Ludewa. Ukiwa umepita mwaka mmoja tangu kifo cha aliyekuwa mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe, mjane, wazazi na wakazi wa jimbo hilo wamefanya ibada ya kumkumbuka ambayo imeibua upya simanzi.
Filikunjombe alifariki dunia Oktoba 15, 2015 katika ajali ya helikopta iliyoanguka na kulipuka katika Hifadhi ya Taifa ya Selous mkoani Morogoro wakati akitokea Dar es Salaam kwenda Ludewa mkoani Njombe. Wengine waliokufa katika ajali hiyo ni Egid Nkwera (43), Casablanca Haule (53) na William Silaa, aliyekuwa rubani wa helikopta hiyo.
Akizungumza wakati wa ibada hiyo, mjane huyo, Sarah alisema: “Huwa namuota mara kwa mara na hali hiyo inanifanya nizidi kumuombea kwa Mungu ampumzishe kwa amani.”
Aliishukuru familia ya marehemu kwa kuendelea kumpa mahitaji muhimu na kusomesha watoto.
Sarah ambaye wakati wa uhai wa mumewe alikuwa mama wa nyumbani, kwa sasa ameanzisha kilimo cha matunda na mbogamboga ili kuongeza kipato chake.
Philip Filikunjombe ambaye ni mdogo wa marehemu, amesema kifo cha kaka yake kimemuachia mzigo wa kutunza familia tatu ikiwamo yake na wazazi wake (Deo).
Mbali ya kutunza familia hizo, pia anaendelea kusomesha zaidi ya watu 700 ambao walikuwa wakilipiwa ada na kaka yake wakati wa uhai wake.
Mkazi wa Ludewa, Ludende Mgimba alisema kifo cha Filikunjombe kilizima nuru ya maendeleo ya haraka aliyokuwa nayo kwa wakazi wa jimbo hilo.
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya wa Ludewa, Juma Madaha amesema anamkumbuka Filikunjombe kutokana na ujasiri na mapenzi aliyokuwa nao kwa wananchi wake.
Ibada hiyo ilifanyika Kanisa Katoliki la Ludewa kuanzia asubuhi na kufuatiwa na chakula cha mchana nyumbani kwa Filikunjombe, Mtaa wa Ibani
0 comments:
POST A COMMENT