Mbinu Nane (8) Za Kuanza Siku Yako Kwa, Furaha, Hamasa Ya Hali Ya Juu Ili Kuwa Na Mafanikio Makubwa. | Bepari Classic
Breaking News
Loading...

Jumanne, 8 Novemba 2016

Mbinu Nane (8) Za Kuanza Siku Yako Kwa, Furaha, Hamasa Ya Hali Ya Juu Ili Kuwa Na Mafanikio Makubwa.

Habari mpendwa rafiki na msomaji wa BEPARI CLASSIC? Natumaini unaendelea vema kabisa na pole kwa majukumu lakini pia na changamoto unazokutana nazo hupaswi kukata tamaa bali zipokee na kabiliana nazo kwani ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Karibu mpenzi msomaji tujifunze kwa pamoja.

Hali ya watu kukosa tumaini la maisha na kukata tamaa katika maisha limekuwa ni wimbi kubwa katika jamii zetu. Kukata tamaa katika jambo lolote linaanzia na jinsi ulivyoianza siku yako, jinsi unavyoyachukulia mambo kwa mitazamo tofauti aidha chanya au hasi. Kama ni mtu wa kuamini katika uwezekano uko sehemu salama na kama uko katika hali ya kutoamini katika uwezekano wa mambo na kuona mambo hayawezekani uko sehemu ya hatari. 
Leseni ya kuweza kufika pale unapotaka kwenda unayo wewe mwenyewe. Leseni ya kuamka utoke kwenye giza na kwenda kwenye mwanga iko mikononi mwako. Upo duniani kufurahia zawadi ya uhai, hujaja duniani kuishi kwa mateso na leseni ya kuingia katika maisha ya furaha na kutoka katika maisha ya mateso iko mikononi mwako. 
Mabadiliko yoyote katika maisha yako yanahitaji leseni moja tu nayo ni maamuzi. Kama uko katika chumba kilichofungwa madirisha na milango halafu unajisaidia haja zote humo humo basi, hali ya hewa ya chumba hicho kitakua ni mbaya. Hivyo basi, badala ya kulalamika hali ya hewa imekua mbaya na dunia imekua mbaya basi fanya maamuzi ya kukifanya chumba chako kuwa sehemu salama ya kuishi. Kuna matatizo mengine yako ndani ya uwezo badala ya kulalamika fanya maamuzi ya kutatua usisubiri mhisani aje akutatulie matatizo yako. 


Kwa hiyo, ndugu msomaji, matatizo ya mtu yanatatuliwa na mtu mwenyewe kwani hakuna mtu anayejua matatizo ya mtu zaidi ya yeye mwenyewe. Na hakuna mtu anayeweza kutatua matatizo ya mtu ndio maana kuna msemo unasema ya ngoswe muachie ngoswe. 
Ndugu msomaji, karibu katika somo letu la leo ambapo tutajifunza mbinu za kuanza siku yako kwa hamasa ya hali ya juu na mafanikio makubwa. Na zifuatazo ni mbinu za kuanza siku yako
kwa furaha na hamasa ya hali ya juu na mafanikio makubwa; 

1. Kuamka Mapema Alfajiri; Kwanza kuamka mapema inaleta afya ya akili, mwili na kadhalika. ukitaka kuanza siku yako kwa furaha, hamasa na mafanikio makubwa siku yako amka mapema. Lala mapema na amka mapema ili mwili wako uweze kupata mapumziko mazuri kwa ajili ya uzalishaji wa siku inayofuata. Mtu anayeamka mapema alfajiri anakua na uwanja mpana wa kuianza siku yake kwa furaha na hamasa ya hali ya juu. Ukichelewa kuamka utaanza kukimbizana na muda na hutofanya mambo yako kwa ustadi wa hali ya juu na kuipangilia siku yako. Unapoamka asubuhi unaweza kuchagua kua na furaha au kutokua na furaha. Kama umeharibu asubuhi umeharibu siku yako nzima.

2. Fanya Juhudi, Sala, Tafakari (Meditation); kama unaweza kusali na kufanya tafakari katika hali ya ukimya fanya. Hakikisha akili yako haihami katika jambo lako husika na kwenda nje ya mada. Hii itakusaidia kua huru kiakili hata kimwili hatimaye ujihisi mwenye furaha na amani. Akili yako inahitaji kupata muda wa ukimya ambao ni tafakari. Tafakari inakusaidia kupata kuisikia sauti yako ya ndani inasema nini. Hivyo, hii itakusaidia kuanza siku yako kwa furaha na hamasa kubwa.

3. Soma Kitabu/Sikiliza Vitabu Vilivyosomwa; Utamaduni wa watu wengi kusoma kwao ni wakati wakiwa shule tu baada ya kumaliza anakua amefunga kila kitu. Jijengee utamaduni wa kusoma kila siku asubuhi kabla kelele za dunia hazijaanza. Lisha akili yako chakula cha kutosha ambacho ni maarifa. Unatakiwa kukua kiroho, kimwili na kiakili. Sasa huwezi kukua kiakili kama husomi vitabu. Jinoe tafadhali, usiridhike na maarifa uliyonayo. Kama hujawahi kusafiri na kuijua dunia basi anza kusoma vitabu utasafiri na kuzijua nchi nyingi na vitu vingi. Unatakiwa kubadilika kila siku kama vile kalenda inavyobadilika.


4. Usisikilize Habari; Kama unataka kuanza siku yako hovyo basi anza kusikiliza habari, uchambuzi wa magazeti nk. Habari hazitakusaidia bali zitakuhubiria vitu ambavyo vitakwenda kuharibu siku yako na hatimaye kukusababishia kukosa furaha na hamasa ya kwenda kutekeleza majukumu yako kwa ufanisi wa hali ya juu. Ni vema usikilize hata sauti za hamasa au nyimbo za hamasa zinazokupa furaha na hamasa kuliko kuanza siku na kusikiliza nyimbo za huzuni. Huwezi kuondoa huzuni kwa kusikiliza nyimbo za huzuni. Kwa kifupi, epuka kusikiliza mambo hasi yote yatakayoharibu siku yako.
http://beparilakihaya.blogspot.com

5. Jinenee Maneno Chanya (Affirmation);Kile ambacho unajiambia kila siku na kujithibitishia ndiyo kinachotokea katika maisha yako mara nyingi. Kama unapenda kujiambia wewe una bahati kila siku utakua na bahati, kama unajiambia wewe ni mtu wa nuksi tu na mikosi tu basi utakua hivyo. Hivyo jihadhari sana na ulimi wako kwani kinaumba kile unachosema. Pendelea kujiambia mambo chanya na siyo hasi. Kwa mfano, katika kikundi cha kisima cha maarifa kupitia mtandao wao whatsapp huwa wanaanza siku yao kwa kujinenea maneno chanya kama vile leo ni siku bora sana kwangu, namshukuru Mungu kwa zawadi hii nakwenda kufanya kilicho bora na nategemea kupata kilicho bora, kwa kusimamia misingi ya uaminifu, kujituma na nidhamu. Kwa hiyo ukijiambia kila siku maneno hayo asubuhi utakua wapi baada ya mwezi mmoja? Lazima utabadilika utakua unajipa leseni ya kuwa mwana mafanikio bora na kuachana na kulalamika hovyo. Mwandishi Makirita aliwahi kuandika hivi katika moja ya tafakari zake ambazo anatoa kila siku asubuhi ‘’kila siku fikiria na jiambie maneno chanya kama;
Ø Ninaweza kufanya makubwa kwenye maisha yangu.
Ø Leo ni siku bora sana kwangu, nakwenda kufanya makubwa na nategemea kupata matokeo bora.
Ø Nina bahati nzuri kila wakati, mambo yangu yanakwenda vizuri kila mara.
Ø Mimi ni mwana mafanikio, kila siku kwangu ni siku ya kufanikiwa.
Ø Duniani ni sehemu bora sana ya kuishi, na mimi nakwenda kuifanya izidi kuwa bora zaidi.’’ Unaweza kuziona na kudharau kauli kama hizo lakini anza leo kujiambia halafu utaona mabadiliko chanya yatakavyokuja kwenye maisha yako. 


6. Usianze Siku Yako Kwa Kutembelea Mitandao ya Kijamii; Mitandao ya kijamii siku hizi imekua ikihubiri habari hasi sana na kukatisha tamaa watu wengi sana. Mtu anapoanza siku yake kwa kufungulia mtandao wa kijamii na kukuta habari ya kuumiza moyo na kuona wenzake wakifanya vitu Fulani na kuweka matukio ya picha ambayo mara nyingi siyo maisha yao halisi. Watu wanavyoona mtu anaweka picha katika mitandao ya kijamii na kuweka mazuri akija kujilinganisha na yeye mwenyewe anajikuta anaingia katika shimo la maisha ya maigizo na mwishowe kukata tamaa, wivu nakadhalika.
 
 7. Andaa Ratiba Ya Siku Nzima; Kuanza siku bila ratiba ni sawa na kujenga nyumba bila kuwa na msingi. Msingi wa siku yako unaanza na kuweka ratiba. Orodhesha mambo utakayofanya na mpango kazi wako wa siku nzima. Kwa kufanya hivi utakua umewasha moto mzuri wa hamasa na kuifanya siku yako kuwa bora sana.
8.  Maliza Siku Yako Kwa Kuifanyia Tathimini; hapa sasa ndio unafanya tafakari je siku yako ilikuwaje? Ilikwendaje? Unajiuliza maswali na kujipima ili kupata mrejesho wa siku yako nzima kulingana na ratiba yako uliyojiwekea.

Mwisho, jiamini wewe ni mshindi na hakuna mtu kama wewe duniani kote, una kitu ulichonacho ndani yako ambacho ni msaada kwa dunia hivyo itoe hiyo hazina uliyonayo. Usisubiri ruhusa anza hapo hapo ulipo. Huwezi kuwa mchoraji mzuri kama hujaionesha dunia kuwa unachora. Una thamani kubwa ndani yako ambayo mtu mwingine hana itoe na acha kulalamika kwani kulalamika ni utamaduni unaozalisha wavivu wengi. 
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepedeokessy.dk@gmail.com

Siku zote wanaofanikiwa ni wale wasio na roho ya kupata peke yao. Nakuomba na wewe usiwe na roho hiyo ili upate mafanikio kirahisi sana kwa kushea ukurasa huu na wengine na wapate kitu kutokana na makala hii. Siku iwe njema kwako. 
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT