Hekaheka za uchaguzi kuanza Jumamosi | Bepari Classic
Breaking News
Loading...

Jumanne, 6 Desemba 2016

Hekaheka za uchaguzi kuanza Jumamosi

UCHAGUZI mdogo wa Mbunge wa Jimbo la Dimani, wilaya ya Mjini Magharibi na madiwani katika kata 22 nchini, utafanyika Januari 22 mwakani ambapo uchukuaji fomu utaanza Jumamosi ijayo.

Uteuzi wa wagombea utafanyika Desemba 22 mwaka huu huku kampeni zikianza Desemba 23 hadi Januari 21 mwakani.

Taarifa ya Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva ilieleza kuwa Tume hiyo itaendesha uchaguzi mdogo kujaza nafasi ya ubunge katika jimbo la Dimani, Zanzibar kutokana na kifo cha Mbunge wa jimbo hilo.

Mbunge wa Jimbo hilo, Tahir Ali Hafidh alifariki Novemba 11, mwaka huu mjini Dodoma alikokuwa katika mkutano wa Bunge baada ya kuugua ghafla. Alisema pia wataendesha uchaguzi mdogo kwa nafasi 22 za Udiwani zilizoachwa wazi kwa sababu mbalimbali kwa baadhi ya halmashauri za Tanzania Bara.

Alizitaja kata hizo na mikoa ziliko kwenye mabano kuwa ni Ng’hambi na Ihumwa (Dodoma), Kiwanja cha Ndege (Morogoro) Igambavanu, Ikweha (Iringa), Ngarenanyuki na Mateves (Arusha), Kijichi (Dar es Salaam), Kinampundu (Singida), Isagehe (Shinyanga) na Kasansa (Katavi).

Nyingine ni Malya na Kahumulo (Mwanza), Maguu na Tanga (Ruvuma), Kamwani (Kagera), Nkome (Geita), Lembeni (Kilimanjaro), Mkoma (Mara), Duru (Manyara), Mwamtani (Simiyu) na Misugusugu (Pwani).

Wakati huo huo, Baraza la Vyama vya Siasa limetangaza kufanyika kwa uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo utakaofanyika Desemba 19 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na Sisty Nyahoza kwa niaba ya Katibu wa baraza hilo, ilieleza kuwa fomu kwa ajili ya uchaguzi huo unaofanyika kwa mujibu wa kanuni za baraza zitatolewa kuanzia Desemba 7 mwaka huu katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa jijini Dar es Salaam na zinatakiwa kurejeshwa kabla ya Desemba 12 mwaka huu saa tisa na nusu mchana.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT