Usifanye Kosa Hili Wanalofanya Wafanyabiashara Wengi Wanaoshindwa. | Bepari Classic
Breaking News
Loading...

Jumanne, 22 Novemba 2016

Usifanye Kosa Hili Wanalofanya Wafanyabiashara Wengi Wanaoshindwa.

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEizmw2xxEU7V-TbwsUfd8rBv6GHO8104z6q2nP4XmBEal8lwLcIvr0-3ngT-n9uA_hSJKCZ5UnmMs0VLOxhcbO8b3vAmYsPvzRMMXfXfqbpnQyKdgn8SZMso5xOYp8SfP_UYyN3d2T1AFpt/s1600/mja1.jpg
Je umewahi kuona wafanyabiashara ambao wameanza biashara zao chini kabisa, wanaweka juhudi kubwa na hatimaye kufanikiwa kwenye biashara hizo, lakini baadaye unaona wanaporomoka na kushindwa kabisa?
Hii ni picha ambayo ipo kwenye biashara nyingi, huenda imetokea kwako au imetokea kwa watu wa karibu kwako.
Kuna kosa moja kubwa ambao wafanyabiashara wengi wamekuwa wanalifanya, hasa pale biashara zao zinapoonesha mafanikio, na kosa hili linawarudisha nyuma na kuua biashara zao.
Wafanyabiashara wengi wanapofanikiwa kwenye biashara moja, huwa wanafikiri wanaweza kufanikiwa kwenye biashara yoyote watakayofanya. Hivyo wanatoa fedha kwenye biashara walizonazo sasa, ambazo zinaonesha kufanikiwa, na kuwekeza fedha hizo kwenye biashara mpya. Biashara hizi mpya wanakuwa hawajazijua kwa undani, ila wanaingia kwa kutumia uzoefu wao kwenye biashara walizokuwa nazo awali.
Hili ni kosa ambali limegharimu biashara nyingi, kosa ambao limewaondoa watu kwenye biashara zenye mafanikio.
Kwa nini wafanyabiashara wengi wamekuwa wanafanya kosa hili?
Sababu zipo nyingi, lakini kubwa ni ushawishi wa wale wanaowazunguka. Watu wengi wakishaona mtu amefanikiwa kwenye biashara, huwa hawaachi kumshauri, na katika ushauri wanaompa ni fursa mpya za kibiashara ambazo zimejitokeza kwa wakati huo. Baadhi ya fursa huwa zinaonekana ni nzuri na usipochukua hatua haraka unazikosa. Hili limekuwa linawasukuma wafanyabiashara kuchukua hatua za haraka na hivyo kujikuta wakitoa fedha kwenye biashara zao za sasa ili kuanzisha biashara hizo mpya.
Sababu nyingine inayowafanya watu kufanya kosa hili ni tamaa ya kufanikiwa haraka. Unapoingia kwenye biashara kwa tamaa ya kupata mafanikio ya haraka, kitu pekee unachoweza kukipata kwa haraka ni hasara na kushindwa. Kwa tamaa hizi za kupata mafanikio ya haraka, wafanyabiashara wamekuwa hawachunguzi kwa undani na hivyo kujikuta wakifanya makosa makubwa.
Ni kipi kinasababisha wafanyabiashara kushindwa pale wanapoingia kwenye biashara mpya?
Unaweza kujiuliza kwa nini mfanyabiashara ameweza kufanikiwa kwenye biashara yake ya mwanzo, ila akashindwa kwenye biashara mpya aliyoanzisha?
Sababu kubwa ni kwamba kila biashara ina changamoto zake. Kufanikiwa kwenye biashara moja hakukufanyi ujue kila biashara, kuna vitu vingi ambavyo mtu anapaswa kuvijua kwenye kila biashara mpya anayoingia. Changamoto za biashara moja hazifanani na za biashara nyingine. Wafanyabiashara wanaochukulia biashara zote ni sawa, wamekuwa wakipata hasara kubwa.
Kila biashara ina kipindi cha kujifunza na kupata hasara kabla haijaanza kutengeneza faida. Wafanyabiashara wengi hujisahau kwenye hilo na kufikiri kwa kuwa wameshakuwa na biashara inayopata faida, bali kila biashara watakayoingia itawaletea faida kubwa. Kwa kujua kwamba kuna wakati biashara itakuwa inajiendesha kwa hasara, mfanyabiashara anatakiwa kuwa makini kwenye matumizi yake ya mtaji mwanzoni mwa biashara. Wale wanaotoka kwenye biashara moja na kuanzisha nyingine, hawazingatii hilo na hivyo kujikuta wakipata hasara kubwa.
Ufanye nini ili kuondokana na kosa hili pale unapopata fursa ya kuingia kwenye biashara tofauti na unayofanya sasa?
Mara nyingi sana utazipata fursa tofauti za kibiashara, lakini siyo kila fursa inakufaa, hivyo unahitaji kuwa na njia ya kujua fursa ipi uichukue na namna gani uifanyie kazi.
Kwanza kabisa chagua aina za fursa unazoweza kuziangalia. Tunaishi kwenye dunia ambayo kila kitu kwa sasa ni fursa, kama utakuwa tayari kuchukua kila fursa inayokujia, utapata matatizo, kwa sababu fursa ni nyingi. Ni muhimu ukawa na vigezo na aina za fursa ambazo upo tayari kuzifanyia kazi au unaweza kuziangalia zaidi na nyingine ukaachana nazo kabisa.
Usiingie kwenye biashara mpya kwa lengo la kupata faida ya haraka. Ukisukumwa na lengo hilo utaishia kupata hasara.

SOMA: NAMNA YA KUWA MBUNIFU ENEO ULIPO 
Unapochagua kuingia kwenye biashara mpya, usitoe fedha ya mtaji kwenye biashara yako ya zamani. Badala yake tumia akiba uliyojiwekea kutokana na faida uliyopata kwenye biashara ya zamani. Kama huna akiba ya faida basi achana na fursa hiyo mpya. Hili ni muhimu sana kwa sababu wafanyabiashara wengi wamekuwa wakisukumwa na uzuri wa fursa kiasi cha kwenda kutoa mtaji kwenye biashara zoa za awali, baadaye biashara zote mbili zinakufa.
Unapochagua kuingia kwenye biashara nyingine mpya baada ya biashara yako ya mwanzo kuwa na mafanikio, unahitaji kuwa makini ili usiishie kuua biashara zote mbili.
PENDA BIASHARA, JIFUNZE BIASHARA.

Ukijenga utamaduni wa kutembelea mtandao huu kila siku muda si mrefu unakuwa tajiri wa mali, maarifa na afya. Kazi kwako!

Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT