Gwajima kujitetea kesi kuhusu bastola, risasi 17 | Bepari Classic
Breaking News
Loading...

Ijumaa, 2 Desemba 2016

Gwajima kujitetea kesi kuhusu bastola, risasi 17

Dar es Salaam. Kesi ya kushindwa kuhifadhi silaha inayomkabili Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na wenzake watatu imefikia hatua ya kuanza kujitetea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Washtakiwa hao sasa wataanza kujitetea katika mahakama hiyo Desemba 13, 2016 dhidi ya mashtaka yanayowakabili.

Hatua hiyo, imefikiwa baada ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Cyprian Mkeha kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka na vielelezo na kuwaona washtakiwa hao wana kesi ya kujibu na wanapaswa kujitetea.

Baada ya uamuzi huo wa Hakimu Mkeha,  wakili wao, Peter Kibatala aliiambia mahakama kuwa wateja wake watajitetea kwa njia ya kiapo na wataita mashahidi watatu.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Mkeha alisema siku hiyo watasikiliza ushahidi wa utetezi wa washtakiwa wote wanne na mashahidi wao watatu.

Mbali na Gwajima, washtakiwa wengine ni  Askofu Msaidizi,  Yekonia Bihagaze, mfanyabiashara Gerge Mzava  na mkazi wa Kimara Baruti, Geofrey Milulu.

Awali, shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, Koplo Sospiter kutoka ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, alidai alikuwa  mmoja wa waliomlinda Askofu Gwajima alipokuwa amelazwa  Hospitali ya TMJ, Mikocheni chumba namba 213.

Koplo Sospiter aliiomba Mahakama ipokee  vitu vilivyokuwamo ndani ya begi linalodaiwa la Gwajima ambavyo ni  chupi nyeusi aina ya boksa, suruali mbili, makoti mawili, bastola moja, soksi pea mbili, risasi tatu zilizokuwa katika kasha lake, Ipad moja na CD mbili.

Vingine ni risasi 17 za bastola, vitabu viwili vya kumiliki silaha na hati ya kusafiria ya askofu huyo.

Mahakama ilivipokea kama sehemu ya ushahidi katika kesi hiyo kwa kuwa hakukuwa na pingamizi kutoka upande wa utetezi.

Koplo Sospiter alidai kuwa Machi 28, 2015 mkuu wake wa kazi  ambaye ni Mkuu wa Upalelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Constantine Massawe alimpangia kazi ya ulinzi ya kumlinda askofu huyo hospitalini hapo .

Alidai akiwa na askari mwenzake aliyemtaja kwa jina la Ben, Machi 29, 2015,  saa tisa usiku, watu watatu ambao ni mshtakiwa wa pili hadi wa nne walifika hospitalini hapo  huku mmoja wao akiburuza begi la kijani hadi karibu ya mlango wa kuingilia katika wodi aliyolazwa Gwajima.

Shahidi huyo alidai alipowahoji kilichomo ndani ya begi,  walimjibu asitake kujua mambo yao.

Alidai majibu hayo yalimpa shaka na kuhisi kwamba kuna kitu ambacho si cha kawaida, akawasiliana na bosi wake Massawe na kumueleza hali halisi ikiwamo kuomba nguvu ya ziada.

Alidai kuwa ndani ya robo saa lilikuja gari la askari wa doria akiwamo Koplo Magesa na baadaye ASP Hafidhi na kuwaweka chini ya ulinzi, wakawahoji na kulifungua begi ambapo walikuta vitu hivyo.

Mpelelezi kutoka ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Sajenti Abogasti (46) alidai kuwa washtakiwa Bihagaze, Mzava  na Milulu walipeleka   silaha saa nane usiku katika Hospitali ya TMJ alipokuwa amelazwa Askofu Gwajima baada ya kubaini kwamba walikuwa nayo kinyume cha sheria.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT