
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema wanachama na
viongozi wake 215 wamefunguliwa kesi katika mahakama mbalimbali nchini
tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Chadema imesema wanachama hao wamepandishwa kizimbani katika jumla ya
kesi 78 huku wengi wao wakinyimwa dhamana na wale waliopatikana na
hatia, walipewa adhabu za vifungo bila ya kupewa fursa ya faini.
Kutokana na hali hiyo Chadema inatarajia kuandaa orodha itakayoainisha
kesi zote za jinai ambazo bado zipo mahakamani pamoja na kuonyesha aina
ya mashtaka na vifungo vilivyotolewa, kwa vyombo vya habari na taasisi
za ndani na nje ya nchi.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari aliyasema hayo
jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mrejesho wa kikao
cha kamati ndogo ya Kamati Kuu ya Chadema kilichokaa Jumanne.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 25, 2015 Rais John Magufuli wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliibuka mshindi kwa kupata kura 8,882,935
sawa na asilimia 58.46 ya kura zote halali.
Nafasi ya pili ilishikwa na mgombea wa Chadema aliyeungwa mkono na
mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa
aliyepata kura 6,728,480 sawa na asilimia 39.97.
Prof. Safari alisema mara baada ya Uchaguzi Mkuu huo kumalizika,
viongozi wa Chadema wamekuwa wakikamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya
kubambikizwa; kwa kisingizio cha uchochezi.
“Hivi sasa umekuwa ni mtindo kwa mahakama kuwakatalia dhamana wanachama
wa Chadema bila ya sababu za msingi," alisema Prof. Safari.
"Pia imekuwa ni mtindo kuwahukumu vifungo bila kuwapa fursa ya kulipa faini.”
Prof. Safari alisema katika kikao hicho cha kamati kimetoa wito kwa
mhimili wa Mahakama kutekeleza wajibu wake kwa weledi uliotukuka;
kuhakikisha kuwa haki inatendeka bila kuwapo kwa vitisho kutoka kwa mtu
yeyote.
“Majaji wanapaswa kuiga mfano wa uhuru wa Mahakama na weledi wa majaji
wa Afrika Kusini, Zimbabwe na Marekani ambao waliweza kutengua amri
batili zilizotolewa na marais wa nchi zao,” alisema Prof. Safari.
Aidha, Profesa Safari alisema Kamati Kuu imetoa wito kwa mawakili
kuchukua wajibu mkubwa kuisaidia mahakama kutekeleza majukumu yake kwa
weledi kwa kuhakikisha haki inatendeka bila woga, vitisho au vishawishi,
pamoja na kutokukubali kutishwa na mtu au asasi yoyote katika kuitetea,
kuilinda Katiba na sheria za nchi.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT