JITIHADA za Rais John Magufuli katika kubana matumizi yasiyo ya lazima
serikalini, ambazo alizihamishia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC), ikiwamo kuzuia safari zisizo za lazima katika jumuiya hiyo,
zimewezesha kuokoa zaidi ya Sh bilioni 1.2.
Rais Magufuli ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na aliahidi
kuchukua hatua za kubana matumizi yasiyo ya lazima na ikibidi kutumbua
watendaji wa EAC, baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo Machi mwaka
huu jijini Arusha.
Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Liberat Mfumukeko alisema jana jijini hapa
kuwa jitihada za kubana matumizi yasiyo ya lazima, zimeokoa Dola za
Marekani 588,768 (zaidi ya Sh bilioni 1.2) ndani ya kipindi cha miezi
mitatu kuanzia Mei hadi Agosti mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa mara ya kwanza tangu ashike
wadhifa huo Aprili mwaka huu, Balozi Mfumukeko alisema kiasi hicho cha
fedha kiliokolewa kutokana na kubana safari zisizo za lazima za
watumishi na watendaji wa jumuiya katika kipindi hicho.
“Utekelezaji wa ubanaji wa matumizi yasiyo ya lazima unategemewa kuokoa
dola za Marekani milioni sita kwa mwaka huu wa fedha 2016/2017 na
tutakuwa tunatoa taarifa hizi kwa watu wa Afrika Mashariki kila baada ya
muda,” alisema Balozi Mfumukeko ambaye ni Katibu Mkuu wa Tano wa EAC.
Kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa makubaliano mbalimbali ya jumuiya
hiyo, Balozi Mfumukeko alieleza kwamba utekelezaji unaendelea vyema
pamoja na changamoto mbalimbali zinazojitokeza.
Alisema katika utekelezaji wa kuwa na vituo vya ukaguzi wa mizigo vya
pamoja mipakani, vituo 10 kati ya 15 vinatekeleza ukaguzi huo kwa
mafanikio na kupunguza gharama za kufanya biashara.
“Kutokana na vituo hivyo kuanza kazi, hivi sasa kusafirisha mizigo
kutoka Mombasa hadi Kampala inachukua siku nne badala ya siku 20 za
awali, jambo linalowasaidia wasafirishaji kupunguza gharama za kufanya
biashara,” alisisitiza.
Tangu alipoingia madarakani, Rais Magufuli amedhibiti mianya ya rushwa
ikiwemo kupunguza safari za nje pamoja na kutumbua majipu mbalimbali kwa
nia ya kubana matumizi sanjari na kuhakikisha kila mtu ananufaika na
matunda ya nchi yake pamoja na kurejesha heshima ya kazi kwa watumishi
wa umma.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT