MAMBA ni mnyama anayekula nyama, huweza kuishi nchi kavu lakini maisha
yake kwa kiasi kikubwa hupendelea kukaa majini, tofauti na fikra za watu
wengi ambao hufikiri mamba anazaa ukweli ni kwamba huwa anataga, ambapo
kwa wastani hutaga mayai 35 mpaka 50, najua utajiuliza sasa huyu kiumbe
anaatamia vipi wakati maisha yake ni ya heka heka? Mamba hutengeneza
kiota kwa kuchimba pembezoni mwa mto au ziwa na kisha kufukia mayai yake
mpaka hapo ambapo mayai yatakapokuwa tayari.
Mayai yake yanapokuwa tayari kwa kutoa watoto, mamba husikia sauti na
akiyatoa mayai hayo katika kiota watoto wake hujitoa wenyewe, yaani
watoto hutumia nguvu binafsi na kuvunja gamba la yai, kisha hutoka
katika ulimwengu mpya, kazi ya mama kwa wakati huo inakuwa ni
kuhakikisha anawachukua wanawe na kuwapeleka majini na huwabeba kwa
kutumia mdomo wake.
Wakati huu baadhi ya wanyama ambao huliwa na mamba nao hulipiza kisasi,
mfano kenge, mijusi wakubwa pamoja na ndege, humtegea anapopeleka watoto
wa awamu ya kwanza wale wanaosalia hujeruhiwa vibaya, au kubebwa kama
chakula na wanyonge wa mamba. Hujisikia tabu kiasi kwamba anapoibuka
katika maji huwatazama kwa jicho la shari.
Watoto wa mamba ukiwaona katika udogo wao wanashangaza, hutokaa ufikirie
kwamba ndio hao wafikapo ukubwani hufikia urefu wa futi 10 na zaidi,
uzito wa kilo zaidi ya 600, ni viumbe ambao huonekana wadogo unaweza
kuhisi labda ni kenge.
Katika hatua za mwanzo watoto wa mamba hutumia samaki kama chakula chao,
kwa kadri muda unavyokwenda watoto hao nao huanza kuwinda wanyama na
zoezi hilo huwa jepesi kwa kuwa idadi kubwa ya wanyama hufuata maji
katika makazi yao, mnyama mkubwa ambaye maisha yake huathiriwa na mamba
ni nyumbu na hii ni kwa sababu pindi wanyama hawa wafikapo mtoni
hukamatwa kwa urahisi kwa kukosa tahadhari ya kutosha.
Kwa taarifa yako, mamba ni miongoni mwa wanyama wakubwa duniani, meno
yake yamejipanga kwa mfano wa msumeno, ana macho makubwa, ngozi ngumu na
mkia mrefu ambao humsaidia katika kuwinda, hupendelea kukaa kwenye maji
lakini jua linapochomoza na linapo karibia kuzama, ndio wakati hutoka
majini na kukaa nchi kavu.
Ajabu ya mnyama huyu ni moja, pamoja kwamba wanyama wanaokula nyama tu
ndio huishi muda mfupi, lakini yeye maisha yake ni marefu anaweza kufika
miaka 50 na zaidi. Namna unayoweza kuwatofautisha kwa jinsia zao ni
muonekano wao, dume huwa mrefu zaidi ya jike pia huwa mzito zaidi jike.
SIFA ZAKE ZA KIPEKEE
1. Ni mnyama ambaye ana uwezo mzuri na mkubwa katika kuyamudu maji hasa kuogelea.
2. Huishi katika maji baridi na makazi yake huweka sehemu zisizo na kina kirefu.
3. Mashambulizi yake ni ya kushtukiza, anaweza akawa anakuvizia na usijue kwamba yupo jirani kukukamata.
4. Ana akili na mjanja mno anapomuona mnyama ambaye hana uwezo wa kumkimbiza, hujifanya amelala usingizi ili uingie katika maji.
5. Pia anaweza kukukamata hata akiwa amelala usingizi, jicho lake moja
huacha wazi anapolala na lina uwezo wa kufikisha taarifa ya kila
kinachoendelea.
6. Huwa na nguvu maradufu awapo kwenye maji, ni vigumu kumshinda katika mapambano naye ndani ya maji.
7. Hapatani na simba kabisa kwa kuwa ndiye mnyama ambaye hupenda
kumbughuzi awapo mapumzikoni, hivyo wawili hawa wanapokutana nchi kavu
huwa kama watani.
8. Ni mwepesi wa kuzira kitu, hapendi kujitesa anapokutana na changamoto huamua kukaa pembeni.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT