Karibu sana tena katika uwanja wetu tajiri mwenzangu. Utajiri unaozungumzwa hapa sio wa akina Mengi na Bakhresa bali ni utajiri wa madini kichwani yatakayokupelekea kuwa kama akina Bakhresa kwa kuanza taratibu. Kwa moyo wangu wa upendo kwa wenzangu leo hii nimekuletea njia tatu kati ya nyingi zilizopo ambazo ni mbadala za kupata mtaji wa biashara yako. Siku za mbeleni nitakuletea nyingine. Karibu sana.
Kila ambaye anataka kuingia kwenye biashara, lakini bado hajafanya hivyo, ukimuuliza nini kinamzuia atakupa jibu mara moja; MTAJI. Mtaji unaonekana ndiyo changamoto kubwa inayowazuia wengi kuingia kwenye biashara. Na hata wale ambao tayari wameshaanza biashara, wanashindwa kuzikuza kutokana na kukosa mtaji.
Katika vitu ambavyo havipaswi kuwa changamoto kwenye biashara, cha kwanza ni mtaji. Mtaji ndiyo kitu ambacho ni rahisi sana kupata kwenye zama hizi tunazoishi. Changamoto kubwa inayowazuia wengi kuingia kwenye biashara ni utayari. Watu hawapo tayari kufanya kila wanachopaswa kufanya ili kuanzisha au kukuza biashara zao.
Linapokuja swala la mtaji wa biashara, watu hupelekea mawazo yao sehemu mbili pekee.
Sehemu ya kwanza ni akiba zao wenyewe, hapa watu huangalia ni kiasi gani cha fedha wao kama wao tayari wanacho. Kwa kuwa fedha ni changamoto kwa wengi, wanajikuta hawana fedha ya kuwatosha kuanza biashara wanazopanga kuanza, hivyo njia hii ya kwanza inashindikana.
Sehemu ya pili ni mkopo, hapa watu hufikiria kupata mkopo kwenye taasisi za kifedha kama benki na taasisi nyingine. Lakini inakuja kwamba taasisi hizi hazitoi fedha kwa sababu tu unataka, unatakiwa uwe na sifa fulani ndiyo uweze kukopesheka. Wengi wanakuwa hawana sifa hizo za kukipesheka na hivyo kugonga mwamba kwenye sehemu hii ya pili.
Wanashindwa kuanza au kukuza biashara zao kwa sababu hawajapata mtaji, hawana akiba na hawakopesheki, wanaridhika na kuishia hapo.
Swali ni je wewe upo tayari kwenda zaidi ya sababu hizo mbili? Kama ndiyo basi hapa tunakuletea njia tatu mbadala ya kupata mtaji wa biashara. Soma na fanyia kazi ili uweze kuanzisha na kukuza biashara yako.
Njia ya kwanza; kushirikiana na wengine.
Kama una wazo la biashara, ambalo unaona linaweza kuwa na mafanikio, au tayari una biashara ambayo unaona ukipata mtaji zaidi itakua sana, angalia ni watu gani ambao unaweza kushirikiana nao katika biashara hiyo. Kuna watu wengi ambao wana uwezo wa kifedha lakini hawajui ni biashara gani wafanye, au hawana muda wa kusimamia biashara zao. Wajue watu hawa katika wale watu wako wa karibu, tengeneza mpango na ongea nao huku ukiwaonesha ni namna gani watanufaika kupitia biashara hiyo.
Ukiongea na watu wengi kwa namna hii, hutakosa wachache ambao watakuwa tayari kufanya kazi na wewe. Kikubwa utakachohitaji baada ya kuwapata watu hawa ni uaminifu, nakutekeleza kile ambacho umewaahidi.
Njia ya pili; wawekezaji.
Kwa sasa kumekuwa na watu na taasisi mbalimbali ambazo zimekuwa zinawekeza kwenye biashara mbalimbali, ambazo zinaonekana kwenda vizuri. Tofauti ya uwekezaji na mkopo ni kwamba anayekukopesha anataka umrudishie mkopo wake na riba juu, ila anayewekeza kwenye biashara yako, anategemea ukipaya faida na yeye afaidike, ukipata hasara na yeye anapata hasara. Mwekezaji anakuwa sehemu ya umiliki wa biashara yako.
Angalia ni watu au taasisi gani ambazo zinawekeza kwenye biashara, na wapatie mpango wako wa biashara na namna wanavyoweza kuwekeza na kunufaika.
Njia ya tatu; ndugu, jamaa na marafiki.
Kama uko vizuri na ndugu zako, unaweza kuwaomba wakuchangie mtaji wa kuanzisha au kukuza biashara yako. changamoto kubwa kwenye jamii zetu ni kwamba watu wengi wapo tayari kuchangia harusi lakini siyo shughuli za maendeleo. Lakini pia watu hawaombi michango ya mtaji kwa nguvu kama wanavyoomba michango ya harusi.
Kama ukiandaa wazo lako vizuri, na kuongea na watu wengi wanaokuzunguka, kwa namna wanavyoweza kukusaidia kwa kiasi kidogo cha fedha, hutakosa wachache ambao watakusaidia. Kikubwa unahitaji uaminifu na kuweka juhudi kwenye biashara yako, ili watu wawe na imani na wewe.
Usilalamike tena kwamba huna mtaji wa kuanzisha au kukuza biashara yako, badala yake tumia njia hizo tatu kupata mtaji wa biashara yako.
Kama ulivyofurahia kujifunza hiki basi mshirikishe na wenzio wapate maarifa haya na Mungu atakupanulia mafanikio yako. Karibu tena.
https://telegram.me/joinchat/AswM6T8wMmAXKdneD-7mcQ
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT