Mpemba wa meno ya tembo kortini | Bepari Classic
Breaking News
Loading...

Alhamisi, 17 Novemba 2016

Mpemba wa meno ya tembo kortini

MFANYABIASHARA Yusuf Ali Yusuf, maarufu ‘Mpemba’ na wenzake watano, wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kukutwa na meno ya tembo yenye thamani ya Sh milioni 392.8.

Jamhuri imeweka wazi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, kwamba inatarajia kuihamishia kesi hiyo katika Mahakama ya Rushwa na Uhujumu Uchumi (Mahakama ya Mafisadi), baada ya kuwasomea washtakiwa maelezo.

Mpemba na wenzake, walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana wakikabiliwa na mashtaka manne ya uhujumu uchumi.

Akiwasomea mashtaka, Wakili wa Serikali, Paul Kadushi, aliwataja washtakiwa kuwa ni Mpemba, Charles Mrutu maarufu Mangi Mapikipiki na Mangi Mpare, Ahmed Nyagongo, Pius Kulagwa, Benedict Kungwa na Jumanne Chima, maarufu Jizzo au JK.

Kadushi alidai washtakiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari 2014 na Oktoba 2016 maeneo ya Dar es Salaam, Morogoro, Iringa, Tanga na Mtwara, kwa pamoja na wenzao ambao hawapo mahakamani, walikutwa wakijihusisha na biashara ya nyara za Serikali.

Inadaiwa washtakiwa walikutwa na meno 50 ya tembo ambayo ni sawa na tembo 25, yenye thamani ya Sh 392,817,600 mali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania bila kibali.

Shtaka la pili, washtakiwa wanadaiwa Oktoba 26, mwaka huu maeneo ya Mbagala Zakhem wilayani Temeke, walikutwa na meno 10 ya tembo yenye uzito wa kilo 13.85 yakiwa na thamani ya Sh 65,469,600.

Katika shtaka la tatu, washtakiwa hao wanadaiwa Oktoba 27, mwaka huu maeneo ya Tabata Kisukulu, walikutwa na meno manne ya tembo yenye uzito wa kilo 11.1 yakiwa na thamani ya Sh 32,734,800 bila kibali.

“Mheshimiwa hakimu, shtaka la nne, washtakiwa wote wanadaiwa Oktoba 29, mwaka huu, maeneo ya Tabata Kisukulu, bila kibali walikutwa na meno 36 ya tembo yenye uzito wa kilo 58.55 yakiwa na thamani ya Sh 294,613,200,” alidai.

Mpemba (35) mkazi wa Tegeta, Charles (37) mkazi wa Mlimba Morogoro, Benedict (40), mkazi wa Mbagala Chamazi, Jumanne (30) mkazi wa Mbezi Msakuzi, Ahmed (33) mkazi wa Vikindu Mkuranga na Pius (46) mkazi wa Temeke, baada ya kusomewa mashtaka hawakutakiwa kujibu.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Wakili Kadushi aliifahamisha mahakama kuwa upelelezi umekamilika, wanaomba wapewe muda wa kuandaa maelezo ya kesi kisha waihamishie Mahakama ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Kesi hiyo mpya ambayo ni ya kwanza kuhamia katika mahakama hiyo, iliahirishwa na Hakimu Simba hadi Desemba mosi kwa ajili ya kutajwa.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT