.
Pia
inapendekezwa kufuta kifungu cha 11 ili kuondoa masharti yanayokataza
Baraza la majadiliano ya pamoja ya watumishi na baraza la pamoja la
watumishi wa umma kutoa mapendekezo kuhusu ujira.
Kwa
upande wa marekebisho ya Sheria ya Leseni na Usafirishaji, Mamlaka ya
Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kutaongezwa kifungu
ili kuweka masharti yanayoruhusu ulipwaji wa faini pale mkosaji
anapokiri kosa, badala ya kila kosa kufuata taratibu za kimahakama.
Muswada
huo una marekebisho kwenye Sheria ya Mazingira ambako kutawekwa
mwongozo wa namna ya kupima urefu wa mita 60 kwenye kingo za bahari,
ziwa, mto au bwawa la maji kinachozuiliwa kufanyia shughuli zozote za
binadamu. Upimaji utapimwa kuanzia kwenye kingo za maeneo hayo.
Sheria
nyingine zitakazofanyiwa marekebisho kwenye Mkutano wa Tano wa Bunge la
11 ni ya Usafiri wa Anga, Sheria ya Msajili wa Hazina na Sheria ya
Vipimo.
Spika
Job Ndugai wakati akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuanza
kwa Mkutano wa Tano wa Bunge wiki iliyopita, alieleza kuwa kwa wiki hii
Bunge litapokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za
Serikali(CAG) ya mwaka 2014/2015 kisha kujadili na kuishauri serikali
kuhusu Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Jumuiya ya Ulaya (EU)
na Afrika Mashariki (EPA-EU) na kisha taarifa ya kamati ndogo kuhusu
uchambuzi wa sheria ndogo.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT