
MMOJA wa wazazi ambao watoto wao wamefariki katika ajali ya gari
iliyosababisha vifo vya wanafunzi 33 wa Shule ya Msingi Lucky Vincent,
alikuwa miongoni mwa mashuhuda wa ajali hiyo pasipo kujua kama mtoto
wake, Justine Alex, alikuwamo katika msafara wa gari hilo.
Mzazi huyo, aliyetambulika kwa jina la Lemburis Saruni, inadaiwa kuwa
alishuhudia ajali hiyo akiwa kwenye gari la nyuma, huku lile
lililobeba wanafunzi hao likiwa mbele.
Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, ndugu wa karibu na Lemburis ambaye
hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema baada ya kuona gari hilo
limeanguka kwenye korongo alilazimika kushuka ili kwenda kuangalia bila
kujua kama mtoto wake ni miongoni mwa waathirika wa ajali.
“Hiyo ajali imeua ndugu zangu, akiwamo mtoto wa baba yangu mdogo, na
yeye leo alikuwa anakwenda Ngorongoro, alifuatana na hilo basi la
wanafunzi bila kujua na kaliona likidondoka, akashuka akalifuata
akakuta mwanawe ndio yupo ananing'inia mlangoni,” alisema ndugu huyo.
Alisema baada ya kumuona akiwa katika hali hiyo, alilazimika kumwondoa
na kumuweka pembeni, lakini kwa bahati mbaya alikufa akiwa amemshika
mkononi.
Alisema Justine alikuwa mtoto pekee wa Lemburis. Alisema mama wa Justine alifariki dunia mwaka juzi.
Gazeti hili lilijaribu kumtafuta mzazi huyo kwa njia ya simu ya
kiganjani ili aweze kuelezea tukio hilo, lakini hakupatikana hewani.
Mbali na mtoto huyo, mtoa taarifa alibainisha kuwa ajali hiyo huenda
ikawa imesababisha vifo vya ndugu zao wengine watano ambao walikuwapo
katika msafara huo, ambao ni wanafunzi na walimu.
Credit - Mtanzania
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT