
Wanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamesema
wamemshauri Mwenyekiti wao wa Taifa, Freeman Mbowe, asiende kuripoti
polisi leo.
Mwanasheria wa Chadema, John Mallya, amesema Mbowe hatakwenda kuripoti
polisi leo kwa sababu amefungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu, Kanda ya
Dar es Salaam na inaanza kusikilizwa Februari 21 mwaka huu.
“Mbowe haendi polisi, tumemshauri asiende kwa sababu kesi yake inaanza kusikilizwa Jumanne (kesho).
“Kama wanamhitaji, waje keshokutwa (kesho) Mahakama Kuu, watampata hapo,”alisema Mallya.
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema yuko Mwanza na hajawasiliana na Mbowe.
“Hapa niko Mwanza sijawasiliana na mwenyekiti, lakini kama nikiwasiliana naye, nitamshauri asiende huko polisi.
“Kwa hiyo, naweza kusema kilichofanywa na Kamishna Sirro si wito wa
kipolisi bali ni siasa kama ambavyo alifanya Makonda kwa kutangaza
majina ya watu hadharani.
“Wito wa polisi huwa ni wa kimaandishi, hawajamwandikia barua, hawajampigia simu.
“Hawa maafande wana namba zetu za simu sisi kama mawakili wa chama, kama
wanamhitaji Mbowe kwanini wasitupigie simu mpaka watangaze kwenye
vyombo vya habari,”alihoji Lissu.
Alipoulizwa kama Mbowe atakamatwa wakati wowote kuanzia sasa, Lissu
alisema watalazimika kulishtaki mahakamani Jeshi la Polisi kwa kitendo
hicho.
“Hatuwezi kukubali utaratibu huu, waache kufanya siasa, wakimhitaji
mwenyekiti wetu wamwandikie barua,”alisema Lissu ambaye pia ni Mbunge wa
Singida Mashariki.
Mwanzoni mwa mwezi huu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda,
alitaja majina 65 ya watu wanaodaiwa kujihusisha na biashara ya dawa za
kulevya akiwamo Mbowe.
Pamoja na kutaja majina hayo, Makonda aliwaagiza watuhumiwa hao kuripoti
Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa dhidi ya
tuhuma hizo.
Februari 10 mwaka huu, akiwa mjini Dodoma, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa
Hai, alizungumza na waandishi wa habari na kusema hajawahi kujihusisha
kwa namna yoyote na biashara ya dawa za kulevya na pia hatakwenda polisi
kuhojiwa kama alivyoagizwa na Makonda.
Hata hivyo, alisema atakwenda polisi, kama jeshi hilo litafuata taratibu za kumuita kwa mujibu wa sheria.
“Siwezi kwenda polisi kwa wito wa Makonda kwa sababu hana mamlaka hiyo
kisheria. Kama polisi wananihitaji, waniite kwa kufuata utaratibu,
nitakwenda kwa sababu mimi siogopi kwenda polisi,”alisema Mbowe.
Wakati Mbowe akisema hayo, juzi Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar
es Salaam, Simon Sirro, alisema Jeshi la Polisi linamtafuta Mbowe na
kwamba limeshindwa kumpata kwa sababu amezima simu.
Kutokana na hali hiyo, Kamanda Sirro alitoa saa 48 kwa Mbowe kuripoti
polisi na endapo hatafanya hivyo atatafutwa kwa namna ambayo jeshi hilo
litaona inafaa.
“Jumatatu (leo) asiporipoti kutakuwa hakuna namna ya kulizuia tena Jeshi la Polisi kutafuta namna ya kumhoji.
“Mbaya zaidi juzi tumejitahidi kumtafuta hapatikani, tulikwenda
nyumbani kwake hakupatikana, tulikwenda mahali anakoishi sasa, pia
hakupatikana,”alisema Sirro
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT