JPM aitwa kusimamisha bomoabomoa Kivule | Bepari Classic
Breaking News
Loading...

Jumanne, 13 Desemba 2016

JPM aitwa kusimamisha bomoabomoa Kivule

Dar es Salaam. Wakazi wa mtaa wa Magole A, Kata ya Kivule wamemuomba Rais John Magufuli kuingilia kati ubomoaji wa nyumba unaoendelea katika eneo lao na kuwakosesha makazi maelfu ya wananchi.

Wakazi hao wamesema wao ni Watanzania wanyonge, hivyo wanahitaji kuangaliwa kwa huruma na kiongozi huyo kama alivyofanya kwa wamachinga wa Mwanza hivi karibuni.

Akizungumzia ubomoaji wa nyumba ulioendelea jana, Mwenyekiti wa kamati ya maafa ya waathirika hao, Abdul Majengo alisema wanashangaa kuona hakuna kiongozi yeyote wa Serikali aliyeingilia kati suala hilo.

Majengo alisema walikwenda ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala wakaambiwa siyo eneo la Ilala, hata ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke nako waliambiwa hivyo hivyo, jambo linalowafanya washindwe kufikisha kilio chao serikalini.

“Tunataka Rais Magufuli atusaidie katika hili, hapa kuna kaya za Watanzania zaidi ya 700 ambazo sasa hawana makazi. Rais hawezi kushindwa na alishasema hataki kuona wanyonge wanaonewa,” alisema.

Alisisitiza kwamba hadi sasa hawajui mipaka halisi ya eneo linalotakiwa kubomolewa, pia watu ambao hawajabomolewa wanaishi kwa hofu na kushindwa kuendelea na ujenzi.

Wakielezea tukio hilo huku wakiangua vilio, wanawake waliobomolewa nyumba zao walisema wamekuwa wakimbizi kwenye nchi yao wakati ina sifa ya kuhifadhi wakimbizi.

Mkazi wa Magole A, Fatuma Abdallah alidai bomoabomoa hiyo inaendeshwa kisiasa kwa sababu diwani na mbunge wao wanatoka upinzani.

Hata hivyo, alisema Rais Magufuli aliahidi kwamba atakuwa kiongozi wa wote bila kujali itikadi za vyama vyao, lakini sasa wanashangaa kuona Serikali ikikaa kimya huku wao wakiendelea kubomolewa.

“Mimi nimeishi hapa kwa miaka saba, leo wananiambia nimevamia wakati Serikali ya mtaa iliidhinisha wakati nimenunua kiwanja na asilimia 10 nikalipia. Nashangaa Serikali hii hii inasema tumevamia,” alisema huku akilia.

Mama huyo mwenye watoto wanne alisema amekuwa na maisha magumu baada ya kubomolewa nyumba yake na sasa hana makazi mazuri na watoto wake hawaendi shule kama zamani.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT