Akizungumza wakati wa mazishi ya mtoto wake, mzazi wa kijana huyo, Juma
Sleym, alisema kabla ya kuuawa Isihaka alikodiwa na watu wasiojulikana
Desemba 10, mwaka huu, lakini hakurudi tena mpaka Desemba 11, mwaka huu
bajaji yake ilipoonekana ikiwa pembezoni mwa barabara kuu ya lami.
Alisema baada ya kuiona bajaji hiyo walianza kumtafuta mtoto wake na
kuupata mwili wake ukiwa umefichwa kichakani huku shingo ikiwa
imenyongwa na kichwa kikiwa kimepigwa kwa kitu kizito.
Kufuatia tukio hilo, wananchi waligoma kuuzika mwili wa marehemu,
wakimtaka Mkuu wa Polisi Igunga, Mayala Kepha, kwenda msibani hapo ili
atoe maelezo juu ya matukio ya kuuawa waendesha bajaji kushamiri na
kushindwa kuwakamata wauaji.
Hata hivyo, baada ya umati huo kumsubiri mkuu huyo wa polisi kwa muda
mrefu bila mafanikio, walikwenda barabara kuu ya lami ilipokutwa
pikipiki ya marehemu na kufunga barabara kwa kuweka mawe, magogo na
matawi ya miti.
Hali hiyo ilisababisha magari zaidi ya 400 kutoka Dar es Salaam na
Mwanza kukwama katika eneo hilo kuanzia saa 6:15 hadi saa 11:00 jioni
hadi pale polisi wilaya ya Igunga walipoenda kuwatawanya kwa kupiga
mabomu ya machozi mfululizo, lakini bila ya mafanikio na kulazimika
kuomba msaada wa kuongezewa askari wengine kutoka mkoani Tabora.
Baada ya polisi kupiga mabomu kwa wingi, wananchi hao walitawanyika na kuwezesha magari yaliyozuiliwa kuendelea na safari zao.
Baadhi ya madereva waliokwama katika eneo hilo, Selemani Issa na Salum
Hussein, walisema ni vyema Jeshi la Polisi likakaa meza moja na wananchi
wa Igunga ili kudhibiti matukio kama hayo yasijirudie.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi walioshiriki mazishi ya mwendesha
huyo bodaboda, Ramadhani Hussein, Moshi Haruna, Ras Karetus walisema
wameamua kufunga barabara kwa sababu Agosti, mwaka huu aliuawa mwendesha
bajaji mwingine, Alex Okungu, lakini polisi Igunga wameshindwa
kuwakamata wahalifu na kumtaka waziri wa mambo ya ndani ya nchi amuondoe
mkuu wa polisi wilayani humo.
Diwani wa Kata ya Igunga, Charles Bomani, alisema wananchi walikuwa
watulivu, lakini kutofika kwa mkuu polisi ndiyo kuliwaongezea machungu
na kuamua kwenda kufunga barabara na kuongeza kuwa yeye kama diwani
hayuko tayari kuona wananchi wake wakipoteza maisha huku polisi
wakishindwa kuwakamata wauaji.
Naye Mbunge wa Manonga, Hamis Seif Gulamali, alisema polisi hawakupaswa
kutumia nguvu kubwa kwani wananchi hao wasingechukua hatua hiyo endapo
mkuu huyo wa polisi angefika kwenye msiba na kuzungumza nao na kwamba
suala hilo ameliwasilisha katika mamlaka husika ili kujua ufumbuzi wake.
Mganga Mfawidhi Hospitali ya Wilaya ya Igunga, Marchades Magongo,
amethibitisha kupokea mwili wa kijana huyo na kusema kuwa chanzo cha
kifo chake ni kutokana na ubongo kutikisika kutokana na mashambulizi
aliyoyapata.
Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Hamisi Issa, ili
kuzungumzia tukio hilo hazikuzaa matunda baada ya kupigiwa simu yake ya
mkononi bila ya kupokelewa.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT