Wabunge wandamizi nchini Marekani wamemvaa Rais Donald Trump kwa kumtaka
asalimishe kanda ya mazungumzo yoyote yaliorekodiwa kati yake na
aliyekuwa mkurugenzi wa shirika la FBI, James Comey aliyemfuta kazi.
Kiongozi wa Chama cha Democrats katika Bunge la Seneti, Charles Schumer
alionya kuwa uharibifu wa kanda hizo utakuwa uvunjaji wa sheria.
Naye Seneta wa Republican, Lindset Graham alisema kuwa Ikulu ya
Whitehouse inahitaji kuwa wazi kuhusu iwapo kulikuwa na kanda zozote za
rekodi za mazungumzo hayo au la.
Matamshi hayo yanajiri baada ya Rais Trump kusema katika mtandao wake wa
Twitter matamshi yanayoonekana kuwa vitisho kwa mkuu huyo wa zamani wa
FBI. Alimuonya Comey wiki iliopita dhidi ya kuzungumza na vyombo vya
habari akisema natumai hakuna rekodi za mazungumzo yetu.
Ikulu ya Whitehouse haijathibitisha wala kukana kuwepo kwa kanda hizo.
Bwana Schumer pia alionya kwamba masenata wa chama cha Democrats
watakataa kumuunga mkurugenzi mpya wa FBI hadi pale mtaalam
atakapochaguliwa kuchunguza hatua ya Urusi kuingilia maswala ya Marekani
katika uchaguzi uliopita.
FBI inachunguza madai hayo pamoja na ushirikiano wa Urusi na kampeni ya
rais Trump ambapo hata hivyo rais huyo amekana uhusiano wowote na
anasema bwana Comey amemhakikishia kwamba hachunguzwi.
Anasema kuwa alimpiga kalamu bwana Comey kwa sababu alikuwa ameshindwa kufanya kazi vizuri.
Wanachama wa Democrats wameshutumu Trump kwa kumfuta kazi Comey ili kujaribu kusitisha uchunguzi wa FBI.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT