BOMBA la gesi asilia kutoka mkoani Mtwara hadi jijini Dar es Salaam lililokamilika ujenzi wake mwaka jana limekabidhiwa rasmi kwa Kampuni ya Tanzania ya Kusambaza Gesi (GASCO).
Aidha baada ya kitendo hicho uunganishaji wa gesi majumbani unatarajiwa kuanza mwakani.
Makabidhiano hayo yalifanyika jana jijini Dar es Salaam baina ya Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Kapuulya Musomba na Makamu Meneja Mkuu wa Kampuni ya China Petroleum Pipeline (CPP), Joseph Zhang Hongilei waliokuwa wakifanya kazi ya kutandaza bomba hilo.
Hatua hiyo inatoa fursa kuunganisha matoleo yaliyopo katika maeneo ya Mtwara, Mkuranga, Lindi, Kilwa na Dar es Salaam ambapo matumizi ya gesi hiyo majumbani inatarajiwa kuanza kuunganishwa mapema mwakani. Musomba alisema baada ya kukabidhiwa bomba hilo, GASCO wataanza kusambaza gesi maeneo mbalimbali, ikiwemo majumbani.
Alisema katika usambazaji gesi katika viwanda na makampuni wanatarajia kuunganisha katika maeneo matano ikiwemo Kiwanda cha Vigae, Kiwanda cha Bakhresa eneo la Mkuranga na Kiwanda cha Dangote Mtwara ambapo mazungumzo yatakamilika baada ya wiki mbili.
Alisema maeneo mengine ni Eneo huru la Uwekezaji (EPZA) Bagamoyo ambapo walianza mazungumzo na viwanda vya eneo hilo juzi.
0 comments:
POST A COMMENT