Serikali yatangaza Jumamosi ya pili ya mwezi ni ya mazoezi | Bepari Classic
Breaking News
Loading...

Jumapili, 18 Desemba 2016

Serikali yatangaza Jumamosi ya pili ya mwezi ni ya mazoezi

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inaunga mkono kampeni ya kudhibiti na kuzuia magonjwa yasiyo ya kuambukiza iliyozinduliwa jana jijini hapa.

Pia, ametangaza kuwa kila Jumamosi ya pili ya kila mwezi, itatumika kwa watu kufanya mazoezi.

Suluhu aliyasema hayo alipokuwa anafungua kampeni hiyo ambayo imeanzia jijini hapa, kisha itaendelea nchi nzima.

Alisema kampeni hiyo itaisaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza gharama za kutibu wagonjwa saratani na figo kwa kuteua siku moja kila mwezi ya kufanya mazoezi.

“Nawashauri wananchi kufanya mazoezi kwa kuanzisha na kujiunga na vikundi vya mazoezi, Serikali itatimiza wajibu wake wa kuweka mazingira mazuri ya kufanya mazoezi maeneo yote nchini,” alisema Samia.

Aliwagiza pia watendaji wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kurudisha mchakamchaka shuleni kwa utaratibu maalumu kwa kuwa utasaidia kuimarisha afya za wanafunzi na kukabiliana na magonjwa mbalimbali.

“Vijana wa sasa ni masharobaro, wanavaa nguo ambazo hazitaki watembee umbali mrefu bila kupanda magari, mchakamchaka ukirudi utawasaidia kuwakuza wanafunzi ili wapende mazoezi,” alisema Samia.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema kampeni hiyo itakuwa endelevu mkoa kwa mkoa ili kuhakikisha wagonjwa wanapungua na itakuwa ni sehemu ya kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

“Katika malengo 17 ya SDGs, matatu yanazungumzia juu ya nchi kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ili ifikapo mwaka 2020, tuwe tumepunguza moja ya tatu ya vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa kukinga, kutibu na kuzingatia afya ya akili,” alisema Ummy.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT