Meya Ubungo afichua siri ya Ukawa, RC Makonda | Bepari Classic
Breaking News
Loading...

Ijumaa, 9 Desemba 2016

Meya Ubungo afichua siri ya Ukawa, RC Makonda

Dar es Salaam. Meya wa Ubungo, Boniface Jacob amesema Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekosa mbinu za kushirikisha wapinzani ndiyo maana wanasusa kushirikiana naye.

Jacob alitoa kauli hiyo juzi wakati wa mahojiano na gazeti hili yaliyofanyika ofisi za Mwananchi Communications Limited (MCL), ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake kwa vyombo vya habari anayoiita ya kuitangaza wilaya mpya ya Ubungo na mipaka yake.

Alisema hakuna kitu kibaya baina yake na Makonda isipokuwa kiongozi huyo hana mbinu shirikishi katika utendaji kazi wake, ikiwamo kuwashirikisha wapinzani.

“Siyo Jacob tu, hata baadhi ya wabunge wapinzani. Hutokuja kumuona (Halima) Mdee, (John) Mnyika na (Saed) Kubenea wakihudhuria shughuli aliyoiandaa Makonda tangu alipochaguliwa hadi atakapotoka.

“Huu ni udhaifu wake mwenyewe, siyo wa wapinzani. Ila Rais (John) Magufuli akinialika nitakwenda kwa sababu anatambua umuhimu wangu,” alisema.

Hivi karibuni, Makonda alifanya ziara za kusikiliza kero katika wilaya tano za Dar es Salaam, lakini katika baadhi ya maeneo alikopita, ikiwamo Ubungo wapinzani walikacha kuhudhuria.

Hiyo haikuwa mara ya kwanza kumsusia Makonda baada ya madiwani na wabunge wa Ukawa wa Kinondoni kususia kikao cha madiwani wa Dar es Salaam alichoikitisha katika ukumbi wa Arnaoutoglou, Agosti mwaka huu.

Sababu za kususa zilizotolewa na madiwani hao wakiongozwa na Jacob ni kwamba Makonda hana uhusiano mzuri na wapinzani.

Hata hivyo, Makonda alijibu kwamba siyo kazi yake kuhesabu watu kubaini nani hakufika katika kikao hicho.

Jacob alisema matatizo ya kutoelewana na Makonda yalianza tangu mkuu wa mkoa huyo akiwa mkuu wa Wilaya Kinondoni wakati yeye akiwa meya wa Manispaa ya Kinondoni.

“Katika utendaji kazi wangu siwezi kwenda sehemu ambayo DC (mkuu wa wilaya) anakwenda kutumika wakati meya nipo.

“Tafsiri yake huyo mtu anataka kufanya kazi na DC (mkuu wa wilaya) na siyo meya. Kwa hiyo nikienda nitakuwa pambo, ndiyo maana ishu zote katika vikao vyao wanaohojiwa ni wakuu wa wilaya,” alisema Jacob.

Hata hivyo, Jacob alisema maagizo ya utekelezaji wanayopewa na mkuu wa mkoa baadhi yake ni lazima yapitie kwenye baraza la madiwani ambako meya ndiye mwenye mamlaka.

“Kama huna uhusiano mzuri na wapinzani mwisho wa siku mkakati wako utakwama,” alisisitiza.

Alipoulizwa kwa utaratibu huo matatizo ya wananchi wanatatuaje? alijibu:

“Kila mtu ana ilani yake na wananchi wanajua hila na mbinu zinazofanyika dhidi ya wapinzani. Hivyo hawashangai kutotuona wapinzani. Mimi nina bajeti kupitia halmashauri ambayo inashughulika na kutatua kero mbalimbali za wananchi na hakuna atakayeniingilia.

“Hata hivyo, kama una uhusiano mzuri na DC mnaweza kushirikiana vizuri kutatua kero za wananchi kupitia bajeti za halmshauri.”



Uhusiano wake na Hapi, Polepole

Mbali ya kutokuelewana na Makonda, Jacob alikuwa na mtazamo tofauti kuhusu wakuu wa wilaya za Ubungo na Kinondoni.

Diwani huyo wa Kata ya Ubungo (Chadema), alimtaja Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi kuwa ni mmoja wa viongozi aliofanya nao kazi vizuri.

“Mtu mwingine ninayefanya naye kazi vizuri ni Hamphrey Polepole (Mkuu wa Wilaya Ubungo). Siyo mtu wa majivuno wala kujipambanua na ameweka masilahi ya wananchi mbele,” alisema.

Jacob anaongoza manispaa mpya ya Ubungo iliyoanzishwa mwaka jana baada ya kugawanywa ile ya Kinondoni.

Jacob alisema wilaya hiyo mpya ya Ubungo inategemea kukusanya mapato kutoka katika kata tano kati ya 14 ambazo ni Ubungo, Sinza, Manzese, Makuburi na Kimara.

Alisema Kata ya Ubungo ina viwanda vingi wakati Sinza ina hoteli, Manzese kunafanyika shughuli mbalimbali za kiuchumi wakati Makuburi na Kimara zinakaliwa na watu wenye uchumi wa kati.

Jacob alisema Manispaa ya Ubungo imepanga kukusanya Sh38 bilioni kwa mwaka na kwamba ana uhakika watafikia lengo kutokana na vyanzo vya kodi 42 vilivyopo.

“Miongoni mwa vyanzo hivyo ni majengo, ushuru wa huduma za jiji na masoko, leseni za biashara, uwekezaji na masoko,” alisema.

Alisema kwa sasa ofisi za Manispaa ya Ubungo zipo maeneo ya Kibamba kwa muda na ifikapo mwakani zitahamia Kata ya Kwembe.

Wakati manispaa hiyo mpya ikiendelea kusaka vyanzo vipya vya fedha, Meya huyo alisema uamuzi wa kuzitaka daladala za Mlandizi na Msata ziishie Kituo cha Mbezi, umesababisha hasara kati ya Sh8 milioni hadi Sh9 milioni kwa mwezi.

“Daladala hizi zingekuwa zinakwenda hadi Kituo cha Mawasiliano, tungepata ushuru huu. Pia wafanyabiashara wa kituo hiki wangefaidika lakini hali ni tofauti,” alisema.

Alisema kwamba Kituo cha Mbezi kipo chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na siyo Halmashauri ya Ubungo, hivyo hawapati mapato mengi.

Sanjari na hilo, meya huyo alifichua kwamba eneo la Manzese limepangwa kuwa mahususi kwa kuendelezwa majengo ya maghorofa kwa sababu ya unyeti wake wa kibiashara.

“Manzese inaitwa kwa jina tu. Lakini mpango huu unajumuisha Sinza, Mabibo na Manzese yenyewe na michoro imeshaandaliwa,” alisema.



Ubungo inaanzia wapi?

Jacob ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alifafanua pia kuhusu suala la mipaka baina ya Ubungo na wilaya Kinondoni ili kuondoa mkanganyiko.

Meya huyo aliitaja baadhi ya mipaka kati ya Ubungo na Kinondoni, kuwa ni eneo la Hoteli ya Friends Corner.

Akieleza kuwa kwa upande wa kulia, kama unaelekea Magomeni unafika hadi kona ya kwenda kwa Sheikh Yahya Hussein ambako kuna njia ya kuelekea Mburahati kwamba ndiyo mpaka kati ya Ubungo na Kinondoni.

Wakati ukienda na Barabara ya Sam Nujoma, eneo la Mlimani City ndipo ulipo mpaka. Pia Sinza eneo la Kituo cha Mafuta cha Big Bon ni mpaka mwingine kati ya wilaya hizo.

Hata hivyo, Jacob alisema ingawa Ubungo ina kata chache lakini ina eneo kubwa na watu wengine tofauti na fikra za watu.

Alisema halmashauri yake imejipanga ipasavyo kuhakikisha kwamba wilaya hiyo inakuwa ya kisasa.

Pia, aliwataka wakazi wa Ubungo kuwa makini na mipaka ili wasije kujichanganya ikiwamo suala la ulipaji kodi kutokana na ukaribu wa wilaya hizo mbili.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT